Thursday, March 5, 2020

IGP SIRRO AKIPANDISHA HADHI KITUO CHA POLISI MURIET KUWA KITUO CHA WILAYA


Mkuu wa majeshi nchini IGP Sirro akikata utepe ishara ya kuweka jiwe la msingi katika uzinduzi wa nyumba za polisi zinazojengwa na mwekezaji katika hoteli za kitalii za Grand Media katika eneo la Feed force lililopo kata ya Muriet mjini hapa pembeni yake ni Balozi wa heshima serikali ya Dubai UNT ,Fouad Mustafa Martis
Mkuu wa majeshi nchini IGP Sirro akisoma maelezo yaliyoandikwa katika kibao Cha jiwe la msingi la nyumba za polisi katika kata ya Muriet zilizopo mkoani Arusha ,pembeni yake ni Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akishuhudia uzinduzi huo.
Mratibu wa mradi huo wa ujenzi wa nyumba za polisi katika kata ya Muriet,kutoka kampuni ya China ya  CRJE (EA)Ltd ,Tumainiel Seria akizungumza katika uzinduzi huo kuhusiana na mradi huo.
Mkuu wa majeshi  nchini IGP Sirro akiongozana na viongozi mbalimbali wakati wa kukagua jengo hilo katika eneo la Muriet mkoani Arusha
Mkuu wa majeshi nchini ,IGP Simon Sirro akizungumza na wananchi waliohudhuria katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika nyumba za polisi katika kata ya Muriet mkoani Arusha
(Happy Lazaro)
……………………………………………………………………………………………..
Happy Lazaro,Arusha.
Mkuu wa majeshi nchini  IGP Simon Sirro amekipandisha hadhi kituo Cha polisi Cha Muriet na kuwa kituo Cha polisi  cha wilaya baada ya ombi hilo kutolewa na mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo.
Sirro amekipandisha hadhi kituo hicho jana wakati akizungumza katika hafla ya uwekaji wa  jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za polisi sita zinazojengwa kwa ufadhili wa mwekezaji wa hoteli za kitalii za  GrandMelia ambaye amejitolea kujenga nyumba hizo sita za Askari polisi  katika eneo la FFU Kata ya Muriet mkoani Arusha.
Aidha Sirro alimpongeza mwekezaji huyo kwa moyo huo wa kujitolea  na kufikia hatua ya  kujenga kituo hicho ambacho kitasaidia Sana kupunguza matukio ya uhalifu katika kata hiyo kutokana na idadi kubwa ya wananchi waliopo.
“Kuanzia leo nimekipandisha hadhi kituo hiki na kuwa Cha wilaya Kama ambavyo nimeombwa na mkuu wa mkoa wa Arusha kutokana na  kuwa ni ombi la wananchi kwa muda mrefu na nitamleta OCD na OCCID hapa ili waweze kushirikiana kwa pamoja na naombeni Sana wananchi want mfuate sheria zilizopo kwani tumejipanga kutokomeza uhalifu kabisa.”alisema Sirro.
Aidha Sirro alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi kuhakikisha wanawalea watoto wao katika maadili mema ili waweze kuepukana na vijana wanaokuja kuwa wahalifu mtaani  .
Aliwataka wananchi katika kuelekea uchaguzi kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu za nchi huku akiwataka uchaguzi huo kutowafarakanisha  badala yake Kila my atimize wajibu wake na kwa wakati wake pia.
“Ninachotaka kuwaeleza ni  kuwa sisi Kama jeshi la polisi kazi yetu ni kulinda wananchi na Mali zao na hatuko tayari kuona sheria zinavunjwa na ikitokea mwanasiasa akiingia kufanya uhalifu lazima ashughulikiwe Kama mhalifu mwingine”alisema Sirro.
Naye Mkuu wa  mkoa wa Arusha ,Mrisho Gambo alimshukuru IGP Sirro kwa kukubali ombi lake na kukipandisha hadhi kituo hicho cha polisi ambapo itasaidia Sana kupunguza uhalifu katika kata hiyo huku ikilinganishwa ni eneo linalokuwa kwa Kasi kutokana na idadi kubwa ya watu kuendelea kuhamia.
Gambo alisema kuwa,ameshukuru Sana kutimiza ahadi yake ya kujenga nyumba za polisi kwa kushirikiana na wafadhili mbalimbali ,ambapo  alisema kuwa jeshi limekuwa likijipanga kuhakikisha kunakuwepo kwa ulinzi wa  kutosha kwa wananchi na Mali zao,hivyo ili waweze kutimiza wajibu wao vizuri ni lazima waboreshewe mazingira yao .
“Kwanza kabisa nakushukuru Sana IGP kwa kutupatia Kamanda wa mfano ambaye ni  mahiri mchapa kazi anayehakikisha mkoa wetu unakuwa salama muda wote na tangu utuletee huyo Kamanda kwa kweli uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa Sana akishirikiana na Askari wake pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Arusha”alisema Muro.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwashukuru wawekezaji hao wa hoteli ya Grandmelia kwa kusaidia ujenzi wa kituo hicho kwani kwa kufanya hivyo inaonyesha jinsi ambavyo wapo karibu na jeshi Hilo na kwa kufanya hivyo wameweza kujenga taswira nzuri.”alisema Gambo.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwataka wawekezaji wa mkoa wa Arusha kuiga mfano huo kwa kuhakikisha wanaisaidia jamii katika shughuli mbalimbali za maendeleo Kama walivyofanya wawekezaji hao.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha, Jonathan Shanna ameshukuru kwa kuona  Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo ametimiza ahadi yake ya kujenga nyumba sita za polisi  kila mwaka ikiwa ni ahadi yake kwa jeshi la polisi.
Shana alisema kuwa, jeshi la polisi mwaka Jana walipata nyumba za kisasa eneo la polisi mess pamoja na eneo la feed force Njiro nyumba sita ambapo kwa  mwaka huu tena wamepata nyumba sita pamoja na kupewa gari kwa askari wake .
Naye Balozi wa heshima serikali ya Dubai UNT , Fouad  Mustafa Martis alisema kuwa,wamefikia hatua ya kusaidia ujenzi wa kituo hicho Cha polisi kutokana na mahusiano mazuri waliyo nayo na jeshi hilo,huku wakiahidi kuendelea kusaidia zaidi .
Alisema kuwa,wamekuwa wakishirikiana shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kurudisha faida wanayoipata kwa wananchi na kuwa wamekuwa na mahusiano mazuri Sana na jeshi hilo kwa kushirikiana katika maswala mbalimbali.
Naye Mratibu wa mradi huo  Tumainiel Seria kutoka kampuni ya China ya CRJE (EA) Ltd alisema kuwa ,wanashukuru jeshi la polisi kwa kuwapa dhamana ya ujenzi wa kituo hicho na kuwaamini ambapo waliahidi kuutekeleza kwa wakati na kukamilika kwa muda uliopangwa ambao ni mwezi wa nne mwaka huu.
Alisema kuwa,nyumba hizo hadi kukamilika zitagharimu kiasi Cha dola za kimarekani laki mbili ambapo Hadi Sasa hivi limeshakamilika kwa asilimia 40 .

No comments :

Post a Comment