********************************
Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Ulega amewahakikishia wadau wote wanaokusudia kuwekeza
kwenye sekta ya Mifugo na Uvuvi kuwa Serikali ya awamu ya tano ipo
tayari kuondoa changamoto zote zinazowakabili katika uwekezaji wao na
kuwawekea
mazingira rafiki ya kuendesha shughuli zao hapa nchini.
Mhe. Ulega aliyasema hayo jana
(12.02.2020) muda mfupi kabla ya kufungua kituo cha ufugaji wa samaki
kwa njia za kisasa kinachojulikana kama “Big Fish” kilichopo Wilaya ya
Kigamboni jijini Dar-es-salaam.
“Ninatambua kuwa vifaa
vinavyoletwa hapa nchini kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kukuza
sekta mtambuka huwa vinaondolewa tozo mbalimbali hivyo nimemuagiza
Katibu Mkuu wa sekta ya Uvuvi ashughulikie nyaraka za msingi tuweze
kuziwasilisha kwenye mamlaka husika ili hata vifaa vinavyoletwa nchini
kwa ajili ya kukuza sekta ya uvuvi viondolewe kodi na tozo hizo” Alisema
Mhe. Ulega.
Mhe. Ulega alisema kuwa kwa hivi
sasa takwimu zinaonesha Tanzania inazalisha jumla ya samaki tani elfu 18
kupitia shughuli za ufugaji wa samaki kwa kutumia mabwawa na lengo ni
kuhakikisha idadi hiyo inaongezeka na kufikia tani elfu 50.
“Hitaji la samaki kwa sasa hapa
nchini ni tani laki 7 hadi 8 na uwezo wetu wa kuzalisha samaki kwa njia
zote mpaka kufikia mwaka 2018/19 tumezalisha tani laki 4.4 hadi 4.5
hivyo hili ombwe la takribani tani laki 4 ni fursa nzuri kwa watanzania
kupitia kwa wadau mbalimbali kuhakikisha tunalifikia na kupita hitaji la
taifa” Alisisitiza Mhe. Ulega.
Awali kabla ya kumkaribisha Mhe.
Naibu waziri, Balozi wa Uholanzi nchini Bw. Jeroen Verheul aliisifu
Tanzania kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wenye nia ya kutekeleza
miradi mbalimbali hapa nchini ambapo alitoa rai kwa wadau wengine
kuendelea kubuni miradi ambayo haitaathiri mazingira.
“Tukio la leo linaashiria ni kiasi
gani ushirikiano baina ya nchi ya Uholanzi na Tanzania ni imara na
unatekelezwa kwa vitendo sio tu kuishia kwenye makaratasi”Aliongeza Bw.
Verheul.
Takwimu zinaonesha kuwa mpaka sasa
kila Mtanzania anakula wastani wa kilo 8 za samaki kwa mwaka huku
mpango wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ukiwa ni kuhakikisha kufikia 2025
kila Mtanzania awe anakula kilo 10 za samaki kwa mwaka.
No comments :
Post a Comment