Friday, March 6, 2020

BASHUNGWA NA DKT NCHIMBI WAJA KIVINGINE KWENYE ZAO LA ALIZETI


Mkuu
wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi akimkaribisha Waziri wa  Viwanda na Biashara, Innocent Bachungwa
(hayupo pichani) alipotembelea Ofisini kwake leo kwa ajili ya  ziara ya kikazi ya siku moja kukagua  viwanda vya kukamua mafuta ya Alizeti  Mkoani Singida (Picha na John Mapepele)


Mmiliki wa
Kiwanda cha Kukamua Mafuta  cha
Singida Fresh Oil Mill, Abdallah Omary-Shuru (mwenye kanzu)  akimwonyesha Waziri Bachungwa  (aliyeshika gerani) jinsi mashine
zinavyokamua mafuta katikati ni Mkuu wa
wa Wilaya ya Singida, Injinia  Paskasi Muragili, aliyeshika  daftari ni Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa
wa Singida  Stanslaus Choaji
 
.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Innocent Bachungwa (aliyenyanyua mkono) akiangalia  mashine za kukamua mafuta  kwenye kiwanda cha Mt. Meru mjini Singida;
kiwanda kinachosadikiwa kuwa kikubwa kuliko vyote  Afrika Mashariki na Kati, mbele yake ni Mkuu
wa Wilaya ya Singida,
Injinia
Paskasi Muragili nyuma yake ni
Sailesh Patel, Makamo wa Rais wa Kiwanda cha MT Meru-Tanzania
Na John Mapepele, Singida 
Waziri wa Viwanda na
Biashara, Innocent Bichungwa ameitaka Wizara yake kwa kushirikiana na Mkoa wa
Singida ndani ya mwezi moja kufanya
mkutano wa kitaifa utakaowashirikisha wadau wote wa zao la Alizeti.
Mkutano huo utakuwa ni wa   kujadili
mnyororo wa thamani  wa zao hili
kuanzia kwa mkulima  hadi kwa wenye
viwanda  ili kuleta  mapinduzi ya kiuchumi na kufuta gharama kubwa
ambazo serikali inatumia kuagiza mafuta ya kula toka nje ya nchi. 
Bachungwa  ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya
siku mmoja leo kwenye  Mkoa wa Singida
kutembelea  viwanda vya kukamua Alizeti  ambapo alikagua shughuli zinazofanywa na
kiwanda  kikubwa cha kukamua mafuta
Afrika mashariki na Kati cha Mt. Meru na
Kiwanda cha  Singida Fresh Mill vilivyopo
ndani ya Manispaa ya Mji wa Singida.
Alisema lazima kuwepo na mkutano huo haraka wa wadau
wote  wa zao hilo ili kunusuru fedha
nyingi zinatumika  na nchi kununua  mafuta  ya kula kutoka nje ya nchi
Alisema katika kundi la
bidhaa la vyakula, mafuta ya kula yanashika nafasi ya pili kuwa kutumia gharama
ya asilimia 22.6 ikiongozwa  na zao la Ngano
linalotumia asilimia 57.3 huku Sukari
ikitumia asilimia 16.2  ikifuatiwa
na Mahindi ambayo yanatumia gharama ya asilimia
2.6 kulipiwa toka nje ya nchi ambapo aliongeza  kuwa Tanzania kama nchi inatumia jumla ya
kiasi cha shilingi trioni 1.3 kwa mwaka
kuagiza  bidhaa zote za vyakula
kutoka nje ya nchi.
Bachungwa alisema
Tanzania  imejaliwa kuwa na maeneo makubwa
ya ardhi yenye rutuba ambayo yanaweza kupanda
mbegu bora za Alizeti ambazo zinaweza kutosheleza viwanda vya ndani na
kuuzwa nje ya nchi, kinachotakiwa ni wadau wote kukaa kama taifa na  kujadii namna bora ya kuongeza thamani kwenye
mnyororo wa mzima wa thamani wa zao la Alizeti.
Aliwataja baadhi ya wadau
muhimu katika kikao hicho kuwa mikoa inayolima zao la Alizeti, wizara inayohusika
na kilimo, Mifugo na Uvuvi, Fedha, tasisi za utafiti zinazojiusisha na Alizeti,
wajasiliamali  na wawekezaji wa viwanda
vikubwa vya kukamua mafuta ya Alizeti hapa nchini.
Alisema alichogundua katika
