
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali Bungeni jijini Dodoma, Januari 30, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na
Rais
Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kukemea utendaji usioridhisha pale
inapoona mambo hayaendi sawa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo na
Zanzibar.
Maagizo
aliyoyatoawakati alipotembelea kiwanda cha kuzalisha sukari cha Zanzibar
kilichopo Mahonda, wilaya ya Kaskazini ‘A’, mkoa wa Kaskazini Unguja ni
sahihi kwa kuwa yanalenga kuboresha maendeleo na kulinda wawekezaji.
Waziri Mkuu
ameyasema hayo leo (Alhamisi, Januari 30, 2020) wakati akijibu swali la
Mheshimiwa Jaku Hashimu Ayoub (BLW) katika kipindi cha maswali ya papo
kwa papo kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kufahamu ni lini Serikali
itaruhusu sukari inayozalishwa na kiwanda cha Sukari Zanzibar iuzwe
Tanzania Bara.
Amesema
alipofanya ziara Januari 18, 2020 katika kiwanda hicho, alikuta tani
3,200 zikiwa hazijanunuliwa. “Nilipofika kiwandani hapo nilikuta sukari
nyingi kwenye bohari kwa madai kuwa imekosa soko. Ingawa mbunge amesema
anahitaji soko la Tanzania Bara lakini mahitaji ya sukari Zanzibar ni
tani 36,000 kwa mwaka na kiwanda kinazalisha 6,000.”
Waziri Mkuu
amesema mpango wa uagizaji sukari kutoka nje ya nchi hauko sahihi kwani
wanunuzi walitakiwa kwanza wanunue sukari inayozalishwa ndani ndipo
waagize nje kiasi kinachopungua.“Haiwezekani sukari inayozalishwa ndani
ikakosa soko kutokana na uingizwaji wa sukari kutoka nje. Hii inawavunja
moyo wawekezaji wetu,” amesema.
Hivyo,
amesema yeye na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi
ndio wenye jukumu la kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM
na kwamba suala la viwanda limo katika utekelezaji wa ilani hiyo.
“Ninapokuta
Ilani haitekelezeki popote pale nchini lazima niwe mchungu, lazima
tuweke mpango wa kuwalinda wawekezaji wa ndani na kuwahakikishia masoko
na tunajua masoko hayo tunayo,” amesema.
“Pale wapo
waagizaji wa sukari watatu tu, sasa kwanini wasipewe masharti rahisi ya
kuanza kununua sukari ya ndani na kiasi kinachopungua ndio waagize.
Lazima tulinde viwanda vyetu… halafu mtu anasema nimewachefua
Wazanzibari. Hivi nimewachefua Wazanzibari ama nimewachefua wanunuzi?”
amehoji.
Amesema sera
ya nchi inasisitiza umuhimu wa kulinda wazalishaji wa ndani ambao bidhaa
zao zimethibitishwa na mamlaka husika. Hivyo, ni lazima kuwalinda
wawekezaji kwa kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika.
Waziri Mkuu
amesema viwanda vinasaidia katika kuondoa tatizo la ajira, vinawapa
wakulima soko la uhakika la mazao yao pamoja na Serikali kupata kodi ya
uhakika. “Kiwanda kile kimeajiri watu 400 na Serikali inapata kodi
zinazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.”
Amesema:
“Mwekezaji asipozalisha, wale wananchi hawana ajira. Asipozalisha,
atakosa mishahara ya kuwalipa wafanyakazi wake. Atashindwa kulipa kodi.
Kutokana na kodi hizi, tumeona maabara inajengwa Bwejuu na kituo cha
mama na mtoto pale Bambi; hivyo tutakuwa wakali pale ambapo mambo
hayaendi.”
No comments :
Post a Comment