Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akitoa ufafanuzi wa
swali la nyongeza lililoulizwa bungeni jijini Dodoma leo na Mbunge wa
Kawe Mhe. Halima Mdee kuhusu mikakati ya Serikali kujenga madampo
mengine ili kukidhi mahitaji ya Jiji la Dar es Salaam.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akijibu maswali mbalimbali
yaliyoulizwa na wabunge Daniel Nswanzugwako (Kasuliu Mjini) na Halima
Mdee (Kawe) wakati wa kipindi cha maswali na majibu mapema leo bungeni
jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu na Naibu Waziri
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
wakijadiliana jambo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo mara
baada ya kipindi cha maswali na majibu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu (kushoto)
akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella katika viwanja
vya Bunge jijini Dodoma leo. Katikati ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima.
………………………………………………………………………………………………..
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu amesema Serikali
inatarajia kujenga dampo la kisasa katika Mkoa wa Dar es Salaam ili
liweze kuhimili taka zote zinazozalishwa mkoani humo.
Zungu amesema hayo leo bungeni
jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kawe Mhe. Halima Mdee
aliyeuliza kuwa Serikali ina mkakati gani wa kujenga madampo mengine
katika wilaya zote za mkoa huo kwani hivi sasa kuna dampo moja la Pugu
Kinyamwezi.
Alibainisha kuwa kiasi cha sh.
bilioni 75 zimetolewa na wafadhili kwa ajili ya kazi hiyo ambayo
itakwenda sambamba na ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami katika eneo
la dampo ili kurahisha usafirishaji wa taka ambapo Halmashauri ya Jiji
hilo imetenga fedha.
“Kasi ya taka zinazozalishwa Dar es Salaam ni kubwa na jiji linakua kwa asilimia kubwa sana na kwa miaka miwili ijayo kasi ya population itafika
milioni 8 hadi 9 na dampo ni moja na juzi mimi nimetembelea, dampo hali
ya dampo ni mbaya lazima tukiri ni mbaya miundombinu ni mbaya hatua
zimeshachukuliwa,” alisema Zungu.
Awali akijibu maswali ya msingi ya
Mbunge Mdee kuhusu mkakati gani wa Serikali wa kukabiliana na tatizo la
uchimbaji mchanga na uchafuzi uliokithiri jijini humo, Naibu Waziri
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima alisema
ni kweli uchimbaji huu huleta athari ikiwa ni pamoja na mmomonyoko wa
kingo za mito, uharibifu wa maji na miundombinu na mwingiliano wa maji
ya bahari katika nchi kavu.
Alitaja zingine kuwa ni kubadilika
kwa mkondo wa mto kutoka uelekeo wa asili, kuharibika kwa uimara wa
mto, uharibifu wa mimea ya asili ambayo husaidia kupunguza mmomonyoko na
uharibifu wa mazalia ya viumbe hasa wakati kina cha maji
kinapoongezeka.
Hivyo alibainisha kutokana na
changamoto hizo aliweka wazi kuwa Serikali inaandaa mkakati wa muda
mrefu unaotokana na mapendekeo ya Kamati Maalum ya wadau iliyoundwa na
Ofisi hiyo kupendekeza hatua za kuchukuliwa ili kuwa na uchimbaji
endelevu wa mchanga na usiokiuka Sheria za nchi.
Aliongeza kuwa zitafanyika tafiti
na kuendeleza teknolojia za ujenzi zinazoweza kutumia mchanga kidogo na
kuelimisha wananchi kuhusu athari za uchimbaji holela wa mchanga na
kuzuia uchimbaji holela.
Aidha, Sima alisema kuwa mamlaka
mbalimbali zikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
(NEMC), Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mamlaka za Mabonde na Tume
ya Madini kupitia Ofisi ya Madini Mkoa wa Dar es Salaam, zimekuwa
zikifanya ukaguzi wa mara kwa mara na hatua stahiki kwa mujibu wa sheria
huchukuliwa,
“Kuhusu uchafuzi wa mazingira
uliokithiri, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 Kifungu
139(1) imetoa mamlaka kwa Serikali za Mitaa kuzuia au kupunguza taka
ngumu, taka vimiminika, gesi taka na taka zenye madhara. Serikali
itaendelea kuelimisha wananchi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa
sheria,” alisisitiza Sima.
Aliongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa
Rais kupitia programu ya Elimu kwa Umma inatoa elimu kuhusu usimamizi na
udhibiti wa taka kuanzia ngazi ya jamii, viongozi na wadau, hasa katika
eneo la urejelezaji wa taka ngumu na kutoa wito kwa Serikali za Mitaa
kuwajibika kwa kuweka mipango endelevu ya usimamizi wa taka kama
ilivyobainishwa katika Kifungu 139(1) cha Sheria ya Usimamizi wa
Mazingira ya mwaka 2004.
No comments :
Post a Comment