
**************************
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
TAKUKURU Mkoani
Pwani, imetoa rai kwa viongozi wa kuchaguliwa wakiwemo madiwani na
wabunge kurudi kwa wananchi na kwenda kujitathmini kuwaeleza juu ya
utekelezaji wa ahadi na mambo waliowafanyia katika kipindi cha uongozi
wao ili wachaguliwe kwa haki badala ya kujiingiza kwenye dimbwi la
utoaji rushwa wakati wa uchaguzi mkuu.
Aidha imewataka
madiwani kufuatilia na kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao
na endapo watabaini shaka yoyote watoe taarifa TAKUKURU kwa msaada
zaidi.
Akitoa tahadhali za
kiuchaguzi wakati wa kikao cha baraza la madiwani ,Kibaha Mjini,
mwakilishi kutoka TAKUKURU Pwani, Juma Swalehe alisema ,kila kiongozi wa
kuchaguliwa atavuna kwa alichokipanda ndani ya miaka mitano ya uongozi
wake.
Alieleza kwamba,
ifikie hatua ya kubadili mtizamo wa kushinda uongozi kwa fedha ama kutoa
rushwa ya vitu bali wajipime kwa yale waliyoyaahidi kwa wananchi na
kueleza walichotekeleza na nini serikali imefanyia wananchi wake.
“Elimu tumeshatoa
mara kwa mara ,kuanzia sasa nendeni kwa wananchi wenu mkajieleze
mlichowafanyia,:wawapime mapema kabla ya uchaguzi ili kama mnaweka nia
tena iwe rahisi kwenu wakati wa kampeni na uchaguzi”alifafanua Swalehe.
Pamoja na hilo
Swalehe ,alimuelekeza mkurugenzi,mwenyekiti wa halmashauri kuunda kamati
za kudhibiti uadilifu pia mmomonyoko wa maadili kwa watumishi .
Nao baadhi ya
madiwani akiwemo diwani wa viti maalum Selina Wilson ,alielezea, hata
mh.Rais John Magufuli serikali yake inapiga vita masuala ya rushwa na
inahitaji utawala bora hivyo viongozi wa kuchaguliwa wanapaswa kuwa
sehemu ya kuunga mkono juhudi hizo.
Diwani wa kata ya
Tumbi, Hemed Chanyika alifafanua kuwa, ndani ya Chama Cha Mapinduzi
imeshaelekezwa ,kiongozi akiwa na chembe ya rushwa hafai kuongoza jamii
na ni vyema aenguliwe mapema kabla ya uchaguzi.
“Na hao TAKUKURU
wasiwe miongoni mwa watu wanaochukua rushwa kwa siri ili kusaidia kurudi
kwa hao mabebari wanaowasema bali waweke msimamo wa dhati kushirikiana
na serikali kupiga vita rushwa ya uchaguzi”alisisitiza Chanyika.
Kwa upande wake
diwani wa kata ya Mailmoja ,Ramadhani Lutambi aliwataka wananchi nao
wasiwaendekeze viongozi wanaopitapita kuwapa rushwa ili kuwachagua kwani
endapo wakiwa na msimamo hakuna kiongozi atakae warubuni kwa kuwapa
rushwa.
Aliishauri TAKUKURU
kuharakisha kufanyia kazi mashauri yanayopatikana yasikae mezani kwa
kipindi kirefu na washuke ngazi za chini na kata ili kufanya kazi na
jamii.
No comments :
Post a Comment