ziara hiyo ni  kuwa hakuna  mfumo mzuri wa kufungamanisha  kilimo cha alizeti na viwanda  hali inayowafanya wadau washindwe kupata  faida na badala yake kuhangaika kutafuta
masoko ya bidhaa hizo nje ya nchi  na
kuwakosesha watanzania  ajira na mapato
kwa taifa.
“Nimeshangaa viwanda
vinahangaika kuuza mashudu nchi jirani na kulalamikia kodi na ushuru unaotozwa
na Serikali wakati tunaviwanda vyetu vya kutengeneza vyakula vya kuku
vinahangaika usiku na mchana kutafuta
mashudu wakati Singida  yamejaa”
alihoji Bachungwa
Aliutaka Mkoa wa
Singida  kutumia  fursa ya kuwa jirani na Makao Makuu ya Nchi,
Dodoma  kupanga mipango mizuri kwa
kutenga  maeneo maalum ya uwekezaji kama
ambavyo Mkoa wa Pwani ulivyonufaika kwa kuwa
karibu na Jiji la Dar es Salaam
kwa kutenga maeneo ambayo sasa
maeneo hayo  yameendelea kujengwa
viwanda vya kisasa hivyo  kuendana  na
kauli ya  Serikali ya awamu ya
Tano inayosisitiza  ujenzi wa viwanda
Aidha aliwataka watendaji
Serikalini kote nchini kubadilika  na
kuondokana na dhana kwamba mapinduzi ya viwanda yataletwa na Wizara  ya Viwanda na Biashara  na badala yake  mikoa
iweke  mikakati mahususi ya
kuwavutia wa wekezaji kuja kuwekeza na
baada ya kuwekeza waendelee kuwalea
ili waweze  kuendelea  kuweka mitaji
zaidi ktika mikoa husika.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Singida  Dkt. Rehema Nchimbi alimshukuru
Waziri Bachungwa  kwa  kufanya ziara hiyo ambapo alisema  tayari mkoa wake umeshafanya vikao  vya mara kwa mara na wadau mbalimbali wa zao la
alizeti ambapo amesema hata wiki moja iliyopita Mkoa wa kushirikiana na Shirika
na Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Viwanda Vidogo Nchini (SIDO) walitoa
mafunzo maalum  kwa wajasiliamali wa zao
hilo ambapo amesema mkutano huu utakuwa na manufaa makubwa kwa kuwa utakuwa
katika ngazi ya kitaifa na itashirikisha wadau wengi zaidi.
“Mkoa tunafarijika
sana  kwa wazo lako ulilotoa la kuwa na
mkutano wa kitaifa wa wadau wote wa zao la Alizeti  kwa kuwa ni ndoto yetu kuboresha thamani ya zao
hili ili kuleta mapinduzi makubwa kwa wadau wote na taifa kwa ujumla, nakuahidi
sisi kama Mkoa tutafanya  haraka
iwezekanavyo kuhakikisha mkutano unafanyika ndani ya mwezi huu” alisisitiza
Dkt. Nchimbi
Alisema katika kuratibu
mkutano huo mkoa utawashirikisha wadau mbalimbali ambao wataandaa maonyesho
maalum  ya mnyororo wa zao la Alizeti ili
washiriki waweze fursa  kuona bidhaa
mbalimbali zitokanazo na zao hilo.
Aliongeza kuwa Mkoa umekuwa
ukifanya kampeni mbalimbali ikiwa ni pamoja na kampeni ya mbegu hasara na
mbegu  bora iliyolenga kuwafanya wakulima
kuachana na  mbegu za asilia ambazo  mavuno yake yalikuwa yanazidiwa  mara saba zaidi  na mbegu bora ya kisasa.
Alizitaja baadhi ya faida
ya mbegu bora kuwa ni kuokoa  akiba ya
ardhi, kuokoa muda, bei  ya kuuza kuwa
juu  ambapo pia aliishukuru benki ya
kilimo nchini TADB kwa kutoa mikopo ya zaidi ya
bilioni 4 kwa wadau mbalimbali wa zao la alizeti kwenye mkoa wa Singida.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida  Injinia
Paskasi Muragili  ameishukuru
Serikali  kwa kupanga kufanya  mkutano huo kwenye Wilaya  yake ambapo alisema Wilaya yake ndiyo
mzalishaji  mkuu wa  mbegu bora za Alizeti hivyo mkutano huo
utasaidia  kuwapa msukumo  mpya wadau wote kuboresha thamani ya mnyororo
mzima wa thamani wa zao hilo.

No comments :

Post a Comment