
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Eng.
Evarist Ndikilo akitoa maelekezo alipotembelea banda la Mfuko wa Fidia
kwa Wafanyakazi (WCF) kwenye maonesho ya viwanda yanayoendelea katika
viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Pwani.

Afisa Uwekezaji Mwandamizi Bw.
Michael Semiono akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Eng. Evarist
Ndikilo alipotembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF)
kwenye maonesho ya viwanda yanayoendelea katika viwanja vya Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa, Pwani.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Eng.
Evarist Ndikilo akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Mfuko
wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwenye maonesho ya viwanda yanayoendelea
katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Pwani. .

Afisa Uwekezaji Mwandamizi Bw.
Michael Semiono akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Eng. Evarist
Ndikilo machapisho ya WCF alipotembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa
Wafanyakazi (WCF) kwenye maonesho ya viwanda yanayoendelea katika
viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Pwani.
…………………………..
Na. Sarah Reuben
Wananchi waliotembelea Maonesho ya
Pili ya Viwanda mkoani Pwani wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa maboresho makubwa ya fidia kwa wafanyakazi wa
sekta binafsi na umma.
Akizungumza alipotembelea
banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Mhe. Eng. Evarist Ndikilo amesema tangu kuanzishwa kwake Mfuko huu
umekuwa faraja kwa wafanyakazi wengi hususan wafanyakazi wa viwandani.
“Binafsi niwapongeze sana WCF
kwa kuwa mnafanya kazi nzuri sana na hata wananchi wameendelea
kuipongeza sana Serikali kwa kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii hususan
malipo ya fidia kwa wafanyakazi. Hali hii imechangia kuongeza motisha
kazini na kuimarisha mahusiano kati ya mwajiri na wafanyakazi wake,”
alisema Eng. Ndikilo.
Eng. Ndikilo aliwaalika
wananchi kutembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ili kuongeza
uelewa kuhusu majukumu ya Mfuko huo ikiwemo taratibu za madai ili
kuepukana na usumbufu unaoweza kujitokeza pindi mfanyakazi atakapopata
ajali, ugonjwa au kifo kutokana na kazi.
Nao baadhi ya wajiri
walipotembelea banda la WCF wamesema wameongeza uelewa kuhusu masuala ya
fidia na mafao yanayotolewa na WCF.
“Mimi binafsi nilidhani bima
ya afya inagharamia matibu yoyote ya mgonjwa hata yale yanayotokana na
ajali au ugonjwa unaotokana na kazi lakini leo nimefahamu WCF ndiye
mwenye kulipa gharama za matibabu hayo,” alisema Dkt. Aden Mpangile
alipotembelea banda la Mfuko huo. Aliongeza kuwa, “Hapo awali sikufahamu
kuwa kiwango cha fidia anachostahili kulipwa mfanyakazi hujulikana
baada ya tathmini kufanyika kwa mfanyakazi aliyekamilisha huduma za
matibu ambayo kimsingi matibabu hayo hugharamiwa na Mfuko”.
Naye Afisa Uwekezaji
Mwandamizi Bw. Michael Semiono amesema WCF ni mdau mkubwa wa maonesho ya
viwanda ndio sababu Mfuko umeamua kushiriki kwenye maonesho haya ili
kukutana na wadau wake ikiwemo wafanyakazi na wamiliki wa viwanda
nchini. Katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya
Uchumi wa Viwanda, Mfuko umejielekeza kwenye miradi ya viwanda nchini
iliyopo mkoa wa Dodoma, Morogoro, Tanga na Simiyu alisema Afisa huyo.
Kuhusu mafao yatolewayo na
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Semiono amesema Mfuko unatoa mafao kadha
wa kadha ikiwemo huduma ya matibabu yanayotolewa kwa mfanyakazi
aliyepata ajali au ugonjwa utokanao na kazi. Aliongeza kuwa Mfuko
hugharamia huduma za ukarabati na ushauri nasaha pamoja na malipo ya
ulemavu wa muda au ulemavu wa kudumu kwa mfanyakazi aliyekamilisha
matibabu na kugundulika ana ulemavu huo.
Mafao mengine ni malipo kwa
mtu anayemhudumia mgonjwa iwapo daktari watathibitisha mfanyakazi
aliyepata ajali au ugonjwa kazini hawezi kujihudumia, msaada wa mazishi
na malipo kwa wategemezi iwapo mfanyakazi atafariki kutokana na kazi.
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi
unashiriki kwa mara ya pili kwenye maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia
wadau wengi zaidi ili kutoa elimu kuhusu taratibu za madai kwa
mfanyakazi aliyepata ajali, ugonjwa au kifo kutokana na kazi pamoja na
majukumu ya Mfuko kwa ujumla.
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi
ni Taasisi ya Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambao umeanzishwa kwa mujibu wa
Kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Na. 20 ya mwaka 2008.
No comments :
Post a Comment