Tuesday, October 1, 2019

MAJALIWA AHUTUBIA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA WAZEE DUNIANI KITAIFA MJINI MTWARA




Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika Kitaifa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mjini Mtwara, Oktoba 1, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika Kitaifa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mjini Mtwara, Oktoba 1, 2019. Kulia ni Mkalimani wa lugha ya alama, Ally Nalinga Uwesu.(Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
………………..
WAZIRI MKUU amesema Serikali itaendelea kuwalinda wazee dhidi ya vitendo vya ukatili,
kuwawekea miundombinu na mazingira bora katika kutumia vyombo vya usafiri na kuweka utaratibu na vigezo vitakavyowawezesha kulipwa pensheni.
 Waziri Mkuu ameyataka mashirika ya wazee yaelekeze rasilimali wanazozipata katika kutoa huduma za msingi kwa wazee na waepuke kutumia fedha nyingi kwenye mikutano, warsha na makongamano ambayo hayawafaidishi moja kwa moja wazee wenye uhitaji.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Oktoba 1, 2019) wakati akihutubia wananchi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja Nangwanda Sijaona Manispaa ya Mtwara.
Amesema utoaji wa huduma kwa wazee ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli na kwamba itaendelea  kuchukua hatua za makusudi kwa lengo la kuboresha hali na maisha ya wazee nchini.
Amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha ustawi na maendeleo ya wazee ni pamoja na kuanzishwa kwa mpango wa TASAF wa kunusuru kaya masikini uliolenga kuyasaidia makundi mbalimbali ya jamii yanayoishi katika umasikini uliokithiri likiwemo kundi la wazee.
“Hadi kufikia Septemba 2019 jumla ya wazee 680,056 kutoka kaya 1,118,747 wananufaika na mpango wa TASAF kwa Tanzania Bara na Zanzibar. Mpango huu, umesaidia wazee kujikimu na kumudu majukumu ya kulea wajukuu ambao wazazi wao wamepoteza maisha kwa sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa ukimwi.” 

Amesema Serikali pia inaendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inatambua kuwa wazee ni kundi maalumu linalohitaji kupewa kipaumbele katika kupata huduma bora za afya, inaweka mkazo kuwa wazee wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea na wasiokuwa na uwezo watibiwe bila malipo. 
Hata hivyo, Waziri Mkuu ameendelea kuziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zoezi la kuwatambua na kuwapatia vitambulisho wazee wasiokuwa na uwezo linakuwa endelevu ili waweze kunufaika na huduma ya matibabu bila malipo  wanapougua. 
Kadhalika, Waziri Mkuu amevitaka vituo vyote vya kutoa huduma za afya vya umma kutoa huduma bora na za haraka kwa wazee wenye vitambulisho hivyo na watenge dirisha maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wazee ili wasikae kwenye foleni muda mrefu.
Akizungumzia kuhusu matunzo ya wazee, Waziri Mkuu amesema Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003 inatamka kuwa familia na jamii zina wajibu wa msingi wa kuwatunza na kuwahudumia wazee. 
“Hii ni kutokana na ukweli kuwa mazingira ya familia yanamuwezesha mzee kujiona sehemu ya jamii na hivyo, kumfanya aondokane na msongo wa mawazo unaotokana na upweke na kutengwa. Familia kwa mtazamo wa hapa nchini kwetu inajumuisha baba, mama, watoto pamoja na ndugu wengine.” 
 Waziri Mkuu ametoa  wito kwa familia, jamii na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutimiza wajibu wao wa kutoa matunzo na malezi kwa wazee wasiojiweza, hatua ambayo  itaonesha kuwa jamii inathamini mchango mkubwa walioutoa wazee kwa ustawi na maendeleo ya Taifa. “Vilevile, nisisitize kuwa jukumu la kuwatunza wazee ni la kila mmoja wetu, hivyo kila mmoja anawajibika kuwatunza wazee.”
“Nyote mtakubaliana nami kuwa matunzo ya wazee katika makazi hutolewa kwa wazee wasiojiweza na wasio na ndugu wa kuwatunza. Suala la kumpeleka mzee katika makazi ya wazee litakuwa ni kimbilio la mwisho baada ya njia nyingine zote za matunzo katika familia na jamii kushindikana.” 
Waziri Mkuu amewataka vijana  na jamii kwa ujumla wasikwepe jukumu la kuwatunza wazee kwa sababu bila wao wasingekuwa hivyo walivyo leo. Ikumbukwe kuwa wazee hao nguvu zao za uzalishaji mali zimepungua kutokana na kazi waliyoifanya wakiwa vijana kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa familia zetu na Taifa kwa ujumla. 
Pia, Waziri Mkuu ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa ziombe vibali vya ajira ili waajiri Maafisa  Ustawi wa Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii Wasaidizi ambao wanahitajika kufanya kazi  kuanzia ngazi za Kata hadi Halmashauri ikiwemo kushughulikia changamoto za wazee katika jamii.
Pia, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iendelee kuimarisha na kusimamia Mabaraza ya Wazee ili yashiriki kikamilifu kuelimisha familia na jamii kutimiza wajibu wao wa kutunza wazee.
Pia, Waziri Mkuu ametaja changamoto zinazowakabili wazee ni pamoja na vitendo vya mauaji ya wazee kutokana na imani za kishirikina. “Napenda kurudia Wito kwa jamii kuhusu kuongeza mapambano ya kutokomeza vitendo vya mauaji kwa wazee wasiokuwa na hatia. Wakuu wa mikoa na wilaya waweke utaratibu maalumu wa kuwalinda wazee.” 
Awali,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya wazee ikiwa ni pamoja na kutafakari fursa za changamoto zinazowakabili wazee na namna ya kuzitatua.
Waziri Ummy alisema kupitia maadhimisho hayo jamii inakumbushwa kuzingatia kwa kutekeleza kwa umuhimu haki za wazee na wazee nao wanakumbushwa wajibu wao kwa wajibu wao kwa jamii. Sens aya watu na makazi ya 2012 Tanzania inakadiriwa kuwa na wazee 2,507,568 sawa na asilimia 5.6 ya wananchi wote.
Alisema taarifa kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, hadi Desemba 2018 jumla ya wazee 1,837,162 wametambuliwa na kati yao wazee 684,383 sawa na asilimia 37 ya wasiokuwa na uwezo wamepatiwa vitambulisho vinavyowawezesha kupata huduma za matibabu bila ya malipo. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 319 mara tatu zaidi ya idadi ya wazee 214,370 waliopewa vitambulisho vya matibabu kwa 2016/2017.

No comments :

Post a Comment