
Wataalam wa Kitengo cha Kudhibiti
Magonjwa ya Kuambukiza wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius
Nyerere (JNIA), leo wakijiandaa kabla ya kutua kwa ndege zinazofanya
safari zake kutoka nchi mbalimbali kwenye Jengo la Tatu la abiria (TB3).

Moja ya eneo la ukaguzi wa afya
kwa abiria wanaowasili kupitia Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNIA), wakitokea nchi mbalimbali.

Wataalam wa Kitengo cha Kudhibiti
Magonjwa ya Kuambukiza wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius
Nyerere (JNIA), leo wakijiandaa kabla ya kutua kwa ndege zinazofanya
safari zake kutoka nchi mbalimbali kwenye Jengo la Tatu la abiria (TB3).

Abiria waliowasili kwa ndege ya
Qatar wakikaguliwa kwa mashine maalum za kupima joto la mwili, ili
kubaini walioingia nchini na virusi vya Homa ya Corona iliyoanzia nchini
China hivi karibuni, na kuua watu kadhaa.

Afisa Afya Mkuu Mazingira, Onesmo
Kitange (mwenye mashine ya mkono), leo akimpima Maitrick Dave, raia wa
India, aliyewasili kwa ndege ya Kenya Airways alipowasili leo kwenye
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
……………………………………………………………………………………………………..
Na Bahati Mollel, TAA
KITENGO cha Kudhibiti Magonjwa ya
Kuambukiza, kilichopo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNIA), kimejipanga kukabiliana na wagonjwa
watakaobainika kuwa na virusi vya homa ya Corona, vilivyoanzia nchini
China.
Daktari George Ndaki, ambaye
ni Mdhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza wa JNIA, leo amesema Wizara ya
Afya imekabiliana na ugonjwa huo na tayari imefunga mashine tano
zinazotumia komputa zinazopima joto la mwili la abiria bila kujitambua,
na mashine sita za mkononi, ambazo abiria anapimwa endapo ataonekana
kuwa na joto kali zaidi.
Amesema mashine moja imefungwa
kwenye Jengo la Watu Mashuhuri (VIP) , nyingine imefungwa Jengo la Pili
la abiria na tatu zipo jengo la Tatu la abiria; wakati za mkono
zimeganywa kwenye majengo hayo.
Dkt Ndaki amesema wataalam wa
afya wanaokuwa kwenye mashine zinazotumia komputa wanamtambua abiria
mwenye jotokali mara anapopita mbele ya kamera, na endapo litabainika ni
zaidi ya nyuzijoto 37.4 anahakikiwa zaidi kwa kutumia mashine ya mkono,
huku akihojiwa zaidi juu ya afya yake na nchi aliyotoka, ili kubaini
endapo anavirusi hivyo.
“Hadi sasa hakuna abiria
aliyebainika kuwa na ugonjwa huu, lakini tunaendelea kwani hapa Kiwanja
cha ndege ni moja ya njia kuu au lango Kuu la abiria hususan wa nje ya
nchi wanapotumia kuingia nchini, na ndio maana tunawakagua na
tunashukuru Serikali yetu kupitia Wizara ya Afya kwa kuwa na mashine
hizi mbili, ambazo zinafanyakazi mara mbili na kwa uhakika zaidi ili
kubaini abiria mwenye virusi, ambaye atapelekwa eneo maalum kwa ajili ya
uchunguzi zaidi,” amesema Dkt Ndaki.
Dkt Ndaki amesema pamoja na
kukaguliwa kwa abiria wote wanaowasili kutoka nje ya nchi, pia wanaweka
mkazo zaidi kwa abiria wanaotoka nchi zilizoathiriwa na ugonjwa huom,
ambapo abiria wake mbali na kupimwa joto la mwili, pia wanaandikwa
majina yao na maeneo wanayokwenda baada ya kutoka JNIA.
“Ukiangalia kuna ndege ambazo
zinakuja na abiria waliotoka China baada ya kuunganisha ndege kama Kenya
Airways, Qatar, South Africa, Fly Emirates na na Shirika la ndege la
Tanzania (ATCL), zinakuwa aidha zimebeba abiria waliounganisha ndege
kutoka nchi zilizoshambuliwa na homa ya Corona”. Amesema Dkt Ndaki.
Hata hivyo, amesema siku zote
wamekuwa wakijiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana magonjwa mbalimbali
ya mlipuko na kuambukiza, ili yasiweze kuingia nchini kupitia mipaka
mbalimbali, pamoja na viwanja vya ndege.
Mbali na China nchi nyingine
zilizoathirika na homa hii ni pamoja na Thailand, Australia, Marekani,
Singapore, Malaysia, Japan, Korea Kusini, Ufaransa, Canada, Vietnam,
Ujerumani, Nepal, Sri-lanka na Cambodia. Hata hivyo, kasi ya maambukizi
ya virusi vya Corona sasa ni tishio hadi Barani Ulaya.
Corona ni kundi kubwa la aina
ya virusi, ambavyo huweza kumuathiri binadamu na wanyama, ukubwa wa
maambukizi unahusisha homa za kawaida pamoja na homa kali na wakati
mwingine matatizo katika mfumo wa upumuaji.
Dalili za kuathiriwa na virusi
vya Corona ni pamoja na kukohoa, homa kali, nimonia, kupumua kwa tabu,
kutapika na kuharisha; na hali ikiwa mbaya dalili hizi hujidhihirisha
matatizo kwenye mapafu na figo kushindwa kufanya kazi.
Namna mtu anavyoambukizwa homa
hii ni pamoja na kugusana moja kwa moja bila kinga na muathirika;
kushika kwa mkono vifaa vya muathirika na baadaye kushika mdomoni au
puani, ambapo virusi husambaa kwa kasi.
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, hivi
karibuni amesema hakuna Mtanzania yeyote anayeishi nchini China,
aliyekumbwa na maambukizi ya virusi vya homa ya Corona, vilivyozuka
katika Mataifa ya Marekani, China, Thailand, Korea Kusini na Japan.
Waziri Kabudi ameyasema hayo
wakati akitoa ufafanuzi juu ya hali ya Watanzania waishio nchini China
na kusema kuwa Tanzania ina wanafunzi takribani 4000, ambapo katika mji
wa Wuhan kuna wanafunzi 400 na kwamba kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania
Nchini China, Balozi Mbelwa Kairuki, ameihakikishia Serikali kuwa mpaka
sasa hakuna mtanzania yeyote aliyeathiriwa ama kukumbwa na maradhi hayo.
Ameongeza kuwa Tanzania inaendelea
kufuatilia kwa ukaribu kujua maendeleo na hali za Watanzania wanaoishi
jimboni Wuhan na China kwa ujumla na kuwataka Watanzania kuwa makini na
suala la kutoa taarifa zisizo rasmi ama uvumi, kwani kwa kufanya hivyo
ni kinyume cha sheria za Tanzania na kuwataka kuwa na subira ili kupata
taarifa rasmi kutoka serikalini.
Kutokana na maradhi haya kuwa
mapya hadi sasa hakuna chanjo ya homa hii , na badala yake wagonjwa
wamekuwa wakipewa dawa za kutuliza maumivu pekee.
MWISHO
No comments :
Post a Comment