Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipasngo, Bw. Doto James (wa pili kulia), akizundua Mfumo wa Malipo ya
Serikali kwa njia ya Kielektroniki (GePG) toleo la simu za mkononi (GePG
App), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James Selikali akiziagiza taasisi zote za Umma
nchini kutojenga mifumo ya fedha ya kieletroniki bila ridhaa ya Wizara
ya Fedha na Mipango na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Mfumo wa Malipo ya Serikali kwa njia ya
Kielektroniki (GePG) toleo la simu za mkononi (GePG App), katika ukumbi
wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Mifumo ya Fedha wa
Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Sausi, akielezea mafanikio ya Mfumo
wa Malipo ya Serikali kwa njia ya Kielektroniki (GePG) ambapo awali
miamala 10 ilikua ikifanyika kwa siku na sasa miamala milioni moja
inafanyika baada ya matumizi ya mfumo huo.
Baadhi ya wajumbe wa Benki nchini,
wafuatilia kwa makini maagizo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipasngo, Bw. Doto James (hayupo pichani), wakati wa hafla ya uzinduzi
wa Mfumo wa Malipo ya Serikali kwa njia ya Kielektroniki (GePG) toleo la
simu za mkononi (GePG App), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Jijini Dodoma.
Mwakilishi wa Benki nchini Bi.
Domina Tarimo, ), akieleza faida ya Mfumo wa GePG katika kuongeza
ufanisi na uwazi katika shughuli za kibenki, wakati wa uzinduzi wa toleo
la simu za mkononi (GePG App), Jijini Dodoma.
Wataalam wa Mfumo wa Malipo ya
Serikali kwa njia ya Kielektroniki (GePG) toleo la simu za mkononi (GePG
App), wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa Mfumo huo Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (katikati), akiwa katika
picha ya pamoja na Wakurugenzi na wataalamu wa mifumo ya fedha na
wengine, baada ya uzinduzi wa Mfumo wa Malipo ya Serikali kwa njia ya
Kielektroniki (GePG) toleo la simu za mkononi (GePG App), katika ukumbi
wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
(Picha na Peter Haule, WFM)
………………..
Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Selikali
imezipiga marufuku taasisi zote za Umma nchini kujenga mifumo ya fedha
ya
kieletroniki bila ridhaa ya Wizara ya Fedha na Mipango na Mamlaka
ya Serikali Mtandao (eGA).
Agizo hilo
limetolewa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango,
Bw. Doto James, wakati akizundua Mfumo wa Malipo ya Serikali kwa njia ya
Kielektroniki (GePG) toleo la simu za mkononi (GePG App), hafla
iliyowakutanisha Wizara ya Fedha na Mipango na Idara, Wakala, Taasisi,
Bodi, Mashirika ya Umma yaliyo katika Kanda ya Kati.
Bw. James
alisema kuwa Taasisi zote za Umma nchini zinatakiwa kutekeleza matakwa
ya Waraka namba tano (5) wa Hazina unaozitaka taasisi zote kuhakikisha
zinapata ridhaa ya Wizara ya Fedha na Mipango na Wakala wa Serikali
Mtandao (eGA) kabla ya kufanya ununuzi, uandaaji, usimikaji na utumiaji
wa Mfumo wowote wa kielektroniki wa usimamizi wa Fedha za Umma.
“Imebainika
kuwa kuna baadhi ya taasisi za umma ambazo zinakiuka maelekezo hayo ya
Serikali kwa sababu wanazozijua wao, nitumie fursa hii kutoa onyo kwa
taasisi hizo kutoendelea na vitendo hivyo kwa sababu ni ukiukwaji wa
maelekezo”, alisema Bw. James.
Akizungumzia
kuhusu GePG App, Bw. James alisema kuwa, uboreshaji wa Mifumo ya
Kielektroniki inayoandaa Ankara itawezesha kukusanya fedha kwa wakati na
kutoa huduma bora kwa Umma.
“Baadhi ya
faida za Matumizi ya Mfumo huo ni kuongezeka kwa uwazi na udhibiti
katika ukusanyaji wa fedha za umma, kupata taarifa sahihi na kwa wakati
zinazohusu makusanyo na kuwa na viwango na utaratibu unaofanana katika
ukusanyaji wa fedha za umma kwa taasisi zote za umma”, alisema Bw.
James.
