*****************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali imeboresha utoaji wa huduma za afya kwa
kugharamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo 487 vya kutolea
huduma za afya.
“Maboresho hayo
yanajumuisha vituo vya afya 320, hospitali za halmashauri za wilaya 70,
hospitali za zamani tisa na zahanati 88,” amesema.
Waziri Mkuu
ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Februari 7, 2020) wakati akitoa hotuba ya
kuahirisha Mkutano wa 18 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa
hadi Machi 31, mwaka huu.
Mbali na hayo,
Waziri Mkuu amesema Serikali imejenga na kuboresha miundombinu ya
hospitali za rufaa za Njombe, Simiyu, Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou
Toure, Burigi – Chato, Mwananyamala, na hospitali za rufaa za kanda ya
Kusini Mtwara, kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya, hospitali ya
Kibong’oto na ujenzi wa Isolation centre katika hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Serikali
imekamilisha ujenzi wa nyumba 320 za watumishi wa sekta ya afya pamoja
na kugharamia ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi
kwa gharama ya sh. bilioni 334,” ameongeza.
Amesema katika
kipindi hicho, jumla ya madaktari bingwa 311 wameendelea kulipiwa
gharama za masomo ya uzamili katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi
na kwamba, katika kipindi cha nusu ya pili, Serikali inakusudia kuajiri
zaidi ya watumishi 4,000 wa sekta ya afya.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu ameelezea mafanikio yaliyofikiwa kwenye sekta ya
maji katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019 ambapo sh. bilioni 325.9
zimetolewa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maji ikiwemo uchimbaji wa
visima vifupi, vya kati na virefu.
Amesema fedha
hizo zimetumika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama
vijijini na mijini. Chini ya utekelezaji wa miradi hiyo, miradi 631
inaendelea kujengwa ikiwemo 558 ya maji vijijini na 73 ya maji mijini.
“Miongoni mwa
miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na mradi wa maji
Arusha, mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe na mradi wa kutoa maji
kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa,
Tabora, Igunga, Uyui na Nzega.
Waziri Mkuu
ameema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwahudumia wananchi
sambamba na kuratibu vyema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
kimkakati. Amesema miradi hiyo inayohusisha sekta ya miundombinu
wezeshi, nishati, maji, afya na elimu imekuwa chachu ya kuboresha maisha
ya Watanzania kupitia ukuaji wa sekta rasmi na isiyo rasmi.
No comments :
Post a Comment