Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali bungeni jijini Dodoma, Februari 6, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisikiliza swali kutoka kwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni Freeman Mbowe,
bungeni jijini Dodoma, Februari 6, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
…………………………………………………………………………….
* Asema hakuna mbunge wala diwani aliyezuiwa kufanya mikutano
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano haiongozwi kibabe na
kwamba hakuna mbunge yeyote wala diwani aliyezuiwa na Serikali kufanya
shughuli zake kisiasa katika eneo lake.
“Nakanusha kwamba
Serikali inaongozwa kibabe. Serikali haiongozwi kibabe na Mheshimiwa
Mbowe sisi sote ni viongozi na kawaida huwa tunabadilishana mawazo kwa
lengo la kulifanya Taifa liwe salama na Watanzania tunaowaongoza wapate
maendeleo.”
Waziri Mkuu
ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Februari 6, 2020) wakati akijibu swali
la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe
katika kipindi cha maswali ya papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
Kiongozi huyo
alitaka kujua ni lini Serikali itaruhusu vyama vifanye uenezi kuelekea
uchaguzi mkuu, pia Serikali ina mpango gani kuwezesha kupatikana kwa
tume huru ya uchaguzi ili uwe huru na wa haki. Alisema ni wakati muafaka
kwa wadau kukutana kuliko Serikali kutumia ubabe.
Waziri Mkuu
amesema vyama vya siasa havijazuiwa kufanya shughuli zake, ila umewekwa
utaratibu muhimu unaoviwezesha vifanye shughuli zake vizuri na kama kuna
shida yoyote, wahusika wanatakiwa watoe taarifa.
“Mfano ni mbunge
wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ambaye alisema anazuiwa na OCD asifanye
shughuli za siasa kwenye eneo lake, nilimuita hapa Bungeni, alikuja
tukazunguza na suala hilo likaisha. Serikali inashirikiana na vyama
vyote, kama kuna shida tuwasiliane.”
Kuhusu suala la
vyama kuanza kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Waziri Mkuu
amesema kwamba ratiba zitatolewa na zitaeleza ni lini kampeni zitaanza
ili waweze kueleza sera zao na wananchi waendelee kufanya uamuzi wa sera
ipi inafaa kuleta maendeleo nchini.
Kadhalika, kuhusu
kuwa na tume huru ya uchaguzi, Waziri Mkuu amesema Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ni chombo huru na kimeundwa kwa mujibu wa katiba ya mwaka 1977,
ibara ya 74 kipengele cha (7), (11) na (12) ambayo imeeleza kwamba
chombo hicho ni huru na hakipaswi kuingiliwa na mamlaka yoyote.
Waziri Mkuu
amesema suala la kuona Tume ya Taifa ya Uchaguzi si huru ni mtizamo wa
mtu binafsi lakini ni chombo huru kama Katiba inavyoonesha. “Hatujawahi
kuona chombo hiki kikiingiliwa hata na Rais, kama kuna tatizo semeni
lifanyiwe kazi.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa atoe taarifa ya hatua iliyofikiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuhusu mapitio ya gharama za huduma ya maji nchini.
Waziri Mkuu
ametoa agizo hilo wakati akijibu swali la Mbunge wa Babati Mjini,
Mheshimiwa Pauline Gekul aliyetaka kujua ni lini Serikali itakamilisha
mchakato wa mapitio ya gharama za huduma ya maji.
“Serikali
hailengi kufanya biashara wala kupata faida; muhimu ni wananchi wapate
huduma. Tumeunda kamati na mamlaka za utoaji huduma za maji kwenye
maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kusimamia ujenzi na uendeshaji wa
miradi ya maji.”
No comments :
Post a Comment