Mkurugenzi Mtendaji wa NANHRI,
Gilbert Sebihogo (Kushoto) akikaribishwa na mwenyeji wake Mwenyekiti wa
THBUB Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu (Kulia) katika ofisi za THBUB jijini
Dodoma.
Mwenyekiti wa THBUB Jaji Mstaafu,
Mathew Mwaimu (Katikati) akiongea katika kikao kifupi baina ya THBUB na
Mkurugenzi Mtendaji wa NANHRI, Gilbert Sebihogo (Kushoto). Wengine ni
Makamishna na Maofisa wa Tume.
Mkurugenzi Mtendaji wa NANHRI,
Gilbert Sebihogo (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti
wa THBUB Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu (kushoto kwake) katika ofisi za
THBUB. Wengine ni Makamishna na Maofisa wa Tume.
Mkurugenzi Mtendaji wa NANHRI,
Gilbert Sebihogo (kushoto) akiagana na Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu (wa
pili kushoto) muda mfupi baada ya kikao kilichofanyika katika ofisi za
THBUB, Dodoma. Aliyevaa hijab ni Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Hajjat
Fatuma Muya, (Wa pili kulia) ni Makamu Mwenyekiti, Mohamed Hamad, na
(kulia) ni Kamishna, Fatma Khalfan.
……………………………………………………………………………………………………..
Na Mbaraka Kambona,
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa
taasisi ya Haki za Binadamu Afrika (NANHRI), Gilbert Sebihogo ameishauri
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kushirikiana na
serikali katika kuboresha upatikanaji wa haki kwa wananchi, huku
akiwaasa kujiepusha na vitendo vya kukosoa kila jambo linalofanywa na
Serikali.
Sebihogo alitoa kauli hiyo Januari
30, 2020 katika ofisi za THBUB zilizopo Dodoma alipozitembelea kwa
lengo la kutambuana na Makamishna wa tume na kuimarisha uhusiano wao wa
muda mrefu .
Alimueleza Mwenyekiti wa THBUB,
Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu kuwa tume itafute namna nzuri ya kuishauri
serikali na kujenga ushawishi utakaofanya serikali iendelee kuwawezesha
kutekeleza majukumu yao.
“Tume mnapaswa kuendelea
kuishawishi serikali kufanya nao kazi kama washirika, mfanye kazi bila
misuguano wala kudharau mambo mazuri yanayofanywa na serikali, kwa
kufanya hivyo kutaifanya serikali kushirikiana na nyinyi”, Sebihogo
alisisitiza
“Msiwe wakosoaji wa kila jambo
kama baadhi ya watu au taasisi nyingine zinavyofanya, kuna mambo mengi
mazuri yanayofanywa na serikali, hamna budi kutambua juhudi hizo na pale
mnapoona kuna jambo ambalo alijafanywa vizuri na serikali toeni maoni
yenu kwa busara, alieleza Sebihogo
Aliongeza kuwa sio jambo rahisi
kwa taasisi nyingi za haki za binadamu kufanya kazi kwa kushirikiana na
serikali bila misuguano, lakini inawezekana kwa kutumia njia nzuri za
kuishawishi serikali kujua kuwa taasisi ya haki za binadamu ipo kwa
ajili ya kuisaidia serikali kutimiza wajibu wake na sio vinginevyo.
“Tume ni muhimu kutambulika na
serikali na wananchi, ifanye kazi kwa kuwafikia wananchi wa kawaida hadi
ngazi za chini, ikifanya hivyo watu watashawishika kuja kwenu kupata
huduma na hata zile taasisi zenye majukumu kama yenu zitashawishika
kuja kupata maoni na ushauri”aliongeza
Sebihogo aliendelea kusisitiza
kuwa THBUB ikipoteza uhalali wake kwa wananchi, wengine watapaza sauti
zao, na wataisemea THBUB, kitu ambacho sio sawa, lakini tume ikifanya
kazi zake ipasavyo taasisi zote zenye majukumu sawa na tume zitawaunga
mkono.
Akiongezea hapo, aliieleza THBUB
kuwa kupitia mamlaka iliyopewa inayo nafasi ya kushiriki kuisaidia
serikali kutimiza malengo makubwa iliyojiwekea.
Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu
alimwambia Sebihogo kuwa tangu walipoteuliwa kuwa Makamishna wa THBUB
wamefanya mbalimbali za kujaribu kukutana na viongozi mbalimbali kwa
lengo la kutafuta ushirikiano na mpaka sasa juhudu hizo zinaenda vyema.
“Tutaendelea kutafuta fursa za
kukutana na kukaa pamoja na serikali ili kuwaelewesha waweze kutambua
mamlaka na majukumu ya tume, tunajua kuwa kuna maeneo bado tunahitaji
kuyaboresha ili kushirikiana bega kwa bega na serikali, wadau na jamii
kwa ujumla” Jaji Mwaimu alisema
Makamu Mwenyekiti wa tume, Mohamed
Hamad pia alisisitiza kuwa THBUB inaunga mkono jitihada za serikali
katika kuwapatia haki za msingi wananchi.
“Sisi tume tunaunga mkono jitihada
za serikali, na ni wazi kuwa tume ni taasisi ya umma iliyopewa mamlaka
ya kuisaidia serikali kuhamasisha na kulinda haki za binadamu nchini”,
Hamad alifafanua
Aidha, Hamad aliiomba NANHRI kama
mtandao wa haki za binadamu kuhamasisha wanachama wake kudumisha mila na
desturi za kiafrika na kuachana na baadhi ya haki zinazohamasishwa na
nchi za magharibi na ulaya ambazo zipo kinyume na tamaduni za waafrika.
Mtandao wa taasisi ya Haki za
Binadamu Afrika (NANHRI) ni taasisi muamvuli ya kikanda iliyoanza kazi
mwaka 2007 yenye makazi yake nchini Kenya na ina wanachama 44 kutoka
nchi za afrika ikiwemo Tanzania.
Jukumu la Mtandao huu ni kusaidia
na kuimarisha taasisi za haki za binadamu za Afrika kwa kuziwezesha na
kuhakikisha zinashirikiana zenyewe na taasisi nyingine za kimataifa.
No comments :
Post a Comment