Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete(JKCI) Prof. Mohammed Janabi akizungumza na Waandishi
wa Habari (hawapo pichani), kuhusu mafanikio ya Taasisi hiyo katika
miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, mkutano huo ulifanyika katika
ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dar es Salaam
Januari 28, 2020.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete(JKCI) Prof. Mohammed Janabi akizungumza na Waandishi
wa Habari (pichani), kuhusu mafanikio ya Taasisi hiyo katika miaka
minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, mkutano huo ulifanyika katika ukumbi
wa mikutano wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dar es Salaam Januari 28,
2020.
(Picha na Idara ya Habari-MAELEZO)
…………………
Serikali kupitia Taasisi ya Moyo
ya Jakaya Kikwete(JKCI) ikishirikiana na Serikali ya China wanatarajia
kujenga hospitali kubwa ya moyo katika eneo la Mloganzila ambapo hatua
za
awali za mchakato wa ujenzi zimekamilika.
Akizungumza katika Mkutano na
Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI,
Prof.Mohammed Janabi alieleza kuwa katika miaka minne ya Serikali ya
Awamu ya Tano taasisi hiyo imepanua huduma zake na kuboresha huduma za
matibabu ya moyo kwa kiwango cha kimataifa.
“Katika kipindi cha miaka
minne wagonjwa waliopatiwa huduma ni 300,836 ambao walitibiwa na kurudi
nyumbani na wagonjwa 14,960 ambao walilazwa kwa ajili ya kupata matibabu
zaidi, na mahitaji yanazidi kuongezeka hata kutoka katika nchi
jiraniani”, Alisema Prof.Janabi.
Alisema kuwa mahitaji ya
ujenzi wa hospitali kubwa ya Mloganzila yanatokana na kuwepo kwa
wagonjwa wengi nje ya nchi ambao wamekuwa wakija kupata matibabu kwa
hiyo uwepo wa hospitali hiyo kutaimarisha utoaji huduma za matibabu ya
moyo hapa nchini.
Katika kipindi cha Miaka minne
ya Serikali ya Awamu ya Tano JKCI imeweza kufanya upasuaji mkubwa kwa
kusimamisha moyo kwa wagonjwa 1,537 kwa mafanikio makubwa huku vifo
vikiwa ni asilimia 6 tu sawa na wagonjwa 92 kitu ambacho kinawashawishi
nchi jirani kama Uganda, Rwanda, Malawi, Burundi na Congo DRC kuleta
wagonjwa wao kwenye Taasisi hiyo.
Prof.Janabi alisema kuwa uwepo
wa vifaa vya kisasa na wataalam waliobobea kumewezesha zoezi la
upasuaji kuwa salama, ambapo upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo
linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa cathlab
(catheterization), wagonjwa 4,207 walipata huduma hiyo huku vifo vikiwa
ni asilimia 1.3 tu sawa na wagonjwa 42.
“Katika kipindi cha miaka
minne huduma za JKCI zimeweza kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 86 kwa
kufanya upasuaji kwa wagonjwa 5,744 ambao wangeenda kutibiwa nje ya nchi
kutokana na uwepo wa vifaa vyenye uwezo mkubwa, hususani kwenye masuala
ya upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo” Alisema Prof.Janabi.
Aidha katika kipindi hiki cha
miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, JKCI imeongeza ujuzi wa
wataalam ambapo kwa sasa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa
kutoa matibabu ya moyo yaliyo salama na kwa wagonjwa wengi ikitanguliwa
na Afrika ya Kusini
Aliongeza kuwa JKCI
imefanikiwa kufanya upasuaji wa moyo kwa mtoto mdogo mwenye umri wa siku
7 na mzee mwenye umri wa miaka 101 ambao kwa sasa wagonjwa hao wote
wawili wanaendelea vizuri na maisha yao.
“katika kukabiliana na
changamoto ya idadi kubwa ya wagonjwa, Rais John Magufuli mwezi Januari
2019 alitoa nafasi kwenye jengo la watoto lililopo katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili kwa ajili ya kliniki za watoto tu”, Alisema Prof.
Janabi.
Prof.Janabi alisema kuwa JKCI
imenunua mashine mpya mbalimbali za matibabu ya moyo zikiwemo mashine za
kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi, mfumo wa umeme wa moyo
unavyofanya kazi, ventilators, cardiac monitors, test gears, mashine ya
X-ray pamoja na vifaa vya chumba cha tatu cha upasuaji.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) ni hospitali kuu maalum kwa ajili ya matibabu ya moyo
inayomilikiwa na Serikali ambayo ilianzishwa Septemba 2015,ambayo
imeendelea kuitangaza vyema nchi yetu hata katika nje ya mipaka yetu.
No comments :
Post a Comment