Mjumbe wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi Mhe. Asina Omar akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwenye
Mkutano wa Wadau wa Uchaguzi uliofanyika Mkoani Mtwara

Bw. Musa Kulangwa kiongozi wa chama cha CUF akichangia hoja kwenye Mkutano wa Wadau wa Uchaguzi
……………..
Mtwara,
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
imewahimiza wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura.
Wakizungumza kwenye mikutano ya
wadau wa Uchaguzi iliyofanyika leo (Ijumaa tarehe 03.01.2020) mkoani
Lindi na Mtwara ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari kwenye
mikoa hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji
Rufaa (Mst.) Mbarouk Salim Mbarouk na Mjumbe wa Tume, Mhe. Asina Omar
wamesema zoezi hilo kwa Lindi na Mtwara litafanyika kwa siku saba (7)
kuanzia tarehe 12 hadi 18 mwenzi huu.
Wadau walioshiriki mikutano hiyo
ni pamoja na Viogozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi
wa Asasi za Kiraia, Wawakilishi wa makundi maalum ya Watu wenye Ulemavu,
Vijana, Wanawake na Wazee.
Wakisoma hotuba za ufunguzi wa
mikutano hiyo, viongozi hao wamesema kwamba “kabla ya kuanza kwa awamu
ya kwanza (ya Uboreshaji wa Daftari), Tume ilifanya maandalizi kadhaa
ikiwa ni pamoja na uhakiki wa Vituo vya kujiandikishia, Uandikishaji wa
majaribio, Maandalizi ya vifaa vya Uboreshaji wa Daftari pamoja na
kuandaa Mkakati wa Elimu ya Mpiga Kura”.
Tangu kuzinduliwa kwa zoezi la
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mnamo tarehe 18 Julai,
2019 mkoani Kilimanjaro, tayari mikoa kumi na nane (18) imekamilisha
zoezi hili. Mikoa hiyo ni pamoja na Kilimanjaro, Arusha, Manyara,
Simiyu, Mara, Mwanza, Kigoma, Tabora, Songwe, Kagera, Geita, Shinyanga,
Katavi, Rukwa, Singida, Dodoma, Mbeya na Iringa. Zoezi hilo hivi sasa
linaendelea katika mikoa ya Ruvuma na Njombe kwa Tanzania Bara na Visiwa
vya Unguja na Pemba kwa upande wa Tanzania Zanzibar.
Akitoa mada kwenye mkutano mkoani
Mtwara, Mkurugenzi waUchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles ametoa wito kwa
Wadau hao kutoa ushirikiano katika kuelimisha, kuhamasisha na
kufuatilia zoezi hili. Aidha, amewataka kufanikisha uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga kura ili wale wote wenye sifa waweze
kuandikishwa au kurekebisha taarifa zao katika Daftari.
No comments :
Post a Comment