Mshauri mwelekezi wa Shamba la
Utunge Bw. Uwesu Msumi akimuonesha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki eneo la shamba hilo lenye ukubwa wa
hekari 300 wanalotumia kulima mpunga, vitunguu na mahindi pamoja na
ufugaji wa samaki lililopo Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani
alipolitembelea kukagua eneo hilo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki pamoja na timu aliyoongozana nayo
katika ziara yake wakiangalia namna ya ufugaji wa samaki wa kisasa
katika shamba la samaki la Utunge lililopo Rufiji mkoa wa Pwani,
anayetoa maelezo ni Meneja wa samaki wa shamba hilo Bw. Abdallah
Mtutuma.
Mshauri mwelekezi wa Shamba la
Utunge Bw. Uwesu Msumi akitoa maelezo ya uwekezaji wake kwa Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki
alipotembelea shamba hilo lililopo katika Wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani
mara baada ya kuwasili shambani hapo.
Mshauri mwelekezi wa Shamba la
Utunge Bw. Uwesu Msumi akiwasilisha taarifa ya shamba hilo kwa Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki
alipotembelea katika Wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani kukagua mazingira ya
wawekezaji nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki pamoja na timu yake wakiwa katika
shamba la Utunge lililopo katika eneo la Rufiji mkoa wa Pwani, wakati
wa ziara yake.
Muonekano wa moja ya bwawa la kufugia samaki kati ya mabwawa 30 yaliyopo katika shamba la Utunge Wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mhe. Juma
Njwayo akiwasilisha taarifa ya wilaya yake kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipotembelea katika
Shamba la Utunge lililopo kijiji cha Utunge Wilayani humo ili kukagua
maeneo ya uwekezaji na kusikiliza changamoto zao.

Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (Mwenye t-shirt
ya pink) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa shamba la Utunge
pamoja na timu aliyoambatana nayo katika ziara yake, mara baada ya
kutembelea maeneo ya uwekezaji huo.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
…………………………………………………………………………………………………………..
MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini Mhe.
Angellah Kairuki amewahakikishia wafanyabiashara na Wawekezaji kuwa
Serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya Uwekezaji nchini.
Pia, Amesema
Serikali imejipanga kuboresha mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na
wawekezaji ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa kuwekeza
katika sekta mbalimbali zenye tija katika kuliingizia pato taifa.
Ameyasema hayo
hivi karibu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kuhitimisha ziara yake ya siku 6 katika Wilaya 6 za mkoa wa Pwani
ikiwemo; Bagamoyo, Kibaha, Kisarawe, Mkuranga, Mafia na Rufiji pamoja na
Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze.
Akieleza lengo la
ziara hiyo Mhe.Kairuki amesema mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa
yenye uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali; Uvuvi, kilimo na ufugaji
na amefanya ziara hiyo ili kujionea mazingira pamoja na kusikiliza
changamoto zinazowakabili Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akitoa majumuisho
ya ziara hiyo Mhe. Kairuki amezitaja changamoto zilizojitokeza katika
maeneo mengi aliyotembelea kuwa ni ukosefu wa maji ya kutosha, ubovu wa
barabara, ucheleweshwaji wa vibali vya kazi, kukosa umeme wa uhakika na
utitiri wa tozo.
Mbali ya
changamoto hizo, Mhe. Kairuki ametaja vikwazo vingine kuwa ni kutotengwa
kwa maeneo ya uwekezaji, Taasisi wezeshi kutokuwa karibu na wawekezaji,
ukosefu wa mitaji ya uhakika na utoaji wa adhabu zisizo za lazima.
Ameongeza kuwa
uelewa mdogo wa wawekezaji katika kujiunga na Kituo cha Uwekezaji Nchini
(TIC) ni moja ya changamoto na kuwataka wawekezaji kwa hiari yao
waone umuhimu wa kujiandikisha katika kituo hicho ili kutumia fursa
zinazopatikana.
“Wawekezaji
tunawakaribisha TIC ili mjue fursa ziliopo nchini zaidi na kuona namna
mnavyoweza kunufaika na kituo hiki,”alisisitiza Waziri Kairuki.
Ameongoza kuwa,
ipo haja ya kila Halmashauri kuendelea kutenga maeneo ya uwekezaji ili
kutoa fursa zaidi kwa watu kuwekeza na kuhakikisha miundombinu muhimu
inakuwepo.
“Natoa rai kwa
kila Halmashauri kuhakikisha kila kijiji kinatenga walau heka 20 za
maeneo ya uwekezaji na kuwasilisha taarifa zao TIC” alisema Waziri.
Aidha, Waziri
Kairuki amewataka wawekezaji kuzingatia sheria na taratibu za uwekezaji
nchini ili waweze kunufaika na mitaji yao waliyowekeza.
“Endeleeni
kuwekeza pasipo kuvunja sheria na kanuni zilizopo ikiwa ni kulipa kodi
au kulipa vibali mbalimbali mfanye hivyo tena kwa wakati ili isitokee
mmewekeza kwa mitaji mikubwa halafu ikawa kwa hasara,”alisisitiza Waziri
Kairuki
Aliwahakikishia
wawekezaji kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano, inatambua mchango wao na
imedhamiria kuhakikisha inaboresha miundombinu muhimu ikiwemo uwepo wa
nishati ya umeme ya uhakika, barabara bora, upatikanaji wa maji safi,
kuboresha mifumo ya mawasilino na upatikanaji wa huduma bora za mamlaka
zinazosimamia masuala yanayohusu uwekezaji nchini.
AWALI
Waziri Kairuki
alifanya ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Pwani kwa siku 6 na
kuzitembelea Wilaya 6 ambapo jumla ya viwanda 22 alivifikia ikiwemo;
Kiwanda cha KEDS, EUROPLASTIC, Samaki investment, KAMAL LTD, Hiill
Packaging Company, Tan Choice, Global Packaging Ltd, Hester Bioscience
Africa ltd, Chilambo Investment, Sabai Cash nut Processing, SHAFA
Investment, Everwell Cable, Ice Drop ltd, Lodhia Group ltd, Waja Mabati
na Waja General, Abajuko Enterprises, Tanpesca na kiwanda cha maziwa cha
Mather Dairies. Aidha alipata fursa ya kutembelea mashamba ya uwekezaji
mbalimbali pamoja na Shamba la Utunge, Sah janand, shamba la Utamaduni,
Kigomani na shamba la kuku la AKM.
Wawekezaji wa
maeneo hayo walipata fursa za kueleza changamoto wanazokabiliana nazo
pamoja na mapendekezo kwa Serikali ya namna bora ya kuendelea kuwa na
ushirikiano ili kufikia dhamira ya Serikali ya kuwa na Tanzania ya
Viwanda.
No comments :
Post a Comment