Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akimsikiliza kwa makini Mkuu wa Global
Fund- Afrika Bw. Linden Morrison hayupo pichani wakati wa kikao kati ya
Waziri wa Fedha na Mipango na uongozi wa Global Fund kilichofanyika
Jijini Dodoma. Kushoto ni Kaimu Kamishina wa Idara ya Fedha za nje,
Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Sauda Msemo.
Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt.Philip Isdor Mpango (Mb) akiwa katika picha ya
pamoja na Viongozi wa Taasisi ya Global Fund -Afrika na Viongozi na
Maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango, baada ya kikao kati ya Waziri wa
Fedha na Taasisi ya Global Fun, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt.Philip Isdor Mpango (Mb), akisalimiana na Mkuu wa
Global Fund Barani Afrika Bw. Linden Morrison, walipokutana na kufanya
mazungumzo Jijini Dodoma ambapo pande hizo mbili zimeahidi kuendelea
kushirikiana ambapo Global Fund imeahidi kuipatia Tanzania dola milioni
600 mapema Januari mwaka 2021.
Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolf Ndunguru, akifuatilia jambo
katika kikao kati ya Waziri wa Fedha na Mipango na Uongozi wa Global
Fund Afrika. Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na
Mipango Jijini Dodoma. Kushoto ni Kaimu Kamishina wa Sera -Wizara ya
Fedha na Mipango, Bw. William Mhoja.
Mtalaamu wa Fedha
Mwandamizi kutoka Taasisi ya Global Fund -Afrika Bi. Shevone Corbin
akifafanua jambo katika kikao na Waziri wa Fedha na Mipango uliofanyika
katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma. Kulia kwake
Mkuu wa Taasisi ya Global Fund -Afrika Bw. Linden Morrison.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)
*******************************
Na Ramadhani Kisimba, WFM-Dodoma
Serikali ya
Tanzania itanufaika na msaada wa dola za Marekani milioni 600
zitakazotolewa na
Taasisi ya Global Fund mwezi Januari mwakani kwa ajili
ya kusaidia kukabiliana na maradhi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria
katika kipindi cha miaka mitatu.
Ahadi hiyo
imetolewa Jijini Dodoma na Mkuu wa Mfuko huo Barani Afrika Bw. Linden
Morrison, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na
Mipango Jijini Dodoma.
Amesema kuwa
fedha hizo sawa na takriban shilingi za Tanzania trilioni 1.4 zitatumika
kuimarisha afya kwa kupambana na magonjwa ya Ukimwi, Kikufua Kikuu na
Malaria ambapo vifaa tiba na vitendanishi mbalimbali vitanunuliwa
kupitia msaada huo katika kipindi cha miaka mitatu (2021-2023).
Ameeleza kuwa
katika kipindi cha miaka 15 ambacho taasisi yake imekuwa na uhusiano
mzuri na Tanzania, Mfuko wake tayari umetoa msaada wa dola za Marekani
bilioni 2 kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya hususan katika mapambano
dhidi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.
Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru Taasisi hiyo ya
Kimataifa ya Global Fund kwa mchango mkubwa iliyoipatia Tanzania katika
mapambano dhidi ya magonjwa hayo hasa malaria, ugonjwa unaoongoza
kusababisha vifo vya watanzania wengi.
Dkt. Mpango
aliahidi kwamba fedha hizo zitatumika kikamilifu na kama ilivyokusudiwa
ili zilete matokeo chanya kwa kuwafikia walengwa nchini kote.
‘‘Nimefurahi
kwa sababu nina matumaini kuwa tumepata nguvu ya kupambana na magonjwa
haya makubwa, ili Watanzania wawe na afya njema na waweze kujenga uchumi
wa nchi yao’’ Alisema Mhe. Mpango.
Aidha Dkt.
Mpango alisema katika kikao hicho wamejadili namna ya kuboresha zaidi
ushirikiano uliopo kati ya pande hizo mbili ikiwemo kuangalia namna ya
kutoa msamaha wa kodi kwenye vifaa yakiwemo magari ya kubebea wagonjwa
na dawa zinazoingizwa nchini na Taasisi hiyo kwa ajili ya mradi huo.
“Aidha, Ili
kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Taasisi ya Global Fund, nchi
itahakikisha inakuwa na ushiriki mpana katika Bodi ya Wakurugenzi ya
Mfuko huo ili sauti ya nchi iweze kusikika zaidi” aliongeza Dkt. Mpango
Kuhusu
ubadhirifu wa zaidi ya dola za Marekani 400,000 zinazodaiwa kufujwa na
baadhi ya Watendaji wa Serikali wanaotekeleza mradi huo hapa nchini,
Dkt. Mpango ameuahidi Mfuko huo kwamba Serikali itachunguza na
kuwachukulia hatua kali watu wote waliohusika na vitendo hivyo.
No comments :
Post a Comment