
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali Bungeni jijini Dodoma, Januari 30, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma China
ambao wapo nchini kwa likizo wasiwaruhusu warudi hadi hapo Serikali
itakapotangaza.
Hatua hiyo
inatokana na China kukumbwa na mlipuko wa homa kali ya mapafu
inayosababishwa na virusi vya corona. “Tunawasihi watoto wasirudi hadi
hapo tutakapopata
taarifa za kidiplomasia kuhusiana na maendeleo ya
ugonjwa huo.”
Waziri Mkuu
ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Januari 30, 2020) wakati akijibu swali
la Mbunge wa Mafinga Mjini, Mheshimiwa Cosato Chumi katika kipindi cha
maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma. Mbunge
huyo alitaka kujua namna Serikali ilivyojipanga kukabiliana na homa hiyo
pamoja na baa la nzige.
Waziri Mkuu
Majaliwa amesema ni kweli China kuna mlipuko wa homa hiyo ya mapafu
ambayo hadi sasa imepoteza maisha ya watu wengi na tayari baadhi ya nchi
jirani nazo wananchi wake wameanza kupata maambukizi. “Watoto wasirudi
hali ikikaa vizuri warudi China kuendelea na masomo na ikiwa vinginevyo
Serikali itatafuta utaratibu mwingine.”
Amesema tayari
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu ameshatoa taarifa kwa umma kuhusu ugonjwa huo na aliwahakikishia
Watanzania kuwa homa hiyo haijaingia nchini.
Waziri Mkuu
amesema: “Katika kukabiliana na homa hiyo, Serikali imejipanga kwa
kuimarisha mawasiliano na ubalozi wetu huko China ili kujua hali
inaendeleaje, na Balozi wa Tanzania nchini China, Balozi Mbelwa Kairuki
anafanya kazi hiyo ya kutoa mrejesho wa kila siku wa hali ilivyo huko.”
Amesema licha ya
kutuma mrejesho, pia Balozi huyo anafanya kazi nzuri ya kutoa elimu kwa
Watanzania kwa kutafuta madaktari wa Kitanzania ambao wamejifunza
ugonjwa huo na kuwaelimisha Watanzania waliopo nchini China namna ya
kujikinga na homa hiyo.
Akizungumzia
baa la nzige lililoikumba nchi jirani ya Kenya, Waziri Mkuu amesema kuwa
tayari Serikali imeshachukua tahadhari ambapo Wizara ya Kilimo ya
Tanzania inashirikiana na ya Kenya kumaliza tatizo hilo. Pia amewataka
wananchi wanaoishi kwenye mikoa, wilaya na vijiji vilivyo mipakani,
watoe taarifa mara watakapowaona wadudu hao.
No comments :
Post a Comment