Mkuu wa Wilaya ya Kahama,
Anamringi Macha akielezea mafanikio ya Soko la Madini la Kahama na vituo
vya ununuzi wa madini kwa wanahabari kutoka Idara ya Habari MAELEZO
(hawapo pichani) tarehe 06 Februari, 2020.
Mchambuzi wa Madini ya Almasi wa
Tume ya Madini Nelson Magawa, akithaminisha baadhi ya madini ya almasi
katika Soko la Kimataifa la Madini ya Almasi na Dhahabu lililopo mjini
Shinyanga.
Mfanyabiashara kutoka kampuni ya
Fretja Natural Energy Resources Tanzania Ltd, Teddy Goliama (kulia)
akipima madini ya almasi ya mteja katika Soko la Kimataifa la Madini ya
Almasi na Dhahabu lililopo mjini Shinyanga.
*******************************
Wadau mbalimbali wa madini pamoja na viongozi waandamizi katika
mkoa wa Shinyanga wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. John Magufuli, Wizara ya Madini pamoja na Tume ya Madini kwa hatua
ya uanzishwaji na usimamizi wa masoko ya
madini na vituo vya ununuzi wa
madini kwani yameleta mabadiliko ya kiuchumi katika mkoa wa Shinyanga.
Wakizungumza na timu ya maafisa
habari kutoka Idara ya Habari MAELEZO na Tume ya Madini kwenye ziara ya
maandalizi ya vipindi vinavyohusu mafanikio ya masoko ya madini katika
mkoa wa Shinyanga leo tarehe 06 Februari, 2020 mbali na kupongeza juhudi
zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, wameeleza kuwa masoko ya
madini yameleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na ajira,
mapato kwa Serikali na kuongeza kasi ya ukuaji wa shughuli za uchimbaji
wa madini katika mkoa huo.
Akizungumza ofisini kwake Mkuu wa
Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha alisema kuwa, kabla ya kuanza kwa
masoko ya madini katika Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Ofisi ya Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga ilikuwa inakusanya jumla ya kiasi cha
shilingi milioni 593.6 kwa mwaka, lakini baada ya masoko kuanzishwa
mapema Julai mwaka jana hadi kufikia Januari, 2020 ofisi hiyo imeweza
kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 9.7.
Macha alieleza mafanikio mengine
kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa udhibiti wa utoroshwaji wa madini hali
iliyopelekea uzalishaji wa madini katika Mkoa wa Kimadini wa Kahama
kuongezeka kutoka kilo 100 kwa mwaka hadi kilo 1572 tangu kuanzishwa kwa
masoko ya madini.
Aliongeza kuwa elimu ya uzalendo imekuwa ikitolewa mara kwa mara
kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ambapo katika Wilaya ya
Kahama kila mchimbaji anapopata madini hupeleka katika Soko la Madini la
Kahama na vituo vya ununuzi wa madini na kupata faida kubwa pasipo
kudhulumiwa.
Katika hatua nyingine, Macha
aliwataka masonara kupokea madini kutoka kwenye masoko ya madini
yaliyoanzishwa badala ya kununua moja kwa moja kwa wachimbaji na
kuongeza kuwa kutotumia masoko ya madini yaliyoanzishwa ni kinyume na
sheria.
Aidha, mbali na kumpongeza Rais
Magufuli, Waziri wa Madini, Doto Biteko na Tume ya Madini kwa ujumla,
Macha alitumia fursa hiyo kupongeza vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo
vimekuwa vikifanya kazi usiku na mchana katika udhibiti wa utoroshwaji
wa madini nchini.
Pia, aliwataka wawekezaji
wanaopewa leseni za utafiti wa madini kuanza shughuli za utafutaji wa
madini badala ya kuacha maeneo kukaa wazi kwa muda mrefu hali
inayopelekea kuvamiwa na kuleta migogoro.
Naye mfanyabiashara mdogo wa
madini aina ya almasi katika Soko la Kimataifa la Madini ya Almasi na
Dhahabu lililopo mjini Shinyanga, Jafari Kashinde alisema kuwa soko hilo
limeleta mabadiliko makubwa kwenye biashara ya madini ya almasi katika
mkoa wa Shinyanga kwa kuwa kabla ya kuanzishwa kwa soko hilo biashara
ilikuwa ikifanyika kwa kificho na madini kutopatikana kwa urahisi.
Alieleza manufaa mengine ya soko
hilo kuwa ni pamoja na kufanyiwa uthaminishaji wa madini hayo na
wataalam kutoka Tume ya Madini hivyo kuepushwa na utapeli na
wafanyabiashara wasio waaminifu.
Naye mfanyabiashara wa madini kutoka kampuni ya Tripple A
Diamond Group Co ltd, Ali Ahmed aliongeza kuwa manufaa mengine katika
soko hilo ni pamoja ulinzi ulioimarishwa na mazingira mazuri ya ulipaji
kodi yaliyowekwa na Tume ya Madini.
Aidha, mfanyabiashara mwingine wa
kutoka kampuni ya Fretja Natural Energy Resources Tanzania Ltd, Teddy
Goliama mbali na kuipongeza Serikali kwa uanzishwaji wa soko hilo,
aliongeza kuwa heshima kwa nchi kwenye umiliki wa uchumi wa madini
imeongezeka kwa kuwa awali madini yalikuwa yakitoroshwa nje ya nchi na
wafanyabiashara wasio waaminifu hivyo kudhaniwa yanapatikana nchi
nyingine.
“Mfano hai ni madini ya Tanzanite
ambayo yanapatikana Tanzania pekee, kabla ilikuwa inafahamika
yanapatikana pia katika nchi nyingine kutokana na kutoroshwa kwa wingi
lakini baada ya ujenzi wa ukuta wa Mirerani na uanzishwaji wa masoko ya
madini, sasa inafahamika kuwa madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania
pekee,” alisisitiza Goliama.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Shinyanga Vijijini, Hoja Mahiba alisema kuwa, mara baada
ya kuweka utaratibu mzuri wa usimamizi wa uchimbaji wa madini katika
eneo la wachimbaji wadogo wa madini la Mwakitolyo eneo hilo limeanza
kuzalisha gramu 300 hadi gramu 500 kwa siku tofauti na awali ambapo
kulikuwa hakuna kinachopatikana.
Aliongeza kuwa mafanikio mengine
kuwa ni pamoja na halmashauri ya Shinyanga Vijijini kukusanya kiasi cha
shilingi milioni 77 kwa nusu mwaka wa fedha 2019/2020 tofauti na mwaka
2018/2019 ambapo walikusanya shilingi milioni 73 tu.
No comments :
Post a Comment