Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias
Kwandikwa, akizungumza na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa
wa Mtwara Mhandisi Dotto Chacha, wakati alipokagua hatua za ujenzi wa
barabara ya Mtwara-Mnivata yenye urefu wa KM 50, mkoani Mtwara. Kushoto
kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Bw. Evod Mmanda.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias
Kwandikwa, akikagua moja ya gari la kumwaga kokoto katika mradi wa
ujenzi wa barabara ya Mtwara – Mnivata yenye urefu wa KM 50 inayoendelea
kujengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Mtwara.
Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS), mkoa wa Mtwara Mhandisi Dotto Chacha, akitoa maelezo kwa
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, kuhusu hatua zilizofikiwa
katika ujenzi wa barabara ya Mtwara – Mnivata yenye urefu wa KM 50 kwa
kiwango cha lami.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya
Mtwara – Mnivata yenye urefu wa KM 50 inayojengwa kwa kiwango cha lami
mkoani humo. Mradi huo hadi sasa umekamilika kuwekwa lami kilometa 43.
………………
Serikali imemuondolea hofu
mkandarasi wa kampuni ya Dott Services anayejenga barabara ya
Mtwara –
Mnivata yenye urefu wa kilometa 50 kwa kiwango cha lami kuwa
itakamilisha malipo anayoyadai mapema zaidi ili barabara hiyo iweze
kukamilika na kupitika vipindi vyote.
Ameyasema hayo Naibu Waziri wa
Ujenzi, Elias Kwandikwa, wakati alipokuwa akikagua mradi huo unaojengwa
kwa zaidi ya shilingi Bilioni 89 na kumsisitiza mkandarasi huyo
kukamilisha barabara hiyo ndani ya miezi mitatu.
“Mkandarasi endelea na kazi kwa
kuzingatia viwango na ubora na maombi yenu ya madai tumeyapokea na
yatafanyiwa kazi mapema”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Kwandikwa amesema kuwa uamuzi wa
Serikali wa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ni mwendelezo wa
mikakati ya kuboresha miundombinu hapa nchini, kwa ajili ya kukuza
shughuli za kiuchumi na za kijamii na hatimaye kuipeleka nchi katika
uchumi wa kati unaotegemea viwanda.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Mtwara, Bw. Evod Mmanda, amesema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo
kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo mbalimbali hususani
katika ukanda huu wa mikoa ya kusini pamoja na nchi jirani.
Awali akitoa taarifa ya
utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa
wa Mtwara, Mhandisi Dotto Chacha, amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa hadi
sasa mradi umefikia asilimia 75 ambapo kilometa 43 zimekamilika kuwekwa
lami na kazi zilizobaki ni kumalizia kipande kilichobaki na kuweka
alama za barabarani.
Pia Mkurugenzi wa Kampuni ya Dott
Services, Raj Prudhvi, ameahidi kuendelea na kazi zilizobakia na
kukamilisha ndani ya miezi mitatu waliyopewa na Naibu Waziri huyo.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya
Mtwara – Mnivata yenye urefu wa kilometa 50 ni sehemu ya barabara ya
Mtwara – Newala – Masasi yenye jumla ya urefu wa kilometa 210 ambayo ni
muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu na pia uchumi wa wananchi wa maeneo
ya Nanyamba, Tandahimba, Newala hadi Masasi kwa kuwa ni wakulima
wakubwa wa zao la Korosho.
No comments :
Post a Comment