Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa walipotembelea katika
daraja lililokata mawasiliano kati ya Mkoa wa Rukwa na Katavi katika
kijiji cha Muze Wilayani Sumbawanga.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo akiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wakizungumza na vijana
waliojitolea kujaza kifusi katika moja ya madaraja yaliyosombwa na
mafuriko katika kijiji cha Lwanji bonde la Ziwa Rukwa, Wilayani
Sumbawanga.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo akitoa hela ya soda kwa vijana waliojitolea kujaza kifusi katika
daraja lililokatika la mto Lwanji katika Kijiji cha Lwanji kwa juhudi
zao za kuwawezesha wananchi wanaotumia daraja hilo kuwezea kuendelea na
shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
………………
Mvua
zinazoendelea kunyesha katika mkoa wa Rukwa zimeendelea kusababisha
maafa baada ya
kusomba madaraja manne katika barabara ya Kasansa –
Kilyamatundu inayounganisha mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi iliyopo
bonde la ziwa Rukwa Wilayani Sumbawanga huku ikisababisha vifo vya watu
watatu katika wilaya ya Kalambo na Nkasi mkoani humo.
Mvua hizo
zilizosomba madaraja katika vijiji vya Muze, Kifinga, Lwanji na Msia
vilivyopo Wilaya ya Sumbawanga imesababisha kukatika kwa mawasiliano
baina ya kata na kata, kijiji na kijiji pamoja na mikoa hali iliyoleta
taharuki kwa wananchi wanaoishi katika bonde hilo lenye kata 13 na
wakulima wengi wa mpunga wanaosafirisha bidhaa zao katika mikoa ya
jirani.
Aidha, Mvua hizo
zimesababisha vifo vya Mama mjamzito na mwanawe kwa kusombwa na maji yam
to Kalambo huko wilayani Kalambo na kifo cha mwanafuzi wa darasa la 4
mwenye umri wa miaka 12 katika Wilaya ya Nkasi ambae pia alisombwa na
maji wakati akitoka shuleni kurudi nyumbani.
Hayo yamesemwa na
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipofanya ziara ya
kutembelea maeneo yaliyokumbwa na maafa hayo na hivyo kuwatahadharisha
wananchi kuacha tabia ya kulazimisha kupita katika njia ya maji pindi
wanapoona mvua ni kubwa na hivyo kuwataka kusubiri mvua ipungue ndipo
waendelee na shughuli zao.
“Mimi niwaombe
ndugu zangu hasa kinamama na watoto, mnapoona mvua zimekuwa nyingi maji
yanaweza yakajaa wakati wowote, jihadharini msipite, acheni maji
yapungue halafu mpite, lakini msiwe wabishi, mkiwa wabishi mtabebwa na
mafuriko, hasa watoto wadogo hawalelewi kitu wanadhani maji kama hivi
anaona kama yametulia anasema mimi nitapita tu, kwahiyo waambieni watoto
nyumbani wachukue tahadhari, mkiona kuna mvua kuna mafuriko watoto
wasiende kwenye shughuli zao muwazuie kuokoa maisha yao” Alisisitiza
Na kuongeza kuwa
hali hiyo si ya kudumu ni ya muda tu kwani serikali kupitia wakala wa
barabara nchini TANROADS inaendelea na matengenezo ya dharura katika
maeneo hayo ili kurudisha hali ya mawasiliano baina ya vijiji, kata
pamoja na mikoa ili wananchi waendelee na shughuli zao za kila na hivyo
kuwataka wakala hao kuweka kambi katika maeneo yaliyoharibiwa na mvua.
“Bonde la ziwa
rukwa limeshakatika kimawasiliano kabisa kwasababu magari yanayotokea
Mbeya, kule Somgwe kupitia daraja letu la Kilyamatundu pale hawawezi
kufika Muze mpaka huko Katavi kama hapa hapatakuwa pameshughulikiwa
kwahiyo weka nguvu kubwa sana Meneja wa TANROADS hapa ili kuhakikisha
wananchi wetu wanapata usafiri wao wa kawaida ndani ya muda
mfupi,”Alisema.
Kwa upande wake
Meneja wa TANROADS mkoa wa Rukwa Mhandisi Masuka Mkina amesema kuwa
tayari wamekwisha omba fedha za matengenezo ya dharura kutoka makao
makuu na kuwataka wananchi kuacha tabia ya kufanya shughuli za
kibinaadamu katika kingo za mito ili kuweza kuokoa miundombinu hiyo
kuharibiwa na mafuriko.
“Nichukue nafasi
hii kuwaomba viongozi wa vijiji na wengine watusaidie kwasababu sheria
ya mazingira inasema wasifanye kazi karibu na mito na panapotukwamisha
ni huko juu ambapo watu wanalima wanaharibu mazingira kwahiyo maji
yanakuja kwa nguvu matokeo yake yanasomba miundombinu yetu na kutuacha
kama hivi tukiwa wakiwa kabisa,” alisema
Kwa upande wao
wananchi katika maeneo hayo waliiomba serikali kuharakisha matengenezo
ya haraka kwani atahri wanayoipata ni kubwa katika upande wa kiuchumi na
kijamii, miongoni mwa wananchi Erasmus Muhagama alisema, “Mi naiomba
serikali iharakishe hili zoezi maana mawasiliano ndio yameshakatika”.
Nae Magdalena
Tangi alisema, “Kwakweli kuna shida watu hawapiti safari zimekuwa ngumu,
usafiri umekuwa wa pikipiki gharama kubwa kwahiyo wananchi tunapata
shida sana kama hivi mlivyoona barabara zimekatika toka Muze mpaka hapa
Msia sijui huko mbele sasa”.
Barabara hiyo
Kasansa – Kilyamatundu yenye urefu wa kilomita 178 iliyopo kwenye bonde
la ziwa Rukwa lenye kata 13 ni kiungo muhimu sana kwa kuunganisha mkoa
wa Rukwa na mikoa ya Songwe na Katavi hasa katika shughuli za kiuchumi
kwani asilimia kubwa ya wakazi wa bonde hilo ni wakulima wa mpunga,
mahindi, alizeti pamoja na kufanya ufugaji.
No comments :
Post a Comment