Afisa Forodha TRA Mtwara,
Salvatory Chami akitoa elimu kwa wananchi wa kijiji cha Kitaya wilaya ya
Mtwara kuhusu faida za kutumia vituo vya forodha halali kupitisha
bidhaa kutoka nje ya nchi
Wananchi wa kijiji cha Kivava wakimsikiliza kwa makini Jackline Lutatare, Afisa Usimamizi wa Kodi
Afisa Forodha TRA Mtwara,
Salvatory Chami akitoa elimu kwa wananchi wa kijiji cha Msimbati wilaya
ya Mtwara kuhusu faida za kutumia vituo vya forodha halali kupitisha
bidhaa kutoka nje ya nchi
Afisa Forodha TRA Mtwara,
Salvatory Chami akitoa elimu kwa wananchi wa kijiji cha Kivava wilaya ya
Mtwara kuhusu faida za kutumia vituo vya forodha halali kupitisha
bidhaa kutoka nje ya nchi
Bi Valentina Bartazar, Afisa Mkuu
Usimamizi wa Kodi akitoa elimu kuhusu athari ya biashara ya magendo kwa
wananchi wa kijiji cha Kitaya
………………………………………………………………………………………………………..
Na Oliver Njunwa-Mtwara
Wananchi wanaoishi katika vijiji
vilivyoko pembezoni mwa Bahari ya Hindi Mkoani Mtwara, wamehimizwa kuwa
walinzi wa mipaka ya nchi kwa kutoa taarifa kuhusu biashara za
magendo
ili kuepukana na athari zinazotokana na biashara ya magendo na matumizi
ya bidhaa za magendo.
Wito huo umetolewa na Afisa Mkuu
Usimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Valentina
Bartazar wakati akitoa elimu ya uzuiaji wa bidhaa za magendo katika
nyakati tofauti kwa wananchi wa vjijiji vya Msangamkuu, Msimbati,
Kivava, Kitaya na Dindwa wilaya ya Mtwara, Mihambwe na Chikongo Wilaya
ya Tandahimba na Chikunya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara.
“Tunawasihi wananchi kutoa taarifa
kuhusu shughuli za magendo zinazofanyika katika maeneo yenu ikiwemo
uingizaji wa bidhaa za magendo ili kuwaepusha na madhara ya shughuli za
magendo na matumizi ya bidhaa za magendo”, alisema Bi Bartazar na
kuongeza kwamba vitendo vya magendo vinaathaari za kiafya, kijamii,
kiuchumi, pamoja na kiusalama kwa wananchi wa maeneo husika na taifa kwa
ujumla.
Bi Bartazar alisema kwamba bidhaa
za magendo ni hatari kwa afya za wananchi kutokana na ukweli kwamba
bidhaa hizo zinapoingizwa nchini hazifuati utaratibu wa kuthibitishwa
ubora na taasisi zinazohusika kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Pia bidhaa za magendo
Pamoja na kuwa na athari kiafya
bidhaa za magendo pia zinadidimiza uchumi wa nchi kwa kuwa hazilipiwi
kodi na hivyo kukwamisha juhudi za serikali za kuongeza mapato ya ndani
ili nchi iweze kujitegemea na kuimarika kiuchumi.
Aidha aliwahimiza wafanyabiashara
kutumia vituo vya forodha vilivyohalalishwa kupitisha mizigo ili kulipa
kodi halali ya serikali pia kuepuka kupata hasara baada ya bidhaa hizo
kukamatwa na kutaifishwa.
Bi Bartazar amesema kwamba TRA
imeamua kuendesha kampeni ya uelimishaji kuhusu uzuiaji wa biashara ya
magendo ili wananchi wafahamu athari zake pamoja na kufahamu faida za
kutumia vituo vya forodha vilivyoidhinishwa na serikali.
