Friday, March 6, 2020

TANI 31 ZA MIFUKO YA PLASTIKI KUTEKEKEZWA SONGWE



Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila mapema leo akizindua zoezi la uteketezaji wa mifuko ya plastiki ambapo tani 9 kati ya 31 zimeteketezwa katika kichomea taka kilichopo katika Mgodi wa Dhahabu wa Shanta New Luika uliopo Wilayani Songwe.
Sehemu ya tani 9 kati ya 31 za Mifuko ya plastiki ikiteketezwa katika kichomea taka kilichopo katika Mgodi wa Dhahabu wa Shanta New Luika uliopo Wilayani Songwe.
Maafisa wa Mgodi wa Dhahabu wa Shanta New Luika uliopo Wilayani Songwe wakihakikisha Sehemu ya tani 9 kati ya 31 za Mifuko ya plastiki zinateketezwa katika kichomea taka kilichopo mgodini hapo ikiwa ni uzinduzi wa uteketezaji wa mifuko hiyo kwa Nyanda za Juu Kusini.
Sehemu ya tani 9 kati ya 31 za Mifuko ya plastiki iliyokamatwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kabla ya kuteketezwa katika kichomea taka kilichopo katika Mgodi wa Dhahabu wa Shanta New Luika uliopo Wilayani Songwe.
……………………………………………………………………………………….
Tani 31 za Mifuko ya Plastiki iliyo kusanywa kutoka Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha Mikoa ya Songwe, Mbeya, Iringa na Njombe itateketezwa Mkoani Songwe ikiwa ni utekelezaji wa katazo la
serikali la matumizi ya mifuko ya plastiski isiyo ya lazima.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila mapema leo amezindua zoezi la uteketezaji wa mifuko ya plastiki ambapo tani 9 kati ya 31 zimeteketezwa katika kichomea taka kilichopo katika Mgodi wa Dhahabu wa Shanta New Luika uliopo Wilayani Songwe.
Kafulila amesema licha ya athari nyingi za kiafya kama vile kusababisha magonjwa ya saratani, taka za plastiki zinazoingia katika vyanzo vya maji zinaipelekea dunia kupoteza takribani dola trilioni 2.5 lakini pia tafiti zinabainisha kuwa taka hizo huharibu ubora wa ardhi.
Amesema Serikali ya Tanzania imekuwa kinara wa kutunza mazingira na maliasili kwa kuwa asilimia 70 ya wananchi hutegemea maliasili katika kuendesha maisha yao jambo ambalo ni la kumpongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli.
Ameongeza kuwa  Mkoa wa Songwe utaendelea kusimamia utekelezaji wa agizo la Serikali ya awamu ya tano ambalo linalenga utunzaji wa mazingira huku akisisitiza ngazi zote za uongozi kuanzia Vijiji, halmashauri na Mkoa kushirikiana katika kutekeleza agizo hilo ili kulinda taifa letu kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo.
Naye Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Anorld Mapinduzi amesema katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki lilianza kutumika rasmi  Juni 01, 2019 na lilitangazwa katika gazeti la serikali namba 349.
Mapinduzi amesema serikali imeruhusu baadhi ya bidhaa zifungashwe na sio kubebewa katika Mifuko ya plastiki na bidhaa hizo ni pamoja na baadhi ya dawa na vifaa tiba, baadhi ya vyakula na mbolea ambavyo visipo fungashwa katika plastiki vitapoteza ubora wake.
Ameongeza kuwa wananchi wasidanganyike kuwa mifuko laini ya plastiki imeruhusuiwa kwani serikali imeruhusu tu matumizi ya vifungashio vya plastiki ambavyo hutengenezwa maalumu kwa ajili ya bidhaa husika, vina nembo ya bidhaa iliyo fungashwa na vitatengenezwa kabla ya bidhaa kuingizwa sokoni.
Mapinduzi amesema lengo la kuteketeza rasmi mifuko ya plastiki ni kutoa ujumbe kwa wananchi waendelee kutambua kuwa serikali bado inapinga matumizi ya mifuko plastiki ambayo ina athari nyingi kwa taifa pia kaguzi mbalimbali zinaendelea na watakao kamatwa adhabu zitatolewa kwa mujibu wa sheria.
Menenja Mazingira wa Mgodi wa Dhahabu wa Shanta New Luika Washington Onyango amesema wako tayari kushirikiana na serikali katika kutunza mazingira na pia uwepo wa kichomea taka katika Mgodi huo ambacho kina ubora utawezesha uteketezaji wa taka katika Mkoa wa Songwe.
Onyango amesema uwezo wa kichomea taka katika mgodi huo ni kuchoma takataka tani moja kwa siku lakini taka ambazo huzalishwa na kuchomwa mgodini hapo ni tani tatu mpaka nne tu jambo ambalo hufanya kichomea taka hicho kufanya kazi chini ya kiwango huku kikiwa  ni rafiki wa mazingira kwakuwa hakiruhusu kemikali kusambaa.

No comments :

Post a Comment