Uzinduzi Rasmi: Makamu wa Rais
Samia Suluhu Hassan (wapili kulia), akikata utepe kuzindua tawi la 225
la benki ya NMB lililopo Busega mkoani Simiyu akiwa pamoja na Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Ashatu Kijaji( watatu kulia), Mbunge wa
Busega, Raphael Chegeni na Kaimu Mkurugenzi wa benki hiyo Ruth Zaipuna
(pili kushoto). Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka. Kabla ya
tawi hili la NMB Busega kuzinduliwa, wananchi walilazimika kusafiri
hadi Magu takribani kilomita Zaidi ya 30 kupata huduma za kibenki.
Kaimu Mkurugenzi wa NMB Ruth Zaipuna, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa tawi la Busega Mkoani Simiyu.
Salaam bila kupeana mikono:
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan (kushoto) akisalimiana na Mjumbe wa
Bodi ya NMB Mathias Magwanya (wa nne kulia) akiwa ameambatana na Kaimu
Mkurugenzi wa benki hiyo Ruth Zaipuna pamoja na wafanyakazi wengine wa
Benki hiyo. Kabla ya tawi hili la NMB Busega kuzinduliwa, wananchi
walilazimika kusafiri hadi Magu takribani kilomita Zaidi ya 30 kupata
huduma za kibenki.
*************************
Benki
ya NMB imezindua tawi jipya Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu na kufikisha
matawi 225 nchi nzima huku ikitangaza neema ya huduma bora na mikopo
nafuu kwa wananchi wakiwemo wakulima, wafugaji na wavuvi kusaidia
shughuli za kiuchumi.
Akitoa
taarifa ya utendaji wa benki hiyo kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu
Hassan wakati wa hafla ya ufunguzi wa tawi hilo mwishoni mwa wiki, Kaimu
Mkurugenzi mtendaji wa NMB, Ruth Zaipuna alisema ufunguzi wa tawi hilo
pamoja na mengine maeneo ya vijijini ni utekelezaji sera huduma jumuishi
ya kifedha kwa makundi yote ya kijamii hadi vijijini.
Alitaja baadhi ya huduma jumuishi
zinazotolewa na benki hiyo hadi katika ngazi ya wilaya, kata na vijiji
kupitia mawakala kuwa ni pamoja na mikopo ya mitaji kwa wafanyabiashara
wadogo, kati na wakubwa, pembejeo kwa wakulima na aina zote za bima
kuanzia ya afya, vyombo vya usafirishaji na ujenzi wa nyumba bora.
Alisema
pamoja na huduma za kibenki ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, NMB pia
inatoa huduma ya aina zote za bima, malipo kwa njia ya mtandao na elimu
ya usimamizi wa fedha kwa wakulima kupitia vyama vyao vya msingi vya
ushirika (Amcos) kupitia NMB Foundation.
“NMB imetoa mikopo kwa Amcos 202 kati ya 383 za mkoa wa Simiyu,” alisema Zaipuna.
Alisema
kupitia huduma ya NMB Mkononi, wateja wa benki hiyo wataweza kufungua
akaunti kupitia simu zao za kiganjani bila kulazimika kwenda benki na
kuwaomba wananchi walioko maeneo ambako hakuna matawi ya benki
kuchangamkia fursa.
Akizindua
tawi hilo, Makamu wa Rais Mhe. Samia Hassan Suluhu alisema uimara na
huduma ya sekta ya fedha ni mhimili muhimu katika katika maendeleo na
uchumi wa Taifa na kuzitaka mabenki na taasisi za fedha kuimarisha
shughuli zao huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira
bora na wezeshi kuendeleza sekta hiyo.
Aliipongeza
Benki ya NMB kwa uendeshaji mzuri unaoiwezesha kupata faida na hivyo
kuiwezesha Serikali kuvuna zaidi ya shilingi bilioni 586 kupitia kodi na
ushuru mbalimbali.
Makamu
wa Rais pia aliishukuru NMB kwa kutenga na kutumia zaidi ya shilingi
bilioni 5 kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia sera ya
kurejesha sehemu ya faida kwa jamii.
No comments :
Post a Comment