
………………………………………………………………..
Serikali imewatoa hofu wakulima
nchini kuwa hakuna taarifa za uthibitisho wa uwepo wadudu hatari aina ya
Nzige wa Jangwani walioripotiwa katika nchi za jirani.
Waziri wa Kilimo Japhet
Hasunga ametoa kauli hiyo jana (29.01.2020) wakati alipozungumza
na
waandishi wa habari ofisini kwake Dodoma na kusema Serikali inaendelea
kuchukua hatua madhubuti za kufuatiliaji viashiria vya uwepo wa Nzige wa
Jangwani (Locust Desert).
“Hadi sasa hakuna uthibitisho wa kitaalam kuhusu uwepo wa Nzige wa Jangwani nchini Tanzania” alisisitiza Waziri Hasunga
Alibainisha wazi kuwa Serikali
imejipanga kuwadhibiti nzige hao endapo wataingia nchini na tayari ina
lita 7,000 za viuatilifu kwa ajili ya tahadhari ya kukabiliana na tishio
hilo na ununuzi wa viuatilifu vingine zaidi unaendelea kufanyika.
Alisema Wizara yake inaendelea
kuchukua tahadhali kuhakikisha visumbufu vya mazao ya kilimo kama Nzige
Wekundu, Ndege waharibifu wa nafaka aina ya Kwelea kwelea, panya na
Kiwavijeshi Vamizi zinaripotiwa na kudhibitiwa kwa haraka.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo
tishio la Nzige wa Jangwani limeripotiwa katika nchi za Eritrea,
Ethiopia, Somalia, Sudan na Kenya hivyo kuwepo uwezakano wa Tanzania
kuvamiwa na Nzige hao.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi
zinazoweza kuathirika na aina mbili za Nzige yaani Nzige Wekundu na
Nzige wa Jangwani hivyo tumejipanga kuwadhibiti wakitokea” alisema
Waziri wa Kilimo.
Waziri wa Kilimo amewataka
wataalam wa kilimo kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali
za Mitaa kuwasimamia Maafisa Ugani waliopo kwenye maeneo yao ili
kuhakikisha kwamba wanawatembelea wakulima mashambani na kubaini endapo
kuna viashiria vya uwepo wa Nzige.
Serikali itaendelea
kuhakikisha visumbufu vya mimea na mazao vinadhibitiwa ili wakulima
wavune mazao yao kwa wingi na nchi kuendelea kuwa na uhakika wa chakula.
Mwisho
No comments :
Post a Comment