
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akizungumza kwenye kikao
cha menejimenti ya Kiwanda cha Tanga Fresh na wanachama wa Chama Kikuu
cha Ushirika wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU)

Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akisikiliza kwa makini
baadhi ya hoja kwenye kikao cha menejimenti ya Kiwanda cha Tanga Fresh
na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa
Tanga (TDCU)

Mkuu
wa Mkoa wa Tanga Bw. Martine Shigella akizungumza kwenye kikao cha
menejimenti ya Kiwanda cha Tanga Fresh na wanachama wa Chama Kikuu cha
Ushirika wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU).
…………………..
Na. Edward Kondela
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo
na Uvuvi imeshtukia kusuasua kwa uendeshaji wa kiwanda cha Tanga Fresh
hali iliyolazimu kuundwa tume kufanya uchunguzi wa namna kiwanda
kinavyofanya kazi ikiwemo kuchunguza mtambo unaotumika kusindika maziwa
ya muda
mrefu ambao unadaiwa umekuwa ukiongeza gharama ya uendeshaji wa
kiwanda hicho.
Akizungumza jana (21.10.2019)
katika kiwanda cha Tanga Fresh mjini Tanga, kwenye kikao kilichohusisha
menejimenti ya kiwanda pamoja na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika
cha Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU) kinachomiliki
asilimia 43 ya kiwanda hicho.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amefafanua kuwa serikali itahakikisha
inachukua hatua kunusuru kiwanda kufuatia ziara ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alipotembelea kiwanda hicho
mwaka 2017 na kuahidiwa na menejimenti kusindika maziwa lita laki moja
kwa siku ambapo katika ziara hiyo Rais Magufuli aliwasaidia kupata hati
iliyokuwa imekwama kwa miaka mingi, kuondoa changamoto ya wanahisa juu
ya hisa zao Tume ya Ushindani (FCC) hali iliyopelekea kiwanda kuanza
kujitanua na kuongeza uzalishaji wa maziwa ya muda mrefu (UHT) ingawa
kiwanda kiliamua kuchukua mkopo Benki ya Biashara (NMB), unaoonekana
kuwalemea na kutofanya vizuri sawa na ahadi kwa Rais Magufuli.
“Kwanza serikali imebaini
manunuzi ya mtambo wa kusindika maziwa ya muda mrefu kuwa ni mtambo
uliyokwishatumika na umenunuliwa kwa zaidi ya Shilingi Bilioni Sita, pia
riba ya mkopo kuwa ni kubwa na kuwa mzigo, hivyo nimeagiza iundwe tume
ambayo tayari Mkuu wa Mkoa wa Tanga ameiunda kuanzia leo kufanya
uchunguzi wa mtambo ulionunuliwa ikiwemo fedha ya kununulia mtambo huo
na utaratibu uliotumika kununulia mtambo.” Amesema Mhe. Ulega
Aidha Mhe. Ulega ameitaka bodi
ya wakurugenzi wa kiwanda pamoja na wamiliki wakae pamoja na Benki ya
Kilimo (TADB) kuitaka benki hiyo kununua deni hilo ili kutoa nafuu kwa
kiwanda na kuondoa mzigo kwa wafugaji na kuinua kipato chao.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa
wa Tanga Bw. Martine Shigella amesema tayari timu ya wataalamu wakiwemo
kutoka Taasisi ya Utafiti wa Viwanda na Maendeleo (TIRDO) imeshaundwa
ili kubaini hali ya mtambo wa kusindika maziwa.
Bw. Shigella amefafanua kuwa
serikali itachukua hatua kwa yeyote atakayebainika kukihujumu Kiwanda
cha Tanga Fresh ikiwemo kununua mtambo wa kusindika maziwa usio na tija
kwa kiwanda hicho.
Nao baadhi ya wanachama wa
Chama Kikuu cha Ushirika cha Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga
(TDCU) wamepongeza hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi
pamoja na uongozi wa Mkoa wa Tanga kutafuta suluhu ya namna ya kuboresha
Kiwanda cha Tanga Fresh ili kiweze kuongeza uzalishaji na kuwanufaisha
wafugaji ambao wamekuwa wakiuza maziwa katika kiwanda hicho pamoja na
kutaka kiwanda hicho kiongeze bei ya kununua maziwa kutoka kwa wafugaji
hao ambao hawaridhiki na bei ya Shilingi 700 kwa lita moja.
Kikao baina ya Wizara ya
Mifugo na Uvuvi chini ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah
Ulega, uongozi wa mkoa wa Tanga, menejimenti ya kiwanda cha Tanga Fresh,
bodi na wamiliki wa kiwanda kinatarajiwa kuendelea hii leo (22.10.2019)
ili kutafuta suluhu ya kunusuru kiwanda hicho baada ya kupata hasara
kwa miaka mitatu mfululizo.
No comments :
Post a Comment