Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
akimshika kobe, wanaohifadhiwa katika hifadhi ya Jozani, mkoani Kusini
Unguja. Januari 17, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
******************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewaagiza wadau wa masuala ya utalii nchini wafanye
mapitio ya gharama za huduma wanazowatoza watalii na amesisitiza kuwa si
sahihi kuwatoza wazawa kwa kutumia fedha za kigeni au gharama sawa na
wageni.
Aliyasema hayo
jana (Ijumaa, Januari 17, 2020) wakati akizungumza na wanachama wa
Umoja
wa Wenye Mashamba Jozani (UWEMAJO) mara baada ya kukagua miradi ya
umoja huo.
Waziri Mkuu
alisema kuwa kuna baadhi ya maeneo ya kutolea huduma za kitalii wazawa
wanatozwa gharama sawa na wageni. Hivyo, aliwasisitiza waandae viwango
maalumu kwa ajili ya wazawa ili kuhamasisha utalii wa ndani.
Alisema ni lazima
wadau hao wakatengeneza mazingira mazuri yatakayowavutia wazawa
kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii nchini. “Kitendo cha
kuwatoza wazawa gharama sawa na wageni kitasababisha baadhi kushindwa
kutembelea maeneo hayo.”
Akiwa katika eneo
hilo, Waziri Mkuu alisema amefurahishwa na namna ambavyo umoja huo
unavyotunza mazingira pamoja na viumbe maliasili nyingine kama kobe,
kasa, samaki na hivyo kulifanya eneo hilo kuwa kivutio cha utalii.
Kadhalika, Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi hao kuendeleza ushirika
wao huo kwa sababu utawawezesha kupata mikopo pamoja na misaada mingine
kama elimu kuhusu kilimo bora.
Waziri Mkuu
alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha wakulima wananufaika kutokana
na kilimo chao. Aliongeza kuwa ushirika unapaswa kuwa chachu ya
mafanikio, hivyo, amewapongeza wananchi hao kwa kuwa na ushirika imara.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu aliwasisitiza wananchi watumie ipasavyo vyandarua
vinavyotolewa na Serikali kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa malaria.
Aliyasema hayo wakati alipotembelea Kituo cha Afya cha Kizimkazi
Dimbani, Wilaya ya Kusini.
Waziri Mkuu akiwa
wilayani humo alishiriki maadhimisho ya Siku ya Afya ya Kijiji kwa
kugawa vyandarua kwa wanawake wajawazito. Wakati akigawa vyandarua
hivyo, alisisitiza umuhimu wa kutumia vyandarua kwa malengo
yaliyokusudiwa badala ya kuvitumia kama uzio katika bustani za
mbogamboga.
No comments :
Post a Comment