Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe akifungua
Mkutano wa Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi na Wadau wa Utatu wa Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika
katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Machi 2, 2020
Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wakifuatilia
hotuba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu,
Maafisa Waandamizi na Wadau wa Utatu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuelekea Mkutano wa Mawaziri wa SADC
sekta ya Kazi na Ajira.
Naibu Katibu Mtendaji mwenye
dhamana ya Utangamano wa Kikanda, Dkt. Thembinkosi Mhlongo (wa pili
kutoka kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano (Kulia) ni Katibu Mkuu,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew
Massawe. Kushoto ni Mwakilishi wa Sekretarieti ya SADC, Bw. Maxwell
Parakokwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kijamii na Rasilimali Watu SADC Bi.
Duduzile Simelane.
Sehemu ya Wajumbe wa Mkutano huo
wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika Mkutano huo wa
Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya
Kazi na Ajira.
Mkurugenzi wa
Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bw. Ally Msaki akielezea jambo kuhusu masula ya
ajira wakati wa Mkutano huo. Kushoto ni Kamishna wa Kazi – Ofisi ya
Waziri Mkuu Kanali Francis Mbindi.
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
………………………………………………………………………………………………………
Na; Mwandishi Wetu
Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimejizatiti kuimarisha
Sera na kujenga mipango ya pamoja itakayowezesha kukuza ajira kwa vijana
katika Ukanda huo.
Akifungua Mkutano
wa Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi na Wadau wa Utatu wa
Jumuiya hiyo
wanaosimamia Sekta ya Kazi na Ajira hii leo Machi 2, 2020 Katibu Mkuu,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu Bw. Andrew Massawe alisema kuwa Mkutano huo umewakutanisha
Wataalamu wa sekta ya Kazi na Ajira kwa lengo la kuandaa nyaraka
mbalimbali zitakazo jadiliwa katika Mkutano wa Mawaziri ambao
utafunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 5 hadi 6 Machi, 2020 katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Alieleza kuwa
ajenda zitakazo jadiliwa ni pamoja na masuala ya kisera kuhusu ukuzaji
wa ajira kwa vijana, pia masuala yanayohusisha uhamaji wa nguvu kazi
ndani ya jumuiya ya SADC ambapo itasaidia pia kutoa fursa ya kukuza
ajira kwa nguvukazi ya nchi wanachama.
“Itambulike kuwa
uimarishwaji wa sera katika sekta ya kazi na ajira utasaidia kwa kasi
kikubwa kuwa chachu ya maendeleo ya nchi wanachama wa Jumuiya ya
maendeleo kusini mwa afrika endapo itasimamiwa vizuri,” Alisema Massawe
Aliongeza kuwa
kauli mbiu ya Mkutano huo isemayo “Kukuza Soko la Ajira na Mahusiano
Mema Sehemu za Kazi kwa Maendeleo Endelevu” inaelezea umuhimu wa sekta
ya kazi na ajira katika kuongeza tija ya ukuaji wa soko la ajira kwa
nchi wanachama.
Naye Naibu Katibu
Mtendaji mwenye dhamana ya Utangamano wa Kikanda, Dkt. Thembinkosi
Mhlongo alieleza kuwa mapendekezo yaliyotolewa katika mkutano
uliofanyika mwezi Novemba 20, 2019 ulioshirikisha wataalamu na wadau wa
utatu umechangia katika kujenga miongozo sahihi na sera zitakazo
wawezesha nchi wanachama wa SADC kukuza sekta ya kazi na ajira.
Kwa Upande wake
Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bw. Ally Msaki alisema kuwa
Mkutano wa Mawaziri utakao funguliwa rasmi tarehe 5 Machi, 2020
utawawezesha Mawaziri wa Nchi wanachama wa SADC kujadili kwa pamoja
ajenda mbalimbali zitakazokuwa zimepitiwa kwenye kikao cha wataalam kwa
lengo la kuimarisha sekta ya kazi na ajira nchini na jumuiya hiyo kwa
ujumla.
Hadi sasa Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zilizoshiriki
katika Mkutano huo ni Angola, Afrika Kusini, Botswana, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Namibia,
Eswatini, Lesotho, Jamhuri ya Shelisheli na Tanzania.
No comments :
Post a Comment