**********************
SERIKALI imetoa
jumla ya shilingi bilioni 128.1 kwa ajili ya kugharamia elimumsingi bila
ada katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2019.
Hayo
yameelezwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo (Ijumaa, Februari 7,
2020) wakati
akitoa hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 18 wa Bunge jijini
Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Machi 31, mwaka huu.
“Serikali
imeboresha elimu ya msingi kwa kuendelea kutekeleza programu ya
elimumsingi bila ada ambapo Serikali inagharamia chakula kwa wanafunzi
189,226 wa kutwa na bweni, posho ya madaraka kwa walimu wakuu 23,843,
fidia ya ada kwa wanafunzi 1,874,331 na ruzuku ya uendeshaji wa shule,”
amesema.
Akielezea
kuhusu matokeo ya mitihani ya kitaifa, Waziri Mkuu amesema matokeo
chanya ya maboresho hayo ni kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu katika
upimaji wa kitaifa kwa darasa la nne, kidato cha pili na mitihani ya
kitaifa kidato cha nne kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2019.
“Shule za Kata nazo zimeendelea kufanya vizuri na kuongeza matumaini kwa
Watanzania walio wengi,” ameongeza.
“Matokeo ya
upimaji wa kitaifa wa darasa la nne kwa mwaka 2019, yamebainisha kuwa
jumla ya wanafunzi 1,531,120 walifaulu ikilinganishwa na wanafunzi
1,213,132 waliofaulu mwaka 2018. Ufaulu huo ni sawa na ongezeko la
asilimia 26.21. Kwa upande wa kidato cha pili, wanafunzi 514,251
walifaulu upimaji wa kitaifa kwa mwaka 2019 ikilinganishwa na wanafunzi
452,273 waliofaulu upimaji huo mwaka 2018 sawa na ongezeko la asilimia
13.7,” amesema.
“Kwa upande
wa kidato cha nne, mwaka 2019 wanafunzi 340,914 kati ya wanafunzi
422,722 walifaulu mtihani wa taifa wa kidato cha nne. Ubora wa ufaulu wa
wanafunzi nao umeongezeka kwa mwaka 2019. Kwa mfano, wanafunzi 135,301
sawa na asilimia 32.01 walipata ufaulu mzuri wa daraja la kwanza hadi la
tatu,” ameongeza.
Akielezea
kuhusu maboresho ya miundombinu ya eimu, Waziri Mkuu amesema maboresho
na uwekezaji wa Serikali katika sekta ya elimu yamekuwa chachu ya
kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu na wakati mwingine kuleta changamoto
kwenye miundombinu ya elimu.
“Hata hivyo,
Serikali imeendelea kukamilisha usajili wa shule mpya, kuongeza vyumba
vya madarasa 1,218 na mabweni 14 ili wanafunzi wote waliofaulu kuingia
kidato cha kwanza mwaka 2020, waweze kuanza masomo kwa wakati,”
amesisitiza.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu maboresho kwenye elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema
Serikali imeimarisha elimu ya juu, ufundi na ustawi wa jamii kwa
kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambapo hadi Desemba
mwaka jana, sh. bilioni 266.4 zimetolewa kwa wanafunzi 130,072. “Kati
yao, wanafunzi 49,493 ni wa mwaka wa kwanza na 80,579 wanaoendelea,”
amesema.
Amesema
Serikali imeendelea kujenga mabweni ya wanafunzi wa kike; kukarabati
majengo ya vyuo vikuu na vyuo vya ualimu; kuboresha vyuo vya VETA kwa
kujenga na kuboresha vyuo na kununua vifaa vya kufundishia na
kujifunzia.
“Vilevile,
Serikali imeimarisha vyuo vya maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii kwa
kuanzisha vituo vya ubunifu vitano sambamba na kutekeleza programu ya
uanagenzi ili wapate ujuzi wa kujiajiri unaoendana na ushindani wa soko
la ajira,” amesema.
No comments :
Post a Comment