*****************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Februari 2, mwaka huu laini za simu
milioni 31.4 kati ya laini za simu milioni 43.9 (sawa na asilimia 71.6)
zilikuwa zimeshasajiliwa kwa alama za vidole.
Ametoa kauli
hiyo leo (Ijumaa, Februari 7, 2020) katika hotuba yake aliyoitoa
wakati kuahirisha Mkutano wa 18 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge
limeahirishwa hadi Machi 31, mwaka huu.
Amesema zoezi
la usajili wa laini za simu ni endelevu na akatumia fursa hiyo
kuwahimiza wananchi ambao hawajasajili laini zao za simu na wale ambao
wanaendelea na zoezi la kupata vitambulisho vya uraia na wamekwishapata
namba za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), wasajili laini zao za
simu kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu wa kusitishiwa huduma za
mawasiliano.
“Ninatoa wito
kwa NIDA, isogeze huduma za kutoa namba za vitambulisho karibu na
wananchi kwa kadiri inavyowezekana. Lengo ni kutoa fursa kwa wananchi
wengi zaidi ili wapate kupata namba za vitambulisho na kuwawezesha
kusajili laini zao za simu na vilevile, kupata Vitambulisho vya Taifa
kwa matumizi mengine muhimu,” amesema.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeendelea na
zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu ya
kwanza.
“Hadi kufikia
tarehe 2 Februari, 2020, Tume ya Uchaguzi imekamilisha uandikishaji wa
wapiga kura katika kanda ndogo 12 kati ya 14 zilizopangwa katika ratiba
ya uboreshaji wa awamu ya kwanza,” amesema.
Amesema kanda
ndogo zilizokamilisha zoezi hilo zinahusisha mikoa 22 ya Arusha,
Kilimanjaro, Manyara, Mara, Simiyu, Mwanza, Geita na Shinyanga. Mingine
ni Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa, Tabora, Singida, Dodoma, Songwe,
Mbeya, Iringa, Ruvuma, Njombe, Lindi, Mtwara, Tanga, Morogoro (Ulanga DC
na Malinyi DC) na Tanzania Zanzibar.
Amesema zoezi la uboreshaji kwenye kanda ndogo ya 13 inayohusisha mkoa wa Morogoro, lilianza Februari 3, 2020 na linatarajiwa kukamilika Februari 9, 2020.
“Uandikishaji
wa wapiga kura ni wa siku saba kwa kila kituo cha kuandikisha wapiga
kura. Aidha, zoezi la uboreshaji linahusisha uandikishaji wa wapiga kura
wapya ambao hawajahi kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga
kura, urekebishaji wa taarifa za wapiga kura walioandikishwa katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuondoa taarifa za wapiga kura
waliopoteza sifa ikiwemo kufariki.
“Idadi ya
wapiga kura walioandikishwa kuanzia kanda ndogo ya kwanza hadi ya 12
walikuwa 18,058,977. Jumla ya wapiga kura 2,012,212 wamejitokeza
kuboresha taarifa zao sawa na asilimia 11.14 ya idadi ya wapiga kura
walioandikishwa mwaka 2015 katika kanda ndogo zote 12,” amesema.
Amesema idadi ya
wapiga kura wapya walioandikishwa katika kanda ndogo zote 12 ni
5,666,343 ambayo ni sawa na asilimia 31.38 ya idadi ya wapiga kura
walioandikishwa mwaka 2015 katika kanda ndogo zote 12. “Hii ni sawa na
ongezeko la asilimia 14.38 la makadirio ya awali (asilimia 17).
Vilevile, idadi ya wapiga kura walioondolewa kwa kupoteza sifa ni 14,894
ambayo ni sawa na asilimia 0.08 ya idadi ya wapiga kura walioandikishwa
mwaka 2015 katika kanda ndogo zote 12.
Waziri Mkuu
ametumia fursa hiyo kuihamasisha Tume ya Uchaguzi iharakishe zoezi la
uandikishaji. “Nitumie nafasi kutoa wito kwa Tume iongeze kasi ya
uandikishaji. Pia, natoa rai kwa wananchi watumie haki yao hiyo ya
kikatiba na wajitokeze kwa wingi kuboresha taarifa zao na kujiandikisha
upya kwa wale wenye umri wa miaka 18 au watakaofikisha umri huo ifikapo
Oktoba, 2020,” amesema.
No comments :
Post a Comment