Thursday, August 1, 2019

WAZIRI UMMY AAGIZA WAAJIRI KOTE NCHINI KUTOA LIKIZO YA KUNYONYESHA AKINA MAMA NDANI YA SIKU 84



Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Waziri wa  Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu ametoa agizo kwa waajiri kote nchini kuendelea kuwapa likizo ya kunyonyesha  ndani ya siku 84   akina mama   mara wanapojifungua kama ilivyo kwa mujibu wa Sheria. 


Waziri Ummy ametoa maagizo hayo leo Agosti 1,2019  jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya  wiki ya unyonyeshaji duniani  ambayo yameanza Agosti 1 hadi 7,2019. 


Mhe.Ummy amesema mama aliyejifungua ana haki ya kupewa likizo ya siku 84 hivyo ni wajibu wa kila mwajiri kutoa likizo kwa waajiri na mwajiri anayekiuka maagizo hayo ni mwajiri adui wa wanawake na watoto wa Tanzania na serikali haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria. 


Aidha,Waziri Ummy amefafanua mchanganuo wa likizo ambapo amesema mama aliyejifungua mtoto mmoja anapaswa kupewa likizo ya siku 84 na aliyejifungua mapacha anastahili kupata likizo ya siku 100 ,baba mzazi ana haki ya likizo ya siku tano huku pia akitoa tahadhari ya kuifuta sheria kwa akina baba kwani baadhi yao wamekuwa wakitumia mwanya huo kushinda baa na vijiweni badala ya kumsaidia mama.
Waziri Ummy ameongeza kuwa kanuni za utumiaji wa Maziwa ya watoto  ya kopo,maelekezo yanatakiwa  kwa lugha zote mbili Kishwahili na kiingereza ili mtu wa kijijini aelewe namna ya matumizi. 


Pia waziri Ummy amesema asilimia 31% ya watoto waliochini ya miaka 5 wamedumaa  kutokana na kukosa maziwa ya mama huku akitaja baadhi ya faida za unyonyeshaji kuwa ni pamoja na hali ya lishe kwa watoto kuwa nzuri,kuondoa uwezekano wa saratani ya matiti na uzazi kwa akina mama,kupungua udumavu na utapiamlo kwa watoto .
Kwa upange wake ,Mwakilishi wa shirika la kuhudumia watoto Duniani  [UNICEF]hapa nchini,James Gitau amesema asasi za kiraia zinapaswa kuendelea kutengeneza mazingira ya Unyonyeshaji katika maeneo ya kazi  huku akiishukuru serikali ya Tanzania  kwa kuendelea kuwawezesha wazazi  kwa kuwatengenezea mazingira rafiki ya unyonyeshaji   .
Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji Duniani hufanyika kila ifikapo tarehe 1 hadi 7 ya kila  mwaka na kaulimbiu mwaka huu ni “Wawezeshe wazazi kufanikisha unyonyeshaji”huku takwimu zikionesha kuwa asilimia 97% ya watoto walio chini ya umri wa miaka 2 wananyonyeshwa maziwa ya Mama  na hali ya unyonyeshaji Tanzania ikipungua kwa asilimia 1% ambapo sawa na watoto elfu 20 hawanyonyeshwi.

No comments :

Post a Comment