………………………………………………………………………….
Tanzania imeieleza Tume ya
haki za binadamu na watu wa Afrika ya Umoja wa Afrika kuwa kuna tofauti
kati ya makosa ya kitaalamu na makosa ya jinai na kwamba Sheria
inapochukua
mkondo wake isitafsirike kuwa ni kukiuka haki za binadamu
kwa kuwa Nchini Tanzania hakuna raia wake yeyote aliye juu ya sheria
pale anapotenda kosa la jinai.
Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John
Kabudi ameyasema hayo katika majadiliano ya taarifa ya Tume ya Haki za
Binadamu katika mkutano wa 33 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika
unaofanyika Addis Ababa Nchini Ethiopia na kuongeza kuwa Tanzania
inaheshimu haki za binadamu,uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya
habari kama ilivyo katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Prof. Kabudi
ameongeza kuwa Nchini Tanzania hakuna raia wake aliye juu ya sheria na
kwamba pale mwanataaluma anapofanya makosa ya kijinai huchukuliwa hatua
za kisheria kama ilivyo kwa wananchi wengine kwa kufikishwa katika
vyombo rasmi vya kutoa haki kama mahakama ambayo iko huru kufanya
maamuzi yake isichukuliwe kama ukiukwaji wa haki za binadamu au kuminya
uhuru wa kujieleza.
Amesema kuwa
kuna baadhi ya wananchi wa Tanzania ambao wamekuwa wakitumia taaluma zao
vibaya na hivyo kuwafanya kutenda makosa ya jinai kwa kutumia taaluma
zao na hivyo kufikishwa mbele ya sheria na kuongeza kuwa mashauri yao
yako mahakamani na vyombo vingine vya sheria na ana imani mahakama na
vyombo hivyo vitatoa haki dhidi ya mashtaka yanayowakabili baada ya
kutoa utetezi wao mbele ya vyombo hivyo.
Hivi karibuni
kumekuwepo na mjadala kutoka kwa baadhi ya wanaharakati,wanasiasa na
Jumuiya za Kimataifa zikiishutuma Tanzania kukiuka haki za binadamu
jambo ambalo serikali imeiambia Umoja wa Afrika na Jumuiya za Kimataifa
kuwa si kweli na kwamba Tanzania inaheshimu haki za binadamu na uhuru wa
kujieleza.
Mkutano wa
kawaida wa 33 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unafanyika
Mjini Addis Ababa Nchini Ethiopia ukitanguliwa na mikutano mbalimbali
ya Baraza la Mawaziri na baadae Wakuu wa Nchi na Serikali na unatarajiwa
kumalizika Februari 10,2020.
No comments :
Post a Comment