*******************************
Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amemuomba Mwanasheria Mkuu
wa Serikali Dkt. Adelardus Kilangi kulitazama suala Mbunge Zitto Kabwe
kutumia nembo ya Bunge katika barua inayotaka Benki ya Dunia kusitisha
mkopo wa
nafuu wa elimu dola milioni 500 wenye lengo la kuboresha
elimu nchini.
Akizungumza leo
Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu, Spika wa
Bunge, Job Ndugai alisema kuwa hatua ya Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto
Kabwe, kuandika barua Benki ya Dunia kwa kutumia nembo ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuitaka benki hiyo isitishe mkopo huo
kwa muda ni kutumia vibaya nembo ya Bunge, na kuwa huo si msimamo wa
Bunge.
“Katika jambo
hili kuna dalili za ujinai, kwa hiyo tunakuomba Mwanasheria Mkuu wa
Serikali uchunguze na mkiona kuna ujinai muweze kuchukua hatua, sisi
kama wabunge hatujafurahishwa na jambo hili” alisema Spika Ndugai
Spika Ndugai
alifafanua kuwa ikiwa Mbunge ana tofauti za kisera ni vyema kurekebisha
kwa muktadha huo kuliko kusababisha nchi nzima kukosa fursa kwa sababu
tu ya kutokubaliana na jambo fulani.
Kwa upande wake,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi alisema kuwa ofisi
yake imepokea maelekezo hayo na itayafanyia kazi kwa mujibu wa sheria
zilizopo.
Januari 28 mwaka
huu, katika hafla ya kuapisha viongozi mbalimbali iliyofanyika Ikuku
jijini Dares salaam, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, alisema kuwa Makamu
wa Rais wa Benki ya Dunia alikuja nchini Tanzania mwaka 2019 kwa ajili
ya mazungumzo na hivyo wanapotoa hizo fedha wanajua msimamo wa nchi na
kuwataka viongozi kutojibishana na baadhi ya watu wanaopotosha kuhusu
suala hilo.
No comments :
Post a Comment