Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya
Biashara ya DCB, Zacharia Kapama (wa pili kushoto), akisoma hotuba yake
katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati
wa kutangaza taarifa za fedha ambapo alisema DCB imepata faida ya shs
bilioni 2.3 kwa mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 43 kutoka faida
ya mwaka 2018 ambayo ilikuwa shs bilioni 1.6. Wengine kutoka kushoto
ni; Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano, Rahma Ngassa, Mkurugenzi wa
Biashara, James Ngaluko na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Fortunata
Benedict, wote kutoka DCB.
………………………………………………………………………………………………….
Benki ya DCB yatangaza ukuaji wa faida wa asilimia 43 kwa mwaka 2019
Dar es Salaam; Januari 31, 2020
Benki ya biashara ya DCB (DCB
Commercial Bank Plc) imetangaza kupata faida ya
shilingi bilioni 2.3
katika mwaka 2019, ikiwakilisha ongezeko la asilimia 43 kutoka faida ya
mwaka 2018 ambayo ilikuwa shilingi bilioni 1.6.
Katika taarifa iliyotolewa kwa
vyombo mbalimbali vya habari leo tarehe 31 Januari 2020 na
iliyochapishwa katika magazeti kwa mujibu wa sharia za benki kuu,
utendaji wa benki umeendelea kuimarika ikilinganishwa na mwaka
uliotangulia huku ufanisi katika nyanja zote muhimu ukiongezeka kwa
kiwango cha kuridhisha.
Akiwakilisha taarifa za fedha za
robo ya nne ya mwaka 2019, mkurugenzi wa Fedha wa benki ya DCB Ndugu
Zacharia Kapama, ameeleza kuwa mafanikio haya yametokana na ukuaji wa
mizania ya benki, ambao umechagizwa na ukuaji wa amana za wateja kwa
asilimia 14 (Shilingi bilioni 10.1), ikilinganishwa na mwaka
uliotangulia.
Ukuaji wa amana umeisaidia benki
pia kuongeza ukuaji wa mikopo ambapo benki imefanikiwa kuongeza kiwango
ghafi cha mikopo kwa asilimia 11 (shilingi bilioni 8.0), ambacho ni
kiasi kikubwa ukilinganisha na ongezeko la mikopo katika miaka miwili
iliyotangulia. Mikopo ghafi ya benki imekua kutoka shilingi bilioni 90.5
mwaka 2018 kufikia shilingi bilioni 93.3 mwaka 2019.
Ili kufikia kiwango hiki, benki
imefanikiwa kutoa mikopo mipya kwa wateja wake kinachofikia shilingi
bilioni 60, huku shilingi bilioni 18 zikiwakilisha mikopo kwa
wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), na Shilingi Billioni 10
ikiwakilisha mikopo ya wanawake na vijana. Benki pia imeendelea kutoa
mikopo kwa sekta mbalimbali zikiwemo sekta binafsi za biashara, elimu
afya na ujenzi.
Akielezea upatikanaji wa faida,
Ndugu Kapama ameainisha kuwa ukuaji wa faida, ukiachilia mbali
kuchangiwa na ukuaji wa mizania, pia umechagizwa na ongezeko la mapato
yasiyotokana na riba baada ya benki kufanikiwa kukuza idadi ya wateja
wake kutoka 175,000 mwaka 2018 kufikia wateja 194,000 mwaka 2020.
Ongezeko hili limeongeza idadi ya akaunti za amana na miamala ya
kibenki, huku wateja wakifurahia huduma za kidijitali bila kwenda
matawini.
Kwa kuongezea, ufanisi wa benki
umeongezeka hasa katika usimamizi wa matumizi ya riba na yasiyo ya riba.
Benki imefanikiwa kudhibiti ukuaji wa matumizi yasiyo ya riba, huku
ikihakikisha huduma kwa wateja zinaboreshwa. Benki pia imefanikiwa
kudhibiti ongezeko la riba kwa wateja na kuhakikisha wateja wanapata
thamani bora ya huduma zake bila kuathiri ukuaji wake.
Katika taarifa hiyo, Ndugu Kapama
pia ameainisha upunguaji wa mikopo chechefu ya wateja kutoka asilimia 19
mwaka 2018 kufikia asilimia 13 mwaka 2019. Hii imetokana na juhudi za
benki kuhakikisha kuna ufanisi na usimamizi madhubuti katika utoaji
mikopo na ukusanyaji madeni. Benki itaendelea na juhudi za kuhakikisha
mikopo chechefu inafikia kiwango kinachokubalika na wadau wa sekta ya
fedha mnamo mwaka huu wa 2020.
