Tuesday, February 4, 2020

DKT NCHIMBI AJA NA NAMJALI MTOTO WA KIKE KWA MAENDELEO YA TAIFA,RAS DKT LUTAMBI APIGILIA MSUMARI


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi  (mwenye nguo za kijani ) akiwapatia wanafunzi  wa Shule ya Sekondari Ikungi boksi la  taulo za kike. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi(mwenye suti nyeusi) Edward Mpogolo, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi
 Wanafunzi wa shule ya Sekondari  ya Ikungi wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi  mara baada ya kupokea maboksi ya taulo za kike kutoka kwa wadau mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Singida  Dkt. Rehema Nchimbi (mwenye skafu) na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi wakijadiliana  mara baada ya kutoka kwenye mkutano wa mafanikio  ya miaka 4 ya Rais Magufuli ambapo Waziri wa TAMISEMI Suleimani Jaffo alipongeza jitihada za Mkoa wa Singida kwenye utoaji wa huduma za afya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi (mwenye suti ya Bluu)  akiwa  pamoja na Mganga Mkuu wa Mkoa Singida, Victorina Ludovick (mwenye sketi nyeusi)na Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Singida(mwenye suruali nyeusi), Mwalimu Eva Simon Mosha wakicheza kuhamasisha uchangiaji wa taulo za kike.
Na John Mapepele
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi  ametoa onyo kali kwa wawekezaji na
wafanyabiasha wa kutengeneza na kuuza taulo za watoto wa kike  kuacha
mara moja tabia ya kutengeneza taulo zisizo  na ubora kwa kuwa Mkoa wake umeanzisha msako
wa kiintelijensia na kistratejia wa kuzisaka taulo zisizo na ubora  ambapo
atakayebainika sheria itachukua mkondo wake mara moja.
Dkt Nchimbi ameyasema haya leo wilayani Ikungi wakati wa
zoezi maalum la uzinduzi wa uchangishaji wa taulo za mtoto wa kike katika Mkoa
wa Singida lililopewa jina la “Mjali mtoto wa kike kwa maendeleo yake na
Taifa lake
” ambapo ametoa rai kwa wadau wote kushiriki kikamilifu
katika kuwabaini na kutoa taarifa za wafanyabiashara watakaojaribu kuuza taulo
zisizo na ubora ili kuwalinda watoto wa kike
Alisema kutokana na mageuzi makubwa ya kiuchumi yanayofanywa
na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli nchi yetu
imekuwa kwenye mashindano ya kiuchumi duniani hivyo mikakati madhubuti ya
kudhibiti ubora unahitajika katika kipindi hiki kuliko kipindi kingine
chochote.
Dkt Nchimbi alisema vyombo vya dola, viongozi wa dini na
wazazi wana mchango mkubwa katika kumlinda mtoto wa kike kwa ustawi wa taifa
letu.
“Ndiyo maana tunasema na tunamaanisha kuwa tunataka kujua
mipango ya udhibiti wa ubora kwa watengenezaji hawa kwa kuwa majuto ni mjukuu,
tusisubiri kufika huko “ alisisitiza Dkt .Nchimbi
Aliongeza kuwa ubora
wa taulo za kike ni ubora wa maisha yao hivyo ni muhimu  kuchukua hatua za kuangalia na kudhibiti mnyororo
mzima wa uzalishaji na usambazaji wa taulo sizizo kuwa na ubora.
Aidha alitoa wito wa wajasiliamali kuja na andiko zuri la
utengenezaji wa taulo bora za kisasa zitakazotengenezwa kwa kutumia malighafi
za hapa nchini ambapo alisema mshindi atakayepatikana atamzawadia tuzo  ya shilingi milioni moja.
Aliwataka watoto wa kike kote nchini kujiamini kwa  kuumbwa wanawake na kwamba hedhi ni kitu cha
thamani kwa kuwa hedhi ni uhai ambapo alisisitiza  elimu ya jinsia na mtoto wa kike kutambua
mabadiliko ya miili yao iendelea kutolewa ili kuwajenga watoto wa kike kujua
thamani ambayo mungu amewajalia kwa kuwaumba wakamilifu.
Aliwataka wadau wote kuendelea kuchangia kwa kutambua thamani
ya mtoto wa kike ambapo katika  uzinduzi
wa huu lengo lilikuwa ni kuchangia paketi 8000 za taulo za kike lakini
zilipatikana jumla ya paketi 9089 kulingana na fedha zilizotolewa.
Lengo la jumla kwa mwaka 2020 katika Wilaya ya Ikungi ni
kuchangia taulo 192,000 kwa watoto wote wa kike kwenye shule 36 za
Sekondari,  na shule  131 za Msingi
zenye jumla ya  watoto wa kike
16,000
Naye KatibuTawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina  Lutambi amesema Serikali imeendelea kutoa
kipaumbele katika huduma za afya zenye ubora na zinazowafikia wananchi wote ili
kuboresha afya zao.
Dkt. Lutambi amesema Serikali inatambua umuhimu wa afya bora
kwa wananchi wake kwani afya bora ni raslimali muhimu kwa maendeleo. Maendeleo
ya Taifa letu la Tanzania yataletwa na wananchi wenye afya na wenye uwezo wa
kuzalisha mali.
Aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa wananchi wana afya
bora, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa huduma za afya
kwa kuzingatia sera na miongozo iliyopo.
“Serikali
haitamfumbia macho mdau yoyote wa utoaji wa huduma ya afya ambaye atafanya
kazi   kwa mazoea bila kuzingatia  sheria na taratibu za utoaji huduma na kwamba
kuanzia sasa Serikali itakaa na kupanga
kwa pamoja ili
kuwapatia wananchi huduma  bora wakati wote kwa
wananchi wa Mkoa wa Singida na taifa kwa ujumla” amesisitiza Dkt. Lutambi
Aidha, Waziri wa Nchi,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)
Selemani Jafo, amepongeza juhudi zinazofanywa
na Serikali ya Mkoa wa Singida kwenye  utoaji wa huduma za afya  wakati akiwasilisha  mafanikio ya TAMISEMI kwa kipindi cha miaka
mine ya Rais Magufuli
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi
alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa wazo la kutaka Halmashauri zote katika Mkoa wa
Singida kutoa elimu ya jinsia mashuleni na kuwachangia wa watoto wa kike taulo
hizo kwa kuwa jambo lenye manufaa kwa taifa kwa kuwa ukimuelimisha mtoto  wa kike umeelimisha taifa zima.
Alizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili watoto wa kike
kuwa ni pamoja na mimba za utotoni,kubakwa,kuozeshwa katika umri mdogo na
kufanyishwa kazi  nyingi nyumbani.
Mratibu wa program hii ya
uchangiaji wa taulo za mtoto wa kike ambaye pia ni Afisa Maendeleo wa
jamii wilaya ya Ikungi Haika Massawe alipendekeza wazazi wahusishwe kikamilifu
katika  program hii.
Alisema vyombo vya Serikali
kama polisi na mahakama
vitende  haki katika kushughulikia
haki za mtoto wa kike aidha  wazazi wa
wanafunzi wa kike mashuleni  waelekezwe
kutoa fedha  maalum kwa ajili ya kununua
taulo za watoto wao.

No comments :

Post a Comment