Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akipeana mkono na Katibu
Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya, baada ya
Mkutano kati yao uliofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akielezea umuhimu wa
kuboreshwa kwa Idara ya Forodha kwa lengo la kuongeza urahisi wa
ufanyaji wa biashara, wakati wa Mkutano na Katibu Mkuu wa Shirika la
Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (hayupo pichani), kulia ni
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede,
katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa
Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (kulia), akieleza
nia ya Shirika lake kusaidia zana za Kisasa katika Idara ya Forodha
nchini, wakati wa Mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), jijini Dodoma, kushoto
ni Meneja Uwezeshaji wa Biashara na Ujenzi wa Miundombinu Mipakani
kutoka WCO, Bw. Kosaka Yoshihiro.
Waziri wa Viwanda
na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) (kushoto), akimuomba Katibu
Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (katikati)
kusaidia katika kuondoa vikwazo vya wafanyabiashara wa Tanzania kuuza
bidhaa zao katika masoko ya Kimataifa, kulia ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede, katika Ofisi za Wizara hiyo
eneo la Mtumba, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati) na Katibu Mkuu
wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (wa pili
kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede (wa pili kulia) na viongozi
wengine, baada ya Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha
na Mipango jijini Dodoma.
Waziri wa Viwanda
na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) (wa pili kushoto) na Katibu
Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (kushoto),
wakiwa katika picha ya pamoja na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede (wa pili kulia) na viongozi wengine,
baada ya mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Viwanda na
Biashara, Mtumba jijini Dodoma.
(Picha na Veronika Kazimoto na Peter Haule)
*******************************
Na. Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali
imekubaliana na Shirika la Forodha Duniani (WCO) kuisaidia nchi zana
zenye
teknolojia za kisasa zinazoweza kung’amua watu wanaofanya biashara
za magendo na kuifanya Forodha kuongeza ufanisi wa ufanyaji biashara na
ukusanyaji wa mapato.
Hayo yamesemwa na
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipokutana nan a
kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO),
Dkt. Kunio Mikuriya, jijini Dodoma.
Dkt. Mpango
alisema kuwa Shirika la WCO limekubali kutoa Boti, mashine za kupiga
picha ndani ya Kontena na vifaa vingine vyenye teknolojia za kisasa
vinavyoweza kung’amua watu wanaofanya biashara za magendo, hivyo
kuifanya Serikali kuwa na uwezo zaidi wa kudhibiti shughuli hizo haramu.
“Ujio wa Katibu
Mkuu wa WCO, katika nchi za Afrika hususani Tanzania na Kenya umelenga
kuziwezesha nchi hizo kuzitumia fursa zilizopo katika Shirika hilo na
kushirikiana na Idara ya Forodha hapa nchini kurahisisha biashara na
ukusanyaji wa mapato jambo ambalo pia ni agenda ya Serikali ya
Tanzania”, alieleza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango
alisema kuwa, Forodha kwa maana ya Bandari na Vituo vya Forodha
vilivyopo katika mipaka ni eneo muhimu katika kukuza biashara katika
nchi na Ukanda wa Kusini mwa Afrika, ikizingatiwa kuwa Tanzania ni
mlango wa kupitisha mizigo kwenda nchi za Zambia, Zimbabwe, Rwanda,
Burundi, Malawi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nyingine,
hivyo kuwepo kwa Teknolojia hiyo kutakuwa nguzo muhimu ya kuifanya
Forodha kuwa ya Kisasa na inayorahisisha biashara.
Alisema kuwa
wamekubaliana kutoa fursa kwa vijana wa Forodha kupata uzoefu wa Forodha
nyingine zinavyoendeshwa kwa ufanisi na pia kutoa mafunzo kwa wakufunzi
ambao si tu watatoa mafunzo nchini lakini pia nje ya nchi.
Wakati huo huo,
Dkt. Mpango amewaonya wafanyabiashara za magendo nchini kuachana na
biashara hiyo kwa kuwa watapoteza mitaji baada ya Serikali kujipanga kwa
teknolojia mpya ya kuwadhibiti kwa kuwa biashara hizo ni hatari kwa
uchumi wa Taifa na pia Afya za wananchi.
“Wito wangu ni
kwamba watanzania wote na wengine walio nje ya nchi wanaoshiriki katika
biashara za magendo waache vitendo hivyo na wafuate taratibu za Forodha
kinyume na hapo watapoteza mitaji yao kwa kuwa tutawakamata’’, alieleza
Dkt. Mpango
Waziri Mpango
amemuagiza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin
Mhede, kuhakikisha Ushirikiano na WCO unaimarika kwa kuwa Shirika hilo
lina manufaa kwa Maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake
Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya,
alisema kuwa katika kuifanya Forodha iwe na ufanisi lazima kuwe na
dhamira njema ya kisiasa, Ushirikiano na wafanyabiashara,wakala na
Forodha nyingine nje ya nchi na pia kuwekeza kwenye rasilimali watu,
jambo ambalo amehakikishiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango
kwamba lipo.
Dkt. Mikuriya
ameahidi kuwa Shirika lake litafanya kazi kwa karibu na Tanzania katika
mambo yote ambayo wamekubaliana ili kuleta tija katika Sekta hiyo ya
Forodha ndani na nje ya Tanzania.
Naye Waziri wa
Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa, ameliomba Shirika la WCO
kuondoa changamoto zinazoweza kuwakwamisha wafanyabiashara wa Tanzania
kuuza bidhaa katika masoko ya Kimataifa na pia waweze kuzitumia fursa za
kibiashara katika masoko hayo.
Kwa upande wake,
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede,
alisema kuwa wamekubaliana na Shirika la WCO, kujenga Maabara ambayo
itasaidia kutambua na kupima bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi ili
kujiridhisha kama zimezingatia utaratibu, lengo likiwa ni kurahisisha
uthaminishaji wa mizigo na uondoshaji wa mizigo bandarini kwa wakati.
“Maabara hiyo
itakayojengwa katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Jijini Dar es Salaam,
itakua miongoni mwa maabara chache Afrika ambayo itakuwa ya mfano katika
kusimamia eneo hilo la Forodha”, alieleza Dkt. Mhede.
Alisema kuwa
wamekubaliana pia kuweka miundombinu itakayochunguza mizigo inayopita
katika Ukanda wa Kusini (Mtwara Corridor), ikizingatiwa kuwa barabara ya
Ukanda huo imesajiliwa kwa lengo la kuhakikisha Wajasiliamali na wenye
viwanda wanaitumia kwa tija.
No comments :
Post a Comment