Katika miaka yake takriban 17
ya uendeshaji, benki ya DCB imeweza kukuza idadi ya matawi kutoka tawi
moja na kufikia manane (8) hadi mwaka huu wa 2019. Pia imekuza idadi ya
wateja kufikia 194,000. Ukuaji huu umechangia benki kupata faida
mfululizo tangu mwaka 2004 hadi mwaka 2015, na imekuwa ikitoa gawio kwa
wanahisa wake katika kipindi chote cha miaka 12.
Hapo mbeleni, benki ya DCB,
inatazamia kukuza mizania yake kwa kutumia fursa za ukuzaji biashara na
ina azimia kutumia ipasavyo fursa na njia mbadala za utoaji huduma kwa
wateja kupitia mitandao, wakala wa kibenki, na upanuzi wa mitandao ya
matawi na vituo vidogo vya huduma ambapo itasaidia kwa kiasi kikubwa
utengenezaji wa mapato kupitia njia ya mapato yasiyo ya riba.
- Benki ya DCB ndio benki ya kwanza kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam huku ikiwa ndio benki pekee iliyokua kutoka benki ya wananchi/jamii (community bank) na kufanikiwa kuwa benki ya biashara (commercial bank)
- Benki ya DCB imefanikiwa kukuza mtandao wa matawi yake kufikia manane huku ikifungua tawi Dodoma na inaendelea na mchakato wa kufungua matawi na vituo vya huduma (service centers) katika mikoa mingine na imefungua mtandao wa mawakala na huduma za kijiditali hadi kufikia mawakala zaidi ya 700 nchini nzima.
- Benki imefanikiwa kuongeza mtaji wake kupitia soko la hisa kwa miaka yote 18 huku ikipata faida mfululizo na kujiimarisha kibiashara. Hivi sasa benki inao uwezo wa kutoa mikopo mikubwa zaidi na ya muda mrefu kwa wateja
- Benki imefanikiwa kuzindua mfumo wa akaunti za kidijitali ambapo umeiwezesha kuhudumia wateja wengi zaidi na kuwafikia hadi wale wa vijijini. Hii imeongeza ukuaji wa mapato na ongezeko la idadi ya wateja na ufanisi katika utoaji huduma
Akielezea maboresho zaidi ya huduma za kibenki yaliyofanyika, Mkurugenzi wa biashara Mr James Ngaluko alieleza:
- Benki imefanikiwa kuzindua huduma na bidhaa mpya kwa wateja wake ambazo ni Lamba kwanza (Fixed deposit), Akaunti ya Skonga, DCB sokoni, pamoja na garantii za wakandarasi zisizo na dhamana wakati wa kuomba tenda.
- Tumeboresha huduma ya mikopo ya nyumba ujenzi wa nyumba kwa kuongeza ushirikiano na Tanzania Mortgage Refinancing Company
- Tumeongeza ufanisi wa huduma ya mikopo kwa ushirikiano na taasisi ya ushauri FSDT, hivyo kufanya huduma ya utoaji mikopo kwa wateja kuwa ya haraka Zaidi.
- Benki imeboresha gharama zake kwa kuondoa gharama katika akaunti za community kama vikoba, akaunti za miradi ya serikali, na akaunti za wastaafu. Hii imepelekea kuongeza idadi kubwa ya wateja ambao wengi ni wa kipato cha cha chini na cha kati.
Benki ya Biashara ya DCB
ilianzishwa mwaka 2002 (Ikijulikana kama Dar es Salaam Community Bank)
kutokana na kilio cha wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam kutokuwa na
namna ya kupata mitaji midogo ya biashara jambo ambalo lilikuwa
changamoto kubwa kwa wajasiriamali wadogo wadogo katika jitihada za
kuboresha biashara zao sambamba na masharti magumu kutoka kwa benki
nyingi za kibiashara. Kwa kipindi chote cha miaka 17 ya uendeshaji,
jukumu mama la benki hii limeendelea kuwa ni kutoa huduma bora za
kifedha huku ikijikita zaidi katika kutengeneza miradi endelevu ya
kupunguza umaskini na kuendeleza jamii.
No comments :
Post a Comment