Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akisalimiana na Miss Tanzania 2019, Sylivia Sebastian, nje ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Mlimwa, jijini Dodoma, Septemba 11.2019. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu).
************************
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
amemtaka Miss Tanzania 2019, Sylivia Bebwa (19) ahakikishe anakuwa
balozi mzuri wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, shughuli
za
maendeleo zinazofanywa na Serikali na aishi kwa kuzingatia utamaduni
wa Mtanzania.
“Miss Tanzania lazima awe
mbunifu na uelewa mpana katika masuala mbalimbali zikiwemo jitihada
zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo ya wananchi kama
kuhamasisha elimu hususan kwa watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto
zao.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Jumatano, Septemba 11, 2019) wakati alipokutana na Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, waandaaji wa
mashindano ya Miss Tanzania, Miss Tanzania na mshindi wa pili na watatu
wa shindano hilo, ofini kwa Waziri Mkuu Mlimwa jijini Dodoma.
Amesema Miss Tanzania
anatakiwa kutumia fursa hiyo kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii
vilivyopo nchini, shughuli zinazofanywa na Serikali katika kukuza uchumi
pamoja na kuhamasisha wananchi washiriki katika kufanya kazi kwa ajili
ya maendeleo yao na Taifa.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema
Miss Tanzania pamoja na washiriki wengine wa mashindano hayo wanatakiwa
waishi kwa kuzingatia utamaduni wa Mtanzania ikiwemo kuwa na nidhamu
katika jamii ili waweze kuwashawishi wengine kushiriki.
Waziri Mkuu amempongeza Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Mwakyembe kwa namna
anavyoratibu shughuli mbalimbali katika wizara hiyo. “Hata katika sekta
ya michezo viwango vimeanza kuonekana.”
Waziri Mkuu amesema Serikali
inaunga mkono masuala ya michezo na inapenda kuona viwango vinapanda,
hatua ambayo itawawezesha wahusika kufanya vizuri katika mashindano
mbalimbali wanayoshiriki.
Kwa upande wake, Waziri Dkt.
Mwakyembe amemshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuonana na ujumbe huo
hususani Miss Tanzania ambaye anajiandaa kwenda kushiriki katika
mashindano ya Miss World yanayotarajiwa kufanyika London, Uingereza
Desemba 14 mwaka huu.
Waziri huyo amesema miaka ya
nyuma Serikali haikuridhishwa na namna mashindano hayo yalivyokuwa
yakiendeshwa lakini kwa sasa hali ni tofauti na yamekuwa na viwango vya
kimataifa. Mashindano hayo kwa sasa yanasimamiwa na aliyekuwa Miss
Tanzania 2008, Basilla Mwanukuzi kupitia kampuni ya The Look.
Naye,Mwandaaji wa Mashindano
hayo, Basilla Mwanukuzi ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa
ushirikiano inaoutoa kwao na pia ameiomba izidi kuwaunga mkono kwa kuwa
watatumia mashindano hayo katika kulitangaza Taifa.
Awali, Miss Tanzania 2019,
Sylivia ameishukuru Serikali kwa fursa aliyopewa ya kukutana na Waziri
Mkuu na alisema kuwa atajitahidi katika kuhakikisha anatekeleza majukumu
yake ipasavyo ikiwemo kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Miss
World na kwamba anakwenda kutumia lugha ya kiswahili.
“Nimefurahi kwa heshima hii
niliyopewa na Serikali ya kukutana na Mheshimiwa Waziri Mkuu, naahidi
kwamba niyatekeleza maagizo yote aliyoyatoa ikiwa ni pamoja na kuishi
kwa kuzingatia maadili ili wazazi wengine waweze kuwaruhusu watoto wao
washiriki katika mashindano haya kwani urembo ni heshima.”
No comments :
Post a Comment