Waziri wa Madini, Doto Biteko
akitoa msimamo wa serikali juu ya mgogoro baina ya Magere Mang’era na
Joseph Ocheng Ndugu mara baada ya kusikiliza na kujadili hoja za pande
zote. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na kulia
kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara Prof. Simon Msanjila.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo akizungumza jambo wakati wa kikao kilichokua kikijadili mgogoro
baina ya Magere Mang’era na Joseph Ocheng Ndugu kilichofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa wizara Jijini Dodoma jana.
Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon
Msanjila akizungumza jambo wakati wa kikao kilichokua kikijadili
mgogoro baina ya Magere Mang’era na Joseph Ocheng Ndugu kilichofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa wizara Jijini Dodoma jana.
Mlalamikaji Magere Mang’era
akiwasilisha lalamiko lake mbele ya viongozi waandamizi wa wizara
alipofika katika kikao hicho ili kutatua mgogoro baina yake na Joseph
Ocheng Ndugu.
Joseph Ocheng Ndugu akionesha
mipaka ya eneo lenye mgogoro baina yake na Magere Mang’era wakati wa
kikao kilichofanyika jana tarehe 12/02/2020 katika ukumbi wa mikutano wa
Wizara ya Madini jijini Dodoma.
Waziri wa Madini, Doto Biteko
akizungumza na mmoja wa wajumbe wakisubiri kuanza kwa kikao cha kutatua
mgogoro baina ya Magere Mang’era na Joseph Ocheng Ndugu katika ukumbi wa
mikutano wa Wizara ya Madini jijini Dodoma.
Waziri wa Madini, Doto Biteko
akimwonesha mlalamikiwa moja ya nyaraka yenye udhibitisho katika mgogoro
baina ya Magere Mang’era na Joseph Ocheng Ndugu wakati wa kikao cha
kutatua mgogoro huo. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo na kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara Prof. Simon Msanjila.
fisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara,
Nyaisara Mgaya akielezea hatua zilizofikiwa katika kutatua mgogoro wa
Irasanilo katika kikao kilichohusisha Viongozi Waandamizi wa Wizara,
kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara jijini Dodoma jana
tarehe 12/ 02/2020
………………………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Madini, Doto Biteko
amewataka Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini kutumia Ofisi za Wizara
katika kufikisha changamoto zao badala ya kufikisha kero zao kwa
viongozi wengine wa nchi na serikali wasio na dhamana ya kusimamia Sekta
ya Madini, kwani kufanya
hivyo ni kuchelewesha utatuzi wa kero
zinazowakabili.
Waziri Biteko aliyasema hayo
jana tarehe 12 Februari 2020, wakati wa kikao kilicholenga kumaliza
mgogoro baina ya wachimbaji wadogo Magere Mang’era na Joseph Ocheng
Ndugu waliokuwa wakigombea umiliki wa eneo la mita 23 lililopo katika
leseni ya Irasamilo Gold Mine iliyopo Buhemba Wilaya Butiama mkoani
Mara.
Pamoja na hayo, Waziri Biteko
aliwataka wachimbaji wa Mkoa wa Mara kupunguza migogoro na kuwaeleza
wizara yake inatamani kukutana nao kwa nia njema na si kwa lengo la
kujadili na kutatua migogoro ambayo inarudisha nyuma maendeleo yao na
nchi kwa ujumla.
“Wizara inashughulika na sekta
ya madini nchi nzima, kama kila mchimbaji atataka kuleta malalamiko
yake ofisini kwa waziri basi kazi hazitafanyika.” Tungefurahi kukutana
nanyi kuwaeleza vitu mnavyotakiwa kuviboresha ili kuongeza mapato ni si
kutatua migogoro, Biteko alisisitiza.
Aidha, Biteko ameutaka uongozi
wa mgodi na uongozi wa wachimbaji wadogo ngazi za wilaya na mkoa
(Marema) kuhakikisha kwamba amani inatawala kwa wachimbaji na kuwafanya
wachimbaji wachimbe na kuzalisha kuliko kutengeneza migogoro isiyoisha
inayochangia katika kurudisha nyuma maendeleo yao. “Wanaotafuta pesa
hawatumii muda mwingi kugombana”, amesisitiza Biteko.
Baada ya kufikia hatma ya
mgogoro huo na kumtaka Afisa Madini Mkazi Nyaisara Mgaya kusimamia haki
katika eneo hilo kama kikao kilivyoafiki kuwa mwenye haki ya kupewa eneo
hilo ni Magere Mang’era, Biteko aliwataka wajumbe walioshiriki kikao
hicho kurudi Mara na kuendelea na shughuli za uzalishaji huku wakitunza
amani na ushirikiano miongoni mwao.
Aidha, aliwataka kumtumia
Afisa Madini Mkazi aliyepo katika eneo hilo kama mlezi lakini pia
alimtaka Afisa huyo kuishi na wachimbaji hao vizuri na kudumisha
ushirikiano wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Naibu Waziri
wa Madini, Stanslaus Nyongo aliutaka uongozi wa Wachimbaji wadogo wa
madini (Marema) kusimamia haki kwa wananchi waliowapa dhamana ya
kuwaongoza ili kupunguza migogoro inayojitokeza mara kwa mara.
“Mkoa wa Mara umejaliwa kuwa
na rasilimali madini nyingi, msigeuze neema hiyo kuwa chanzo cha
migogoro na kutishiana maisha”, alisema Naibu Waziri Nyongo.
Aliendelea kusema Neema ya Rasilimali madini inapogeuka na kuwa chanzo cha matatizo na migogoro inahuzunisha.
Aidha, Nyongo alizitaka pande
zote kukubaliana na matokeo na kuwa maamuzi yaliyofikiwa yasiwe chanzo
cha mgogoro mwingine, “naomba kabisa amani itawale”.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Madini, Prof. Simon Msanjila aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuheshimu
maamuzi ya Serikali na kutokuifanya serikali kutumia gharama kubwa
katika kutatua migogoro ya wachimbaji badala yake muda unaotumika
kutatua migogoro utumike kukusanya mapato ya serikali.
“Tumeweka ofisi za madini
mikoani ili kupunguza matatizo madogo madogo kuletwa wizarani hivyo
mzitumie ofisi hizo na kuamini maamuzi yanayotolewa na viongozi katika
mikoa yenu yanakuwa Baraka zetu”. Msanjila alisisitiza.
Prof. Msanjila aliwahakikishia
wajumbe kuwa maamuzi yaliyofikiwa na Wizara ni sahihi na ya mwisho na
kubainisha kuwa endapo hawakubaliani na maamuzi hayo basi wasingefika
katika kikao hicho.
Profesa Msanjila alisisitiza
kuwa, mlango sahihi wa kutatua migogoro katika sekta ya madini ni Wizara
ya Madini vinginevyo ni kupoteza muda na rasilimali.
Kwa upande wa wajumbe
walioshiriki kikao hicho wengi walikiri kuwa mwenye haki ya kupewa eneo
lililokuwa na mgogoro ni Magere Mang’era na kwa Mamlaka aliyonayo Waziri
aliamuru eneo lenye mgogoro apewe mlalamikaji na kuhitimisha mjadala
juu ya mgogoro huo.
No comments :
Post a Comment