Kamishna Jenerali wa Magereza,
Suleiman Mzee akisema jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya
Ukimwi na Madawa ya Kulevya (hawapo pichani) wakati wa ziara katika
Gereza Kuu la Arusha.
ACP Dkt. Richard Mwankina akisoma
taarifa ya Jeshi la Magereza kwa niaba ya Kamishna Generali wa Magereza
Suleiman Mzee (hayupo pichani) kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga
kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Leonard Subi akisema jambo mbele ya Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya na viongozi
waandamizi wa Jeshi la Magereza nchini (hawapo pichani)
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya wakisalimiana na maafisa
wa Gereza kuu la Arusha walipofanya ziara gerezani hapo kuzungumza na
wafungwa na mahabusu.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya pamoja na wataala kwenye
kikao cha pamoja wakijadiliana masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya
gerezani katika kikao kilichoongzowa na Mwenyekiti Mhe, Oscar Mukasa
…………………………………………………………………………………………….
Na Englibert Kayombo WAMJW -Arusha
Juhudi za Serikali ya Awamu ya
Tano katika kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi zimeliwezesha
Jeshi la Magereza kuboresha huduma za matibabu na upatikanaji wa
dawa za
kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (VVU) hivyo kufikia malengo ya
milenia (90-90-90)
Hayo yamesemwa na Uongozi wa Jeshi
la Magereza wakati wa kikao na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanahusika na masuala ya Ukimwi na
Madawa ya Kulevya.
Akisoma taarifa ya hali ya
maambukizi ya VVU na upatikanaji wa tiba kwa magonjwa nyemelezi kwa
niaba ya Kamishna Jenereali wa Magereza Bw. Suleiman Mzee, ACP. Dkt.
Richard Mwankina amesema “huduma za Afya gerezani zimeboreshwa kwa
kiwango cha juu na imetusaidia kuweza kuboresha matibabu na upatikanaji
wa dawa za kufubaza makali ya VVU kwa wagonjwa”
ACP.Dkt. Mwankina amesema kuwa
kutokana na juhudi za Serikali za kupambana na VVU kumekuwa na ongezeko
la wafungwa na mahabusu kujitokeza kwa hiari kupima afya zao hivyo
kufikia lengo la kwanza (1st 90) ambapo baada ya kuwagundua wagonjwa wa
VVU waliweza kuwaanzishia dozi na kuwa na ufuasi mzuri wa dawa (2nd 90)
Wagonjwa hao wamekuwa na matokeo mazuri ya ufubazi wa VVU (3rd 90) hivyo
kufikia malengo ya milenia (90-90-90)
ACP. Mwankina amesema kuwa
wamefanikiwa kufikia malengo hayo ya milenia kutokana na mikakati
madhubuti ya kuhakikisha wanatoa na kusimamia huduma za afya kwa
wafungwa, mahabusu pamoja na wataalam na familia zao.
“Kabla ya Mwaka 2007 watumishi wa
Jeshi la Magereza na familia zao, wafungwa pamoja na mahabusu walikuwa
wanapata huduma za afya katika vituo vya nje” amesema ACP. Dkt. Mwankina
ACP. Dkt. Mwankina amesema kuwa
kuanzia mwaka 2007 huduma za afya zilianza kutolewa ndani ya Jeshi la
Magereza na walianza kujenga vituo hivyo ambavyo mpaka kufikia mwaka
2020 idadi ya vituo hivyo vimefika 30.
Amefafanua kuwa kupitia vituo
hivyo wameweza kufanya upimaji wa hiari kwa wafungwa na mahabusu katika
nyakati tofauti ambapo walifanikiwa kuwabaini wagonjwa wa VVU na
kuwaanzishia dozi ya kufubaza makali ya VVU.
“Katika kipindi cha Januari hadi
Desemba 2019, jumla ya wafungwa na mahabusu 1372 katika Gereza Kuu la
Arusha walijitokeza kwa hiari kupima afya zao na tuliwabaini wa 34 kuwa
na VVU, kati yao 31 ni wanaume na watatu ni wanawake” amesema ACP. Dkt.
Mwankina
Amesema kuwa wameweza kufikia
mafanikio haya kutokana na elimu ambayo wafungwa na mahabusu wamekuwa
wakiipata ambapo walijitokeza na kupima afya zao pamoja na kuimarisha
ushirikiano mzuri baina yao na vituo vya kutolea huduma za afya nje ya
magereza ili kuweza kupata huduma za rufaa za matibabu pindi ambapo
huduma za vipimo na tiba zaidi zinapokosekana ndani ya gereza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya. Dkt. Leonard Subi amesema kuwa
Serikali imekuwa ikitoa mafunzo ya masuala ya magonjwa ya kuambukiza
ikiwemo Ukimwi na TB katika magereza ambapo kwa mwaka 2019 jumla ya
magereza 17 yalinufaika na mafunzo hayo.
“Mwaka jana tumeweza kutoa elimu
ya magonjwa ya kuambukiza kwa magereza 17 nchini, ambapo tulitoa mafunzo
kwa maafisa magereza 209 na watumishi wengine 1378” amesema Dkt. Subi
na kuendelea kusema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wataalam,
wafungwa na mahabusu kutambua dalili na athari zitokanazo na magonjwa ya
kuambukiza ikiwemo Ukimwi na Kifua Kikuu”
Dkt. Subi amesema kuwa pamoja na
mafunzo hayo waliendeshazoezi la upimaji wa hiari kwa wafungwa na
mahabusu ambapo jumla ya wafungwa 5005 na mahabusu 6795 walipimwa afya
zao.
“Katika upimaji huo tulibaini
uwepo wa waginjwa 42 wenye ugonjwa wa kifua kikuu na tuliweza
kuwaanzishia matibabu mara moja” amesema Dkt. Subi
Kwa upande wake Kamishna Jenerali
wa Magereza nchini Suleiman Mzee amesema kuwa Jeshi la magereza ni moja
ya wahanga wa ugonjwa wa VVU na hawapo nyuma katika kupambana na ugonjwa
huo kwa wafungwa, mahabusu, watumishi na familia zao.
Kamishna Mzee amesema kuwa Jeshi
la magereza linatoa huduma za uchunguzi wa afya, tiba, ushauri nasaha na
upimaji wa virusi vya ukimwi pamoja na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka
kwa mama kwenda kwa mtoto.
“Jeshi la Magereza lina jukumu la
kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanapata huduma bora za afya kama
ilivyo kwenye jamii nyingine” amesema Kamishna Suleiman Mzee.
No comments :
Post a Comment