Thursday, January 9, 2020

DKT. MWANJELWA AAGIZA KITENGO CHA MANUNUZI WILAYA YA MKALAMA KICHUNGUZWE KWA TUHUMA ZA UBADHIRIFU


 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama katika kikao kazi, kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo leo. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Mhe. Emmanuel Luhahula na Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Bi. Elizabeth Rwegasira (kushoto).
 Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) katika kikao kazi kilichofanyika katika  ukumbi wa halmashauri hiyo 
 Mbunge wa Jimbo la Mkalama, Mhe. Allan Kiula akiwasilisha hoja za watumishi wa jimbo lake wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kilichofanyika leo katika ukumbu wa halmashauri hiyo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tatazi iliyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Bw.John Cassiano akiwasilisha hoja kuhusu walimu wanaojiendeleza kielimu kutopandishwa vyeo, wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kilichofanyika katika  ukumbi wa halmashauri hiyo  
NA HAPPINESS SHAYO, MKALAMA-SINGIDA
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amemuagiza...
Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mkalama kuchunguza utendaji wa Kitengo cha Manunuzi cha Wilaya hiyo kutokana na utekelezaji mbovu wa miradi ya maendeleo.
Agizo hilo amelitoa leo wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.
“Nataka TAKUKURU mkichunguze Kitengo cha Manunuzi cha Wilaya ya Mkalama kwa sababu nimebaini kuna mwenendo mbaya katika utekelezaji wa miradi hapa wilayani” Dkt. Mwanjelwa amesema.
Amefafanua kuwa Kitengo hicho kimekuwa kikitoa tenda za miradi mbalimbali bila kufuata utaratibu ikijumuisha pia upotevu wa vifaa vya ujenzi katika mazingira ya kutatanisha.
Dkt. Mwanjelwa ameweka bayana kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikijitahidi kuhakikisha inafikisha huduma karibu na wananchi akitolea mfano ujenzi wa hospitali, upanuzi wa vituo vya afya na ujenzi wa masoko, lakini wako baadhi ya watumishi wanaofanya ubadhirifu.
“Natoa onyo kwa watumishi ambao bado wanafikiria kujipatia fedha kupitia miradi hii na ninawapa pole kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli haitaki mzaha katika utendaji kazi ”Dkt. Mwanjelwa ameongeza.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inataka watumishi walio safi kiutendaji, wanaowajibika ipasavyo na wanaofanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za kiutumishi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwanjelwa amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kutekeleza agizo la serikali la kuwaondoa kazini watumishi wenye vyeti vya kughushi.
Maelekezo hayo ameyatoa baada ya kupokea malalamiko ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Malela, Bw. Alfred Panda aliyetaka kujua hatima ya mmoja wa walimu wake aliyebainika kuwa na cheti cha kughushi wakati wa zoezi la kusafisha taarifa za watumishi, lakini amekuwa akiendelea na kazi na amefuatilia barua yake ya kusimamishwa kazi bila mafanikio.
Dkt. Mwanjelwa amemtaka Mkurugenzi  wa Halmashuri ya Wilaya ya Mkalama kulifanyia kazi suala la mtumishi huyo haraka iwezekanavyo.
“Mkurugenzi hakikisha hatua kali za kisheria zinachukuliwa haraka kwa mtumishi huyu ambaye ana vyeti feki na unipe mrejesho” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Mhe.Dkt. Mwanjelwa yupo Mkoani Singida katika ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF pamoja na kukutana na Watumishi, kusikiliza maoni kero zao na kuzitatua

No comments :

Post a Comment