Happy Lazaro,Arusha.
Naibu waziri wa kazi,
Vijana,Ajira na Ulemavu , Antony Mavunde ameiagiza Mifuko ya hifadhi ya
jamii nchini kuwachukulia hatua kali ya kuwafikisha mahakamani waajiri
wote wasiopeleka michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko hiyo na
kusababisha usumbufu mkubwa kwa wafanyakazi pindi wanapoacha ama
kuachishwa kazi.
Mavunde ametoa kauli
hiyo jijini Arusha wakati alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa hoteli
za Naura springs na Impala za jijini Arusha ambapo wafanyakazi hao
walimweleza changamoto mbalimbali ikiwemo ya suala la michango ya mifuko
ya Hifadhi ya jamii.
Naibu waziri amesema
kuwa kumekuwepo na malalamiko mengi kwa baadhi ya waajiri nchini
kutopeleka michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii
jambo ambalo alionya ni kinyume cha sheria na kuitaka mifuko hiyo
kuwakamata waajiri hao na kuwafikisha mahakamani .
Akiongelea
changamoto za wafanyakazi katika hoteli hizo,Mavunde ameitaka
menejimenti ya hoteli hiyo kuboresha utendaji wake wa kazi na
kuhakikisha wanakuwa kitu kimoja na wafanyakazi wao kwani serikali
inawahitaji wawekezaji wa mahoteli katika kuimarisha sekta ya utalii na
ajira.
Naibu waziri
amempongeza mkurugenzi wa hoteli hiyo,Randy Mrema kwa kukubali kumaliza
changamoto ya malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi wake ndani ya
miezi mitatu kuanzia sasa hadi ifikapo Machi 31 mwaka huu.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa hoteli hizo Randy Mrema alimweleza Naibu waziri kuwa yupo
tayari kumaliza changamoto za wafanyakazi wake na kuahidi pindi ifikapo
Januari 31 mwaka huu atalipa mishahara ya miezi miwili na kwamba ifikapo
Machi 31 mwaka huu atamaliza madai yote ya wafanyakazi hao.
Awali wafanyakazi
hao walimweleza Naibu waziri kuhusu madai ya kutolipwa mishahara ya
miezi sita pamoja na baadhi yao waliopunguzwa kazi hivi karibuni
kutolipwa stahiki zao ikiwemo mishahara ya kuvunja mkataba.
Wamedai kuwa hali
hiyo imewafanya waishi katika mazingira magumu na kushindwa kumudu
maisha ikiwemo kuwasomesha wao ,kodi za pango pamoja na mahitaji mengine
ya kujikimu.
Hata hivyo wameahidi
kuendelea na kazi bila kuwa na kinyongo huku wakisubiri ahadi ya
mwajiri wao ya kuwalipa mishahara katika kipindi cha miezi mitatu
alichoahidi.
No comments :
Post a Comment