Thursday, February 6, 2020

TRA YASHAURIWA KUENDELEA KUWEKEZA KWENYE TEKNOLOJIA YA KISASA



Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede akimpa zawadi ya jarida linaloonesha vivutio mbalimbali vilivyopo hapa nchini Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya wakati alipotembelea TRA jana jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede wakipeana mikono mara baada ya Kamishna Mkuu kumkabidhi zawadi Katibu Mkuu huyo ambaye alitembelea TRA jana jijini Dar es Salaam ili kuona shughuli mbalimbali hususani za kiforodha zinazofanywa na TRA.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede (katikati) akizungumza na Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (kushoto) wakati Katibu Mkuu huyo alipotembelea TRA jana jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya akizungumza na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede wakati Katibu Mkuu huyo alipotembelea TRA jana jijini Dar es Salaam.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede akiwa na mgeni wake Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO) Dkt. Kunio Mikuriya (wa pili kulia) wakielekea eneo la forodha la Bandari ya Dar es Salaam wakati Katibu Mkuu huyo alipotembelea TRA jana jijini Dar es Salaam.
Kaimu Meneja Msaidizi wa TRA Joseph Raymond akimuonesha Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO) Dkt. Kunio Mikuriya mfumo mpya wa kukagua mizigo inayoingia na kutoka nchini wakati Katibu Mkuu huyo alipotembelea TRA jana jijini Dar es Salaam. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO).
****************************** 
Na Veronica Kazimoto
Dar es Salaam

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeshauriwa kuendelea kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa kwa kuwa Tanzania ni nchi mojawapo za ukanda wa Afrika Mashariki yenye
lango kuu la kuingilia ukanda huo suala linalosaidia kukuza uchumi kupitia ushuru wa forodha unaotozwa katika eneo hilo.
Ushauri huo umetolewa jana na Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya alipotembelea TRA akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku tatu hapa nchini
“Ili kusimamia ushuru wa forodha ipasavyo, suala la teknolojia halikwepeki, hivyo ni muhimu TRA ijikite zaidi katika kuendelea kuwekeza kwenye mifumo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na watumishi wenye uwezo wa kuendesha mifumo hiyo,” alieleza.
Dkt. Kunio Mikuriya alisema kwamba, akiwa kwenye mazungumzo na mwenyeji wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede, wamezungumzia juu ya umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kudhibiti na kusimamia ushuru wa forodha kwenye bandari ya Dar es Salaam na maeneo mbalimbali hapa nchini.
Naye, Kamishna Mkuu wa TRA alisema kuwa, ziara ya Katibu Mkuu huyo imelenga kuimarisha mahusiano baina ya nchi wanachama wa WCO ambapo ametokea nchini Kenya kwa ajili ya kazi hiyo pia.
“Tanzania ni mwanachama wa WCO na kuna mashirikianio ambayo tunafanya kwa pamoja kuhakikisha eneo la forodha linatekeleza majukumu yake ili kuhakikisha kuna usalama wa bidhaa kwenye eneo la biashara,” alisema Dkt. Mhede.
Alisema kuwa, Tanzania ni kitovu cha biashara kwa kuwa inahudumia nchi zote ambazo hazina bandari kwa mfano Zambia, Malawi, Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao wote wanatumia Bandari ya Dar es Salaam, hivyo ni muhimu kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika kusimamia masuala yote ya kiforodha.
Katibu Mkuu wa WCO Dkt. Kunio Mikuriya baada ya kutembelea Mamlaka ya Mapato Tanzania alielekea jijini Dodoma kwa lengo la kukutana na baadhi ya watunga sera kwa ajili ya kuimarisha mahusiano yaliyopo.

No comments :

Post a Comment