Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akifungua mkutano wa
Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo kilichofanyika jijini Dodoma leo
ambapo aliwataka kuwajibika ipasavyo mahali pa kazi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akiwasili katika
ukumbi wa mikutano kwa ajili ya kufungua mkutano wa Baraza la
Wafanyakazi wa Ofisi hiyo uliofanyika leo jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi
Joseph Sokoine akimkaribisha mgeni rasmi kwa ajili ya kufungua mkutano
wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo uliofanyika leo jijini Dodoma.
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la
Watumishi la Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwa katika mkutano wa Baraza la
Wafanyakazi wa Ofisi hiyo uliofanyika leo jijini Dodoma na kufunguliwa
na Waziri Mussa Azzan Zungu.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi
Joseph Sokoine (wa pili kulia) akiongoza mkutano wa Baraza la
Wafanyakazi wa Ofisi hiyo jijini Dodoma. Wengine pichani kuanzia kulia
ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Eva Mbigi, Mwenyekiti wa Baraza la
Wafanyakazi Isaya Kisiri na Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa Jane Mbura
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akiwa katika
picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo baada
ya kufungua mkutano leo jijini Dodoma.
………………………………………………………………………………………………………..
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu amemtaka kila
mtumishi katika Ofisi hiyo kuwajibika ipasavyo mahali pa kazi na
kuepuka
kujihusisha na vitendo visivyokuwa vya kimaadili.
Zungu ametoa kauli hiyo leo jijini
Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo
ambapo aliwakumbusha kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa
dhati kuimarisha utendaji kazi ili kufanikisha dhana ya Tanzania ya
viwanda.
“Ninafahamu kwamba watumishi wana
malalamiko yanayohusu kutopandishwa vyeo kwa muda mrefu na upungufu wa
watumishi katika Idara na Vitengo, malalamiko haya ni mtambuka katika
Wizara zote kwani yametokana na uhakiki wa vyeti vya elimu ya sekondari
na ualimu zoezi lililoendeshwa na Serikali kuanzia mwaka 2016.
Ninawasihi muwe na subira wakati Serikali ikiimarisha mifumo yake ya
Usimamizi wa Rasilimaliwatu,” alisisitiza.
Aidha, Waziri Zungu alibainisha
kuwa Baraza la wafanyakazi ni jukwaa muhimu mahali pa kazi kwani ni
kiunganishi kati ya Menejimenti na Wafanyakazi hivyo aliwataka
kuendeleza ushirikiano ili kuleta ufanisi katika kutekeleza majukumu ya
Ofisi na Taifa kwa ujumla.
“Watumishi wenzangu hakikisheni
mshahara mnaopewa mnautendea haki! Msitake kupata mshahara wa bure!
Fanyeni kazi kwa bidii” Zungu alisisitiza.
Aliongeza kuwa kuwepo kwa Mabaraza
ya Wafanyakazi katika Taasisi ni takwa la Kisheria kwa madhumuni ya
kuishauri Serikali katika ngazi za Idara na Ofisi ambapo malengo yake
ni kuhakikisha kuwa majukumu yanatekelezwa ipasavyo, kulinda haki na
wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa ushauri kuhusu kujenga mazingira
bora ya kazi, maslahi ya watumishi na kusimamia haki na ustawi katika
sehemu za kazi.
Aliwakumbusha kuwa wajibu wa
Mabaraza haya kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa
waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao na kuzingatia maadili
ya utumishi wao ili kuleta matokeo chanya katika utendaji kazi.
Agenda na madhumuni ya mkutano huu
ni kutoa Taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais
kwa kipindi cha nusu mwaka cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2019/20.
No comments :
Post a Comment