Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akizungumza jambo katika hafla ya
utiaji saini mikataba minne ya mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa
barabara ya Kabingo – Kasulu -Manyovu (Km 260), mkoani Kigoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, akisoma taarifa
fupi ya utiaji saini mikataba minne ya mradi wa ujenzi kwa kiwango cha
lami wa barabara ya Kabingo – Kasulu -Manyovu (Km 260), mkoani Kigoma.
Wakurugenzi kutoka Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) pamoja na Wabunge wa
Mkoa wa Kigoma wakisikiliza hotoba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (hayupo pichani), katika hafla ya
utiaji saini mikataba minne ya mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa
barabara ya Kabingo – Kasulu -Manyovu (Km 260), mkoani Kigoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (Wanne kulia pamoja na viongozi
wengine wa Serikali wakishuhudia tukio la utiaji saini mikataba minne ya
mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kabingo – Kasulu
-Manyovu (Km 260), mkoani Kigoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale (kushoto), pamoja
na mmoja wa wakandarasi waliosaini mikataba minne ya mradi wa ujenzi
kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kabingo – Kasulu -Manyovu (Km 260),
wakionesha hati za mikataba hiyo mara baada ya kusaini, mkoani Kigoma.
PICHA NA WUUM
………………………………………………………………………………………………………
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), imesaini
mikataba minne
ya mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kabingo –
Kasulu – Manyovu mkoani Kigoma, yenye urefu wa kilometa 260.Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo mkoani humo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36 na utagharimu
Jumla ya shilingi bilioni 585.
“Leo tupo hapa tukiwa na furaha kubwa kushuhudia tukio hili muhimu na la kihistoria katika mkoa huu, kusainiwa kwa mikataba hii ni kutimia kwa ndoto na ahadi ya Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli ya kuifungua Kigoma kiuchumi na kijamii kwa kuiunganisha kitaifa na kimataifa kutokana na barabara hii kuunganisha nchi za jirani za Burundi, Rwanda na DRC – Congo”, amesema Mhandisi Kamwelwe.
Waziri Kamwelwe ametaja
makampuni yaliyopata zabuni ya kutekeleza mradi huo kuwa ni Zhejing
Communication Construction Group Company Ltd (ZCCC), Sinohydro
Corporation Ltd, Stecol Corporation na China Henan International
Corporation (CHICO) ambapo utekelezaji wa mradi huo umegawanywa sehemu
nne.
“Kama ambavyo mmemsikia Mtendaji
Mkuu wa TANROADS kuwa mradi huu utatekelezwa na makandarasi hawa kwa
sehemu nne, sehemu ya kwanza itahusisha ujenzi wa barabara kuanzia
Kasulu junction – Manyovu na viunganishi vya barabara za Kasulu
mjini (Km 68.25), sehemu ya pili itakuwa ni Kanyani- Kidyama- Mvugwe (Km
70.5), ya tatu ni Mvugwe- Njia panda ya Nduta (Km 59.35) na ya mwisho
ni Nduta junction – Kabingo junction (Km 62.5),” amefafanua Mhandisi Kamwelwe.
Aidha, Mhandisi Kamwelwe amewataka makandarasi waliopata zabuni ya ujenzi wa barabara hiyo kuhakikisha wanatekeleza ujenzi wake kwa mujibu wa mikataba na kuwasisitiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha wanawasimimia makandarasi hao ili kupata barabara yenye kiwango sawa na thamani ya fedha iliyotumika.
Waziri Kamwelwe, ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuboresha miundombunu ya barabara katika uwanda wa magharibi ili kuifungua Kigoma na mikoa mingine ya jirani.
“Serikali hii hailali inafanya kazi usiku na mchana, miradi ya ujenzi wa barabara kama ya Chaya – Nyahua (km 85.4), Chagu- Kazilambwa (km 36) na Kaliua – Urambo (km 28) inaendelea kujengwa na inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu”, amebainisha Kamwelwe.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale, amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kati ya Mkoa huo na mikoa ya jirani pamoja na nchi jirani za Rwanda, Burundi na DRC- Congo
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma
Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga, amesema kuwa ujio wa mradi
huo mkoani kwake utapelekea uzalishaji wa ajira kwa vijana na kuimarika
kwa huduma za usafiri na usafirishaji.
No comments :
Post a Comment