Mkurugenzi
wa Kituo cha Faraja Singida, Sr Catherine Grady (wa kwanza kulia) akiwa
na baadhi ya wafanyakazi wa kituo hicho kwenye banda lao la maonyesho
katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, eneo la shule ya
sekondari Mwenge mkoani Singida jana.
Mgeni
rasmi wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa mkoa wa Singida,
Aysharose Mattembe akisikiliza jambo kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa
Faraja Centre kwenye kilele cha siku ya wanawake mkoani Singida jana.
Baadhi ya watoa huduma wa Kituo cha Faraja mkoani hapa.
Na Godwin Myovela, Singida
SUALA
la kupambana na biashara haramu ya ulanguzi wa binadamu sambamba na
kusaidia watoto waishio katika mazingira magumu vinapaswa kupewa msukumo
wa kipekee kuanzia ngazi ya kaya mpaka taifa ili kulinda wahanga-
hususani makundi ya watoto na wasichana ambao wengi wao hujikuta
wakitumbukia katika majanga mbalimbali ikiwemo kupata maambukizi ya
VVU/UKIMWI kwa kigezo cha umaskini.
Akizungumza
kwenye kilele cha siku ya wanawake, mkoani hapa jana, mratibu wa Mradi
kutoka Kituo cha Faraja, Stella Mwagowa alisema Kituo hicho kwa
kushirikiana na serikali, pamoja na Shirika lisilo la kiserikali la
‘CHTEA’ lililopo nchini Kenya wamefanikiwa kuokoa wahanga wapatao 8 na
wengine 5 nje ya Tanzania ambao tayari walikuwa wamelanguliwa.
“Watoto
wengi wamekuwa wakichukuliwa majumbani na kupelekwa kusikojulikana kwa
kigezo cha kwenda kutafutiwa ajira, lakini ukijaribu kufuatilia utakuta
wengi huishia kupelekwa kwenye majumba ya starehe, na wengine
kufanyishwa biashara za ukahaba kwenye maeneo mbalimbali kama kivutio
cha biashara za watu kinyume na matarajio na bila ridhaa yao,” alisema.
Mwagowa
aliwataka wazazi na jamii, na hasa kwenye ngazi ya mtaa kuwa na uelewa
katika utambuzi na ufuatiliaji wa kina kujua wanapomtoa mtoto ndani ya
familia au mtaa ni lazima mzazi awe na uhakika kujua mtoto anapokwenda.
Katika
kukabiliana na tatizo la biashara haramu, pamoja na mambo mengine,
alisema kituo cha Faraja kimejikita katika kutoa elimu na kuhamasisha
kwenye uongozi ngazi za mitaa ili ikiwezekana kabla mtoto hajaondoka
basi sharti uongozi wa mtaa husika upewe taarifa.
Lakini
pia kupitia kituo hicho kumeanzishwa Jukwaa la wadau wakiwemo Kituo
cha Faraja, Jeshi la Polisi, Ustawi wa Jamii, Takukuru, Serikali za
Mitaa, Wajasiriamali, Uhamiaji , Hospitali na wadau wengine, ambalo
pamoja na mambo mengine, azma yake ni kufanya kazi kwa pamoja na umoja
katika kuhakikisha kesi zote zinazoibuliwa na kusajiliwa kuhusiana na
biashara haramu ya ulanguzi wa binadamu na madhara ya ukatili wake
haziishii njiani.
“Pia
kwa baadhi ya shule za msingi na sekondari ndani ya manispaa ya Singida
tayari tumeanzisha “clubs” za wanafunzi, mambo haya ya mtoto kupewa
pipi, biskuti kisha anaishia kubakwa hayakubaliki! tunaendelea kutoa
elimu kwa wanafunzi, viongozi wa dini, makanisa na misikiti zikiwa ni
shabaha za kusambaza jumbe mbalimbali za kukabiliana na hali hiyo,”
alisema Mwagowa.
Akizungumzia
namna Faraja kinavyosaidia watoto walio katika mazingira magumu, Afisa
Ustawi wa Jamii kutoka kituo hicho, Fatuma Jumanne, alisema mpaka sasa
idadi ya watoto waliofikiwa na kupatiwa huduma stahiki ndani ya manispaa
ya Singida imefikia 115, wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi,
sekondari na vyuo
Bi.
Jumanne alisema kituo kimekuwa kikiwapa huduma zote muhimu kwa mahitaji
ya shule ikiwemo kuwalipia ada za shule na michango mbalimbali, sanjari
na huduma za mahitaji ya vifaa vya kujifunzia
“Niombe
sana kuwepo na ushirikiano kwa ngazi zote ndani ya jamii katika
kufuatilia mienendo na tabia za watoto, wazazi na jamii ni wajibu wetu
kuwa karibu na hawa watoto tujikite katika malezi ipasavyo…akitoka
shuleni fuatilia amejifunza nini au ana changamoto gani, kuwa karibu na
mtoto, usimwache,” alisema Jumanne.
Tangu
kuanzishwa kwake Faraja Centre zaidi kimejikita katika kutoa ushauri
nasaha na huduma za upimaji wa VVU/UKIMWI, kusaidia watoto walio katika
mazingira magumu kwenye nyanja mbalimbali, kupambana na biashara haramu
ya ulanguzi wa binadamu kwa kutoa elimu na shughuli za uokozi, sambamba
na huduma ya ‘Tiba Shufaa’ kwa wagonjwa wasiojiweza.
No comments :
Post a Comment