Makombora
yaliyorushwa na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran katika mji
wa Aden ulio kusini mwa Yemen pamoja na mashambulizi kadhaa ya kujitoa
muhanga yameuwa zaidi ya wanajeshi 60 na kuwajeruhi wengine kadhaa.
Shahidi
mmoja aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba aliona miili tisa
baada ya mripuko kutokea kwenye kambi ya kijeshi inayomilikiwa na kikosi
maalum cha Yemen kinachoungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu,
ambayo imo kwenye muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia
kupambana na Wahouthi.
Kwa
mujibu wa chanzo kimoja cha hospitali, miongoni mwa watu 51 waliouawa,
yumo kamanda wa kijeshi. Chanzo chengine kilicho karibu na jeshi la
serikali kimemtambua kamanda huyo kuwa Brigedia Jenerali Muneer
al-Yafee, mmoja wa viongozi wakubwa wa kijeshi kusini mwa Yemen.
Yafee
alikuwa ndio kwanza ameshuka jukwaani kumuamkia mgeni rasmi wakati bomu
liliporipuka. Kwenye gwaride hilo, bendera za zamani za iliyokuwa Yemen
Kusini na zile za makundi yanayounga mkono ushirika wa kijeshi dhidi ya
Wahouthi zilikuwa zimetanda, huku bendi ya kijeshi ikitumbuiza.
Mashahidi
wanasema wanajeshi walisikika wakipiga makelele na kuwakimbilia
waliojeruhiwa kuwawahisha hospitalini. Sare, viatu, na vifaa vyengine
vya kijeshi vilikuwa vimechawanyika aridhini na huku vikiwa vimetapakaa
damu.
Shirika
la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka (MSF) lilituma taarifa kupitia mtandao
wa Twitter kwamba makumi ya watu waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu
mjini Aden baada ya mripuko huo, lakini baadaye shirika hilo lilisema
kwamba mashambulizi mengine tafauti yalifanyika kwenye kituo kimoja cha
polisi kusini mwa mji huo wa bandari. Taarifa hiyo ilisema watu kumi
waliuawa na wengine 16 kujeruhiwa.
Kituo
rasmi cha televisheni kinachoendeshwa na Wahouthi, Al Masirah, kilisema
kundi hilo lilifanya mashambulizi kwa kutumia makombora ya masafa ya
kati na ndege isiyo rubani dhidi ya gwaride hilo la kijeshi, ambalo
kimesema lilikuwa ni matayarisho ya uvamizi dhidi ya majimbo
yanayoshikiliwa na kundi hilo.
Chanzo
chengine kimeliambia shirika la habari la AP kuwa bomu liliripuka nyuma
ya jukwaa ambalo sherehe zilikuwa zikifanyika kwenye kambi ya kijeshi
ya Al Jalaa wilaya ya Buraiqa.
Muungano
unaoungwa mkono na mataifa ya Magharibi ukiongozwa na Saudi Arabia na
Umoja wa Falme za Kiarabu uliingia kijeshi nchini Yemen mwaka 2015 kwa
madai ya kuirejesha madarakani serikali inayotambuliwa kimataifa
iliyokuwa imepinduliwa mwaka 2014 mjini Sanaa na Wahouthi.
Hata
hivyo, wengi wanasema lengo la uvamizi huo wa kijeshi lilikuwa ni
kuizuwia Iran kujipenyeza kwenye taifa hilo masikini la Kiarabu kupitia
utawala wa Kihouthi, ambao nao ni sehemu ya madhehebu ya Shia.
No comments :
Post a Comment