Alisema faida
nyingine ni pamoja na kuchochea ubunifu katika ukusanyaji wa pesa za
Serikali na sekta ya fedha kwa ujumla kwa kuweka mazingira rafiki na ya
usawa kwa wakusanyaji, kutoa huduma bora na rahisi ya malipo ya fedha za
umma hivyo kuchochea ongezeko la makusanyo na kufika haraka katika
akaunti kuu za makusanyo za taasisi.
“Kwa
kutofanya usuluhishi wa miamala kwa wakati kunaweza kusababisha upotevu
wa fedha nyingi za Umma na pia kuwa na taarifa za fedha zisizo sahihi,
hivyo nawaagiza nyote kuhakikisha mnafanya usuluhishi wa miamala
inayopitia Mfumo wa GePG kwa usahihi na kwa wakati, na kufanyia kazi kwa
wakati changamoto mbalimbali zitokanazo na matokeo ya usuluhishi wa
Miamala husika”, alisisitiza Bw. James.
Aidha alimpongeza
Mkurugenzi wa Mifumo ya Usimamizi wa Fedha wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. John Sausi pamoja na timu yake ya wataalam wabobezi kwa
kutengeneza Mfumo wa Kieletroniki wa Kukusanya Mapato ya Serikali (GePG)
sambamba na toleo la simu za mkononi (GePG App) ambao umerahisisha
ukusanyaji wa mapato ya Serikali pamoja na kuwawezesha wadau kupata
huduma kwa wakati.
Aliahidi kuwa
Wizara yake itaendelea kuiwezesha Idara hiyo ili iweze kutekeleza
majukumu yake ya kubuni mifumo kama hiyo kwa faida ya Serikali na
wananchi kwa ujumla.
Aidha, Bw.
James ambaye pia ndiye Mlipaji Mkuu wa Serikali, alisema kuwa Wizara
kupitia Idara ya Mifumo ya Usimamizi wa Fedha inaandaa mfumo mwingine
utakaotumika kwa ajili ya matumizi ya Serikali ujulikanao kwa kifupi
kama MUCE.
“Mfumo huu
umeshaanza kufanyiwa majaribio kwenye taasisi chache za umma na baadae
utasambazwa kwenye taasisi zote na kwamba Mfumo huu utakuwa mwarobaini
wa matumizi yasiyo sahihi ya fedha za Umma”, aliongeza Bw. James.
Alisema Mfumo
huo utakuwa suluhisho la matumizi yasiyofaa ya umma na kuongeza kuwa
watendaji wengi Serikalini hawataufurahia mfumo huo lakini hilo
haliihusu Serikali. Watajua wenyewe! Alisema huku washiriki wakiangua
kicheko ukumbini.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa Mifumo ya Fedha, wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.
John Sausi, alisema kuwa kabla ya kuwa na Mfumo wa Malipo kwa njia ya
Kielektroniki (GePG) ilikua inafanyika miamala 10 kwa siku na baada ya
mfumo huo inafanyika miamala milioni moja kwa siku.
Alisema kuwa
miongoni mwa mafanikio ni kuongezeka kwa Taasisi zinazotumia Mfumo wa
GePG, kutoka taasisi 300 muda mfupi uliopita hadi kufikia taasisi 620
hivi sasa.
Bw. Sausi
alisema kuwa Mfumo wa GePG kwa njia ya mtandao wa simu za mkononi
uliozinduliwa utasaidia watumiaji kupata huduma mbalimbali kama vile
kununua umeme, kulipia Ankara mbalimbali zikiwemo za makosa ya usalama
barabarani, maji na nyingine nyingi ndani ya sekunde 30.
Ametoa wito
kwa wananchi wanaotumia simu janja (android au IPA App) kupakua
application hiyo kupitia play store au App Store na kutafuta neno GePG
Tanzania tayari kwa matumizi yao ambayo amesema wananchi watafurahia
huduma hiyo.
Naye
Mwakilishi wa Benki katika Mkutano huo, Bi Domina Tarimo na Mwakilishi
wa kampuni za Simu, Bw. Alafat Ibrahim, walisema kuwa Mfumo wa GePG
umezisaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha kazi zao, na kuboresha huduma
kwa wateja wao na wameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango na Serikali
kwa ujumla kwa jitihada zake za kuhakikisha kuna mifumo imara ya fedha
inayoongeza uwazi na uwajibikaji.
No comments :
Post a Comment