Dkt Charles Mwamwaja Kamishna wa
Sekta ndogo ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango akiwasilisha mada katika
semina ya wahariri wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kuhusu
utoaji elimu ya Sera, Sheria, Kanuni za biashara ya huduma ndogo za
fedha inayofanyika kwenye hoteli ya Nashera mjini Morogoro.
Bi. Dionisia Mjema Kaimu Kamishna
Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha
akifafanua jambo wakati alipokuwa akiwasilisha mada katika semina hiyo
leo kwenye Hoteli ya Nashera mjini Morogoro.
MKuu wa Mawasiliano na Msemaji
Mkuu wa Wiazara ya Fedha na Mipango Bw. Ben Mwaipaja akitolea ufafanuzi
katika baadhi ya mambo yaliyojitokeza katika semina hiyo.
Bw. Shanil Mayosa Mwanasheria
kutoka tume ya Ushirika ni miongozi mwa wataalamu waliotoa mada kwa
wahariri wa vyombo vya habari na waandishi leo mjini Morogoro.
Bi. Ng’waka Mong’ateko Meneja
Msaidizi Idara ya Huduma Ndogo za Fedha na Maduka ya Kubadilishia Fedha
za Kigeni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) akiwasilisha mada katika
semina hiyo
Wadau mbalimbali wakiwa katika semina hiyo.
Baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali na waandishi wa habari wakifuatilia mjadala katika semina hiyo.
Kutoka kushoto ni Kamishna
anayesimamia Sekta Ndogo ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha , Dkt. Charles
Mwamaja, Bi. Dionisia Mjema Kaimu Kamishna Msaidizi Idara ya Maendeleo
ya Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha na Meneja Msaidizi wa Idara ya Uhusiano wa BOT, Vicky Msina pamoja na washiriki wengine wa semina hiyo wakifuatilia mada mbaimbali zilizokuwa zikiendelea.
……………………………………………………
KATIBU MKuu Wizara ya Fedha na
Mipango, Doto James, amesema Sekta Ndogo ya Fedha ni miongoni mwa sekta
muhimu katika uchumi wa nchi.
Alisema sekta hiyo inatoa huduma
za fedha kwa wananchi wa kipato cha chini na kati ambazo
zinachangia
kuinua uchumi na kuongeza kipato.
Kamishna anayesimamia Sekta Ndogo
ya Fedha kutoka Wizara hiyo, Dkt. Charles Mwamaja aliyasema hayo mkoani
Morogoro kwa niaba ya James kwenye semina iliyoshirikisha Wahariri wa
vyombo mbalimbali nchini ikihusu utoaji elimu ya Sera, Sheria, Kanuni za
biashara ya huduma ndogo za fedha.
Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa
utafiti wa Finscope wa mwaka 2017, asilimia 55.3 ya nguvukazi ya Taifa
wanapata huduma za fedha kutoka taasisi za huduma ndogo za fedha
Kutokana na umuhimu wa Sekta
hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilifanya mapitio ya
Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2000 na kutunga Sera ya
Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017.
Sera hiyo pamoja na mambo
mengine, imeelekeza kutungwa kwa Sheria mahsusi ya kusimamia na
kuendeleza sekta ya huduma ndogo ya fedha ili kuondoa changamoto za
kisheria zilizokuwepo ambazo ziliathiri usimamizi, udhibiti na ustawi wa
sekta hiyo.
Miongoni mwa changamoto hizo ni
pamoja na taasisi za huduma ndogo za fedha kutoa mikopo kwa wananchi kwa
vigezo, masharti magumu hivyo kusababisha madhara kwa wananchi.
Madhara hayo ni pamoja na viwango
vikubwa vya riba, tozo na kukosekana kwa uwazi wa masharti ya mikataba
ya mikopo, utoaji holela wa mikopo unaosababisha limbikizo la madeni kwa
wateja.
Aliyataja madhara mengine ni
utaratibu usiofaa wa ukusanyaji madeni unaosababisha wananchi kupoteza
mali zao, kujitokeza kwa baadhi ya wananchi wasio waaminifu wanaotumia
mwanya wa kutokuwepo sheria mahsusi kutoa huduma ndogo za fedha.
Mashara mengine ni kuwepo kwa
baadhi ya taasisi za huduma ndogo za fedha zisizotoa gawio au faida kwa
wanachama, wateja wanaoweka fedha kati ya asilimia 25 hadi 30 kama
dhamana ya mikopo, ukosefu wa takwimu ama taarifa sahihi za uendeshaji
taasisi za watoa huduma ndogo za fedha.
James alisema pia kukosekana
takwimu, taarifa tajwa husababisha Serikali kutojua mchango wa sekta
ndogo ya fedha katika uchumi wa Taifa, ukosefu wa utaratibu wa kuwalinda
watumiaji wa huduma ndogo za fedha.
Pia kuwepo kwa mianya ya
utakasishaji fedha haramu kutokana na taasisi za huduma ndogo za fedha
kutokuwa na utaratibu wa kisheria unaozitaka kutekeleza matakwa ya
Sheria ya Udhibiti wa Utakasishaji wa Fedha Haramu.
Ili kutatua changamoto
zinazoikabili Sekta Ndogo ya Fedha kama nilivyobainisha katika maelezo
ya awali, Serikali ilitunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka
2018 (The Microfinance Act, 2018).
Lengo la sharia hiyo, kwanza ni kuzitambua
taasisi za huduma ndogo za fedha katika madaraja manne, daraja la
kwanza ni taasisi za huduma ndogo za fedha zinazopokea amana, pili
taasisi zisizopokea amana wakiwemo wakopeshaji binafsi, watoa huduma kwa
njia ya kielekroniki, kampuni za mikopo.
Daraja la Tatu ni vyama vya
Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na daraja la nne ni vikundi vya
kijamii vya huduma ndogo za fedha kama VICOBA, VSLA.
Sheria hiyo imeanza kutumika
rasmi Novemba Mosi, 2019, pamoja na mambo mengine imeainisha kuwa
ifikapo Oktoba 31, mwaka huu, kila mtoa huduma ndogo za fedha lazima awe
amekata leseni au kusajiliwa kufanya biashara ya huduma ndogo za fedha
kwa kuzingatia daraja husika.
“Tayari zimeandaliwa kanuni
mahsusi na kanuni za jumla kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Waziri ya
kisera, kuhamasisha, usimamizi na kuendeleza sekta ndogo ya fedha,”
alisisitiza.
Kwa upande wake, Dkt. Mwamaja
alisema sekta hiyo imepitia changamoto nyingi ambazo zilisababisha
Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kufanya mapitio ya Sera ya
Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2000 na kutunga Sera ya Taifa ya
Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017.
Lengo la kuwepo kwa Sera, Sheria
na Kanuni hizo ni kuweka mazingira wezeshi ya usimamizi, uendelezaji
sekta ya huduma ndogo za fedha nchini ili kuondoa changamoto
zilizokuwepo katika sekta hiyo iweze kutoa mchango mkubwa ili kukuza
uchumi na kuondoa umaskini.
“Semina hii imeandaliwa na Wizara
ya Fedha ikishirikiana na wadau wengine wakiwemo Ofisi ya Raisi-
TAMISEMI, Benki Kuu ya Tanzania, Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na
Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Mfuko wa Kuendeleza
Sekta ya Fedha (FSDT),” alisema.
No comments :
Post a Comment