
*****************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema licha ya kuwepo kwa ugatuaji wa madaraka (D by D), Serikali za Mitaa bado zina wajibu wa kuwahudumia wananchi kwa sababu ziko karibu
nao zaidi kuliko Serikali Kuu.
Ametoa kauli
hiyo leo (Alhamisi, Januari 30, 2020) bungeni jijini Dodoma wakati
akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum, Bi. Ruth Mollel, kwenye kipindi
cha maswali kwa Waziri Mkuu bungeni. Mbunge huyo alisema dhana ya
ugatuaji wa madaraka inakinzana na hali halisi kwani utekelezaji wake
haujaenda sawasawa kwa vile Serikali inakusanya fedha kutoka kwenye
vyanzo vya mapato vya Halmashauri kama vile kodi ya majengo na mabango.
“Wajibu wa
kumhudumia mwananchi ni wa Serikali za Mitaa kwa sababu iko karibu nao
zaidi. Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kuwa tunashirikiana na
Serikali za Mitaa kumhudumia mwananchi lakini hatujaondoa wajibu wa
Serikali za Mitaa kuwahudumia wananchi,” amesisitiza.
Amesema
Serikali Kuu bado inalo jukumu la kusimamia mapato na imeamua kudhibiti
ukusanyaji wa mapato na imekuwa ikihakikisha mapato haya yarudi tena kwa
wananchi. “Tunaporudisha kwa wananchi, tunawapelekea hao hao Serikali
ya Mitaa kwa mahitaji yao ili watekeleze hilo jambo, hatujawaondolea
mamlaka ya kusema tunahitaji darasa, tunahitaji kituo cha afya,
tunahitaji uboreshaji wa miundombinu.”
“Tumeongeza hata taasisi kwa kuunda TARURA ili
isimamie miundombinu; sasa hivi tunaenda kwenye maji, kutakuwa na
taasisi ya kusimamia utoaji wa maji. Pale ambapo kuna mahitaji, Mamlaka
ya Serikali za Mitaa iseme inahitaji shilingi ngapi, kwa ajili ya nini,
nasi tunawapelekea, ndiyo kwa sababu leo tunaona huduma zinatekelezwa
mpaka vijijini. Hii ni kwa sababu tunashirikiana na Serikali za Mitaa
katika kuratibu.”
“Ule udhaifu
wa usimamizi wa makusanyo, na udhaifu wa usimamizi wa matumizi ambao
ulikuwa umejitokeza sasa tunaendelea kuutibu na ndiyo kwa sababu unaona
wakati wote tunapokwenda huko kwenye ziara, kwanza tunauliza ukusanyaji
na kama makusanyo yoyote yamehifadhiwa na matumizi yake yako sawa, na
pale ambapo matumizi yanakuwa si sahihi tunachukua hatua,” amesema.
Amesema
kutokana na muundo uliopo, zipo Serikali za Mitaa ambazo zina majukumu
yake yaliyoainishwa rasmi na kuna Serikali Kuu ambayo pia inawajibika
kuzihudumia Serikali za Mitaa.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amesema haitaleta maana endapo Serikali
italazimika kutengua matokeo ya uchaguzi wote wa Serikali za Mitaa
wakati wagombea ambao hawakuridhishwa na matokeo hayo walikuwa na fursa
ya kukata rufaa.
“Chaguzi zote
nchini zinatawaliwa na kanuni na sheria zake. Kila mmoja aliyeshiriki
kama aliona kuna ukiukwaji wowote, alikuwa na fursa ya kukata rufaa na
kama hajaridhika, alikuwa na fursa ya kwenda mahakamani,” alisema.
Alisema
chaguzi zote zina sheria zake na kanuni zake na hata wakati wa kuandaa
kanuni za Serikali za Mitaa, vyama vyote vya siasa vilishirikishwa
katika kutengeneza kanuni zao na moja kati ya kanuni hizo ni pale ambapo
inatoa fursa kwa yeyote ambaye hajaridhika huko anakogombea, anaweza
kukata rufaa na atakapoona rufaa hiyo kwenye ngazi inayofuata haikutenda
haki, aende mahakamani.
“Kwa hiyo
kulichukua hili kwa ujumla ujumla, inaweza isiwe sahihi sana kwa sababu
kila mmoja kule alipo, alikuwa na mamlaka yake inayoratibu na anayo
fursa ya kwenda kwenye mamlaka kukatia rufaa pale ambapo hajaridhika na
utekelezaji wa jambo hilo. Na vyama vyote vilishiriki kwenye hii kanuni
ya kukata rufaa, kwa hiyo ni wajibu wa huyo mgombea kwenye eneo hilo
kwenda kukata rufaa,” alisema.
Alikuwa
akijibu swali la mbunge wa Mbozi, Bw. Pascal Haonga, aliyetaka kujua
kama Serikali iko tayari kurudia uchaguzi wa Serikali za Mitaa wakati wa
uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu kwa sababu ule uliopita uligubikwa
na dosari nyingi.
“Mchakato wa
uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, uligubikwa na dosari nyingi
sana zikiwemo za wagombea kutoka vyama vya upinzani kunyimwa fomu, ofisi
kufungwa kwa muda wote, hivyo kupelekea baadhi ya wagombea hasa wa
upinzani kushindwa kupata fursa za kugombea. Serikali haioni kwamba ni
vema uchaguzi wa Serikali za Mitaa uweze kurudiwa sambamba na uchaguzi
mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu?” alihoji.
No comments :
Post a Comment