
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga,
akizungumza na Mameneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kutoka
mikoa mbalimbali nchini katika kikao kilichowakutanisha mameneja hao
kujadili tathmini ya utendaji kazi wa Wakala huo, jijini Dodoma.
Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Daudi Kondoro.


Mameneja wa Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA), kutoka mikoa mbalimbali nchini wakimsikiliza Katibu Mkuu
wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch.
Elius Mwakalinga, katika kikao kilichowakutanisha mameneja hao kujadili
tathmini ya utendaji kazi wa Wakala huo, jijini Dodoma.


Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo
(TBA), mkoa wa Rukwa, Arch. David Luoga na Kaimu Meneja wa TBA mkoa wa
Singida, Mhandisi Rebecca Kimambo, wakitoa maoni yao kwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius
Mwakalinga, katika kikao kilichowakutanisha mameneja hao kujadili
tathmini ya utendaji kazi wa Wakala huo, jijini Dodoma.
………………………………………………………………………………..
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga,
ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kujitathmini na kubadilika
katika utekelezaji wa miradi yake ili kuondosha taswira mbaya
iliyojengeka katika jamii dhidi yao.
Akizungumza katika kikao cha
kujadili tathmini ya utendaji kazi wa Wakala huo kilichofanyika jijini
Dodoma, Katibu Mkuu huyo amesema kuwa zoezi hilo la kujitathmini
litasaidia kubaini kasoro walizonazo za utoaji huduma kwa wateja wao na
kuzitafutia ufumbuzi na hivyo kusaidia kujenga tena taswira nzuri ya
Wakala huo.
“Nataka mtumie kikao hiki
kuangalia na kujadili changamoto zinazowapelekea msifanye vizuri kwa
sasa na mzipatie ufumbuzi, nadhani mnayaona na kuyasikia yanayosemwa na
wateja wenu, malalamiko ni mengi na kiukweli hayaridhishi”, amesema
Katibu Mkuu Mwakalinga.
Aidha, Mwakalinga amefafanua kuwa,
Wakala huo umekuwa ukilalamikiwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo la
uandaaji wa makisio ya gharama za ujenzi (BOQ), usanifu wa michoro na
kutokumaliza miradi kwa wakati ambapo amesisitiza Wakala huo kuyaangalia
kwa makini maeneo hayo ili kumaliza sintofahamu kwa wateja wao.
“TBA mnaaminika kwa suala la ubora
na weledi, ila kuna baadhi ya maeneo ambayo hamfanyi vizuri, naomba
kuanzia sasa mbadilike ili wateja wenu waendelee kuwaamini”, amesisitiza
Mwakalinga.
Mwakalinga amewataka TBA
kushirikiana na kutojihusisha na majungu kwani hayana tija katika kuleta
maendeleo ya Wakala huo na Taifa kwa ujumla.
Katibu Mkuu Mwakalinga, ameongeza
kuwa hawatawavumilia wale wanaodaiwa kodi na Wakala huo kwani miradi
mingi inashindwa kutekelezwa kutokana na madeni ambayo Wakala wanadai
kwa wateja wao.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Daudi Kondoro, amemhakikishia Katibu
Mkuu huyo kutekeleza maelekezo aliyowapa na kutatua changamoto
walizonazo.
“Naomba nikuhakikishie Katibu Mkuu
kuwa mbali na kuwepo kwa changamoto ya mtiririko wa fedha kutoka kwa
washtiri, wakala utajitahidi kufuatilia madeni na kuhakikisha tunalipwa
kwa wakati ili kusaidia kutekeleza miradi mingine”, amesema Kondoro.
Ameahidi kuzifanyia kazi
changamoto za ndani walizonazo kama vile upungufu wa watumishi na suala
la uandaaji wa makisio ya gharama za ujenzi ambapo amesema kuwa
atawasilisha ripoti ya majibu ya changamoto hizo kwake mara baada ya
kikao hicho kumalizika.
No comments :
Post a Comment