Naye Afisa Forodha wa TRA Mtwara
Salvatory Chami aliwaambia wananchi hao kwamba baadhi ya bidhaa
wanazoingiza nchini kwa njia ya magendo kutoka nchi jirani ya Msumbiji
hazistahili kulipiwa kodi kutokana nchi hizo kuwa na makubaliano ya
kibiashara.
Akawaeleza kwamba wananchi wengi
wanaingiza bidhaa kwa magendo wakidhani wanakwepa kodi kumbe bidhaa
wanazoingiza hazistahili kulipiwa kodi na wakikamatwa wanatozwa faini na
hivyo kuathiri kipato chao.
“Ofisi za TRA ziko wazi kwa ajili
ya kuwashauri wananchi ambao wanataka kufanya biashara ya kuingiza
bidhaa ndani ya nchi. Hivyo wananchi wanashauriwa kutembelea ofisi hizo
kupata ushauri kabla ya kufanya bashara ili waweze kufahamu bidhaa
zinazostahili kulipiwa ushuru na ambazo hazistahili kulipiwa ushuru,
bidhaa zinazostahili kuingizwa nchini pamoja na viwango vya kodi
vinavyostahili kutozwa kwa bidhaa zinazoingizwa nchini”, alisema Chami.
Akizungumzia adhabu za kufanya
magendo kwa mujibu wa sheria, Chami aliwwambia wananchi hao kwamba
wanaweza kutozwa faini ambayo ni asilimia 50 ya thamani ya mzigo
ulioingizwa kwa magendo, kutaifishwa kwa vyombo ambavyo vimetumika
kubeba bidhaa za magendo pamoja na kufunguliwa mashtaka na kufungwa
jela.
Ili kufanya biashara kwa uhuru
akawahimiza wananchi kutumia vituo vya forodha na kupata nyaraka stahiki
zinazowaruhusu kuingiza bidhaa na kuziuza nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
wakati wa kampeni hiyo, wananchi wa vijiji hivyo wameiomba serikali
kuhalalisha vituo vya forodha vilivyo jirani na vijiji hivyo ili waweze
kufanya biashara halali na kulipa kodi stahiki.
“Sisi tuko tayari kulipa kodi kwa
mujibu wa sheria endapo vituo vilivyo jirani yetu vitawekwa ofisi ya TRA
ili kuturahisishia kuingiza bidhaa kutoka Msumbiji ambazo zinapatikana
kwa urahisi”, alisema Ahmad Juma mkazi wa kijiji cha Chikunya katika
Wilaya ya Newala.
Katika hatua nyingine baadhi ya
viongozi wa vijiiji hivyo wameipongea TRA kwa kuamua kuwaelimisha
wananchi juu ya athari za shughuli za magendo na faida ya kutumia vituo
halali kwa kuingiza bidhaa nchini.
Hamdani Mohammed ni afisa Mtendaji
wa Kijiji cha Msangamkuu kilichopo Wilaya ya Mtwara ambaye amesema
kwamba elimu hii inahitajika mara kwa mara ili kuwakumbusha wananchi
umuhimu wa kulinda mipaka yao kwa kuzuia vitendo vya biashara ya
magendo.
Pamoja na TRA kutoa elimu kuhusu
uzuiaji wa biashara za magendo kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa
Bahari ya Hindi na Mto Ruvuma pia wananchi walipata fursa ya kuuliza
maswali pamoja na kutoa maoni kuhusu shughuli na huduma zinazotolewa na
TRA.
Kampeni ya elimu kuhusu uzuiaji wa
magendo nchini inaendelea katika mikoa ya Dar es salaam, Mtwara na
Tanga lengo likiwa ni kuwaelimisha wananchi wanaoishi kando kando ya
Bahari ya Hindi na sehemu zinatumika kupitisha bidhaa za magendo kuhusu
madhara ya matumizi ya bidhaa za magendo pamoja na kuwahimiza wananchi
kutumia vituo halali kupitisha bidhaa kutoka nje ya nchi.
No comments :
Post a Comment