Serikali ya
Tanzania na China zimetoa tamko la pamoja kuhusu hali za watanzania
walioko nchini China na hatua zinazochukuliwa na nchi hiyo kukabiliana
na virusi vya Corona.
Tamko hilo la
pamoja limetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) pamoja na Balozi wa China
hapa Nchini Mhe Wu Ke wakiwa wameambatana na Waziri wa Afya,Maendeleo ya
Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu Jijini Dar Es Salaam.
Akitoa tamko hilo
Waziri Kabudi amesema Ubalozi wa China umeomba fursa ya kukutana na
Serikali ya Tanzania kwa nia ya kueleza kwa pamoja hali ilivyo nchini
China,hatua zinazochukuliwa na Serikali ya China kukabiliana na maradhi
hayo ili kuzuia kusambaa katika maeneo mengine duniani sanjari na hali
ilivyo kwa Watanzania wanaoishi Nchini humo.
Kwa upande wake
Balozi wa China hapa Nchini Mhe Wu Ke amewaondoa wasiwasi Watanzania
wote wakiwemo Wazazi na Ndugu wa wanafunzi zaidi ya 4000 hususani
wanafunzi 400 walioko Hubei katika Mji wa Wuhan ambapo panatajwa kama
kitovu cha Virusi vya Corona kwa kusema wako salama na hakuna hata mmoja
aliyeathiriwa.
Ameongeza kuwa
Serikali ya China kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani linachukua
hatua zote kuhakikisha kuwa virusi hivyo havisambai katika maeneo
mengine hasa baada ya shirika hilo kuutangaza ugonjwa huo kama
janga,ikiwemo jitihada za China kujenga Hospitali maalum kwa ajili ya
kuwatibu wale wote watakaoathirika.
Waziri wa
Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema
mpaka sasa hakuna mtu yeyote awe rai wa Tanzania ama wakigeni
aliyethibitika kuwa na virusi hivyo na Serikali inaendelea kuchukua
hatua stahiki na za dharura ikiwemo kuwapima watu wote wanaowasili
Nchini kupitia viwanja vya ndege na aina nyingine za usafiri.
Ameongeza kuwa
tayari serikali kwa kushirikiana na wadau wengine imeimarisha uwezo wa
kuwapima ndani ya Nchi mtu yeyote atakayeshukiwa wa virusi hivyo badala
ya kupeleka sampuli hizo sehemu nyingine ikiwa ni pamoja na nje ya nchi.
Amesisitiza kuwa
Mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote ama mtu yeyote aliyeshukiwa ama
kuthibitishwa kuwa na Virusi vya Corona na tayari Wizara imetenga maeneo
manne kwa kuangalia maeneo yaliyoko katika hatari zaidi ya kupata
maambukizi ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam,Mwanza na Kilimanjaro pia
mazungumzo yanaendelea ili Zanzibar nayo iweze kutenga maeneo maalum kwa
ajili ya wagonjwa ama washukiwa wa homa ya Corona.
KATIKA HATUA
NYINGINE, Tanzania imesema hakuna katazo kwa Mtanzania yeyote aliyeko
nje ya Nchi, China ikiwemo anayezuiwa kurudi Tanzania pindi atakapo.
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji
Mnyepe amewaondoa wasiwasi Watanzania hasa wale wanaotaka kusafiri
kwenda ama kurudi kutoka China,na kwamba wale wanaotaka kusafiri kwenda
China tayari waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa ameshatoa
maelekezo lakini kwa wale wanaotaka kurudi kutoka China Ubalozi wa
Tanzania Nchini China unashirikiana nao kuwarejesha Tanzania kwa wale
wanaotaka na kwamba hakuna katazo la kurejea Tanzania.
No comments :
Post